Botswana hakukaliki kwa ukimwi


Zakaria Malangalila's picture

Na Zakaria Malangalila - Imechapwa 23 November 2011

Printer-friendly version

TAIFA kubwa Kusini mwa Afrika la Botswana, linatokomea kwa maradhi ya Ukimwi. Botswana lenye watu 1.7 milioni ina kiwango kikubwa cha ukimwi duniani – karibu asilimia 40 ya watu wake wenye umri mkubwa wana maambukizi; na waathirika ni asilimia 25.

Hii ina maana kwamba katika kila watu wazima wanne nchini humo, mmoja tayari ni muathirika na anapatiwa dawa za ARV.

Kutokana na hali hii, urefu wa maisha ya mtu umepungua na kufikia chini ya miaka 40 kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1950.

Ukimwi umeenea kwa kasi nchini humo kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa biashara ya ukahaba katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, hali iliyosababisha nchi hiyo kutunga sheria kali dhidi ya biashara hiyo.

Botswana ilikuwa ni nchi ya kwanza Barani Afrika kutoa dawa za ARV bure kwa wananchi wake; ikafanya kampeni kabambe za dhati kupambana na gonjwa hilo. Taifa hili linalotajwa kuwa na demokrasia halisi na utawala bora, ina utajiri wa madini ya almasi ambao unasimamiwa vizuri.

Wachunguzi wa mambo wanasema, ikiwa kampeni ya Botswana ya kutokomeza ukimwi itafeli, basi kuna matumaini madogo sana kwa nchi zingine ambazo ni masikini barani humu kufanikiwa.

Madini ya almasi yaligunduliwa nchini Botswana mara tu baada ya nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa Waingereza mwaka 1966. Tofauti na jirani zake Angola, madini hayo yameleta maendeleo makubwa nchini humo, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya bure katika ngazi zote.

“Ukimwi unalimalizia taifa hili nguvu kazi hasa kwa vijana na inakula sana pato la taifa,” anasema Dk. Banu Khan, mkuu wa kitengo cha uratibu wa ukimwi nchini humo.

Anasema, “Tunakabiliwa na kufutwa na kutokomea kabisa kwa taifa letu.”

Angalia takwimu hizi: Wataalamu wanasema Botswana ina aina “C” ya ukimwi – yaani ukimwi ule ambao maambukizi yake ni sugu sana kuliko aina nyingine mbili, yaani “A” na “B”.

Nchi zilizoendela zina aina “B” ya usugu na Afrika Mashariki (ikiwemo Tanzania) ni mchanganyiko wa aina “A” na “B.” Lakini aina “C” ndiyo sugu na kasi ya zaidi kuenea na ambayo ndiyo inayotishia kulipuka China na India.

Kwa ujumla, hali ya ukimwi Botswana inatisha sana hali iliyosababisha baadhi ya viongozi nchini humo kuliangalia upya suala zima la ukahaba na ngono. Kuna wito wa kutaka kuhalalisha ukahaba nchini humo – yaani isiwe makosa kabisa kwa wanaoshiriki, kama ilivyo sasa.

Wazo la kuhalalisha ukahaba limetolewa na rais wa zamani wa nchi hiyo, Festus Mogae ambaye hivi sasa ni mwenyekiti wa Baraza la Ukimwi nchini humo. Amepanga kulipeleka suala hilo katika kikao kijacho cha Baraza la Mawaziri na na hatimaye Bungeni.

Anasema iwapo ukahaba utahalalishwa, basi itawafanya makahaba waweze kuzuia maambukizi ya ukimwi.

Kuhalalisha ukahaba haina maana kuuendeleza, lakini itatoa njia kwa upatikanaji wa sera na sheria zitakazowalinda wale ambao wanalazimishwa kuingia katika biashara hiyo bila ya ridhaa zao, Mogae amenukuliwa akikiambia kikao kimoja cha Baraza la Ukimwi wiki iliyopita.

Amesema iwapo makahaba watalindwa na sheria itakayowekwa,  wanaweza kuwa wanawaripoti wale wanaume ambao huwalazimisha kufanya ngono na kuwaweka katika hatari ya maambukizi ya ukimwi; jambo ambalo litawafanya wanaume hao kuogopa kuwashawishi au kuwalazimisha kufanya ngono na hasa ile isiyo na kinga.

Pamoja na sheria kuweka sheria kali, ukahaba nchini Botswana umeshamiri. Hii inatokana na kwa kiasi kikubwa kujikita kwa rushwa katika suala hilo.

Vitendo vya ukahaba na ngono, ikiwemo ngono zembe, vimeshamiri kwenye miji na vituo vya barabara kuu kati ya nchi jirani ya Afrika ya Kusini na Botswana. Barabara hiyo ndiyo windo kubwa la polisi kukimbizana na makahaba na mabwana zao; lengo si kuwakamata, ni kutafuta fedha za rushwa ambazo huzipata kwa urahisi.

Kuna baadhi ya mashuhuda wanasema, pale ambapo hakuna pesa, polisi huomba rushwa hata ya ngono – hali ambayo imelifanya jeshi la polisi nchini humo kuwa na maambukizi makubwa ya ukimwi.

Chama tawala nchini Botswana ambacho hapo zamani Festus Mogae alikiongoza, bado hakijachukuwa msimamo kuhusu pendekezo lake. Lakini kiongozi wa upinzani, Botsalo Ntuane amesema anaunga mkono pendekezo hilo kwa asilimia 100 kama njia muafaka ya kupunguza maambukizi ya ukimwi nchini humo.

Hata hivyo, pendekezo linaonekana kupata pingamizi kubwa kutoka kwa makundi ya dini nchini.

Padri William Horlu ambaye ni msemaji wa Kanisa katoliki nchini humo anasema, “Kutokana na maadili ya Kikristu, ngono ni kwa ajili ya watu waliomo katika ndoa kwa lengo la kuzaliana.”

Anasema ni dhambi kufanya ngono kwa ajili ya kutafuta fedha; Botswana kama nchi ya Kikristu haiwezi kamwe kuruhusu kuhalalishwa kwa ukahaba.

Kwa upande wake, Mogae ambaye pia anataka kuondolewa kwa sheria inayokataza ulawiti, anajibu kwa kusema makatazo ya kidini hayajasaidia kitu.

Anasema, “Italia ni nchi ya Kikatoliki inayojulikana sana katika biashara ya ukahaba. Pia talaka inaruhusiwa kwa Waislamu, ingawa wao wana taratibu na kanuni kali kuhusu suala hilo. Hivyo basi, sisi hatuwezi kuzungumza kwa namna makanisa yanavyozungumza kwa sababu historia inaonyesha wito wa kanisa umeshindwa.”

 Rais huyo wa zamani anaungwa mkono pia na Mtandao wa Maadili, Sheria na Ukimwi nchini mwake.

Uyapo Ndadi, Mkurugenzi wa chama hicho anasema kuharamisha biashara ya ukahaba kunawaweka makahaba katika hali ya kuingiliwa kwa nguvu pasipo ridhaa na pia maambukizi.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)