Botswana: Mfano mzuri wa mafanikio Afrika


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 November 2009

Printer-friendly versionSend to friend

HAISHANGAZI kukuta Botswana ikiongoza nchi zinazoendeshwa vizuri zaidi barani Afrika. Tangu ilipopata uhuru mwaka 1966, imekuwa ikifanya uchaguzi wa viwango vikubwa ndani ya mfumo wa vyama vingi.

Iliongozwa na baba wa taifa, Sir Seretse Khama, akafuatiwa na viongozi watatu wazuri, akiwemo mwanawe, Ian, ambaye amechaguliwa tena hivi karibuni.

Ina akiba kubwa ya almasi na serikali zote zimetumia vizuri maliasili. Pato la wastani limeongezeka mara tatu katika miongo miwili (miaka 20) na kuiweka Botswana katika kiwango sawa na Mexico cha ukuaji wa uchumi.

Vipo vigezo vya kuthibitisha mfano mzuri wa Botswana kimafanikio. Ina bahati kubwa katika kutumia utajiri wa madini, ikianzia na matatizo yalipokuwa yakichimbwa na De Beers, kampuni ya Afrika Kusini.

Ikiwa na kiasi cha watu 2 milioni tu, Botswana haina tatizo la watu wa makabila mengi, tofauti na nchi nyingi za Afrika zinazotambua mipaka iliyokatwa na wakoloni.

Walakini imekuwa na mashaka yake. Moja ni la kukabiliwa na tatizo la ugonjwa wa ukimwi. Imekosa ustaarabu kwa kutovumilia mienendo ya kale ya watu wachache wa kabila la Bushmen.

Kushuka kwa bei ya almasi katika soko la dunia, kumeathiri mapato ya almasi ya Botswana kiasi cha kusababisha kupungua kwa Pato la Taifa (GDP) kwa asilimia 0.10.

Pamoja na yote hayo, viongozi waliopo madaranai hawajapata changamoto kubwa ya kiuongozi kutokana na udhaifu wa upinzani; kama vile inaendeshwa kwa mfumo wa chama kimoja tu tangu uhuru.

Hiyo ni moja ya sababu zilizoifanya Ghana kuonekana ndio mfano mzuri wa nchi iliyopiga hatua zaidi Afrika katika medani ya maendeleo na demokrasia.

Uthibitisho ni kauli ya pongezi aliyoitoa Rais Barack Obama wa Marekani alipoichagua kuanza kuitembelea wakati wa ziara yake ya nchi tano za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara mwaka huu; baada ya serikali kukubali kushindwa uchaguzi.

Ghana imepata sifa kwa kuendeleza utamaduni wa viongozi kubadilishana madaraka baada ya matokeo ya uchaguzi ya vyama viwili kukaribiana mno.

Afrika Kusini, taifa lenye nguvu zaidi kiuchumi Afrika, ambako demokrasia imestawi vizuri na taasisi za kidola zinafanyakazi vizuri, hakujawa na upinzani mkubwa dhidi ya Chama cha African National Congress (ANC).

Jaribio kubwa la kuendeleza demokrasia litakuja pale ANC itaposhindwa uchaguzi. Kwa Botswana, watu wake wamechagua tena chama tawala. Na wala hawajisikii wameonewa.

Kwa miaka yote nchi yao imetia fora katika kuheshimu misingi ya utawala bora na kuwa mfano mzuri kwa mataifa yaliyotangulia kupata uhuru. Mengine yaweza kufuata?

Kuotesha mizizi ya demokrasia Afrika si kazi rahisi. Viongozi wake wengi wanachukulia upinzani ni usaliti. Mara nyingi vigogo wa Afrika hudhani ni safi baada ya kuendekeza uchaguzi wa ovyo, kama uliofanyika Kenya Desemba 2007 na Zimbabwe mwaka jana ili kutaka walioshindwa waunde serikali ya umoja wa kitaifa na wale walioshinda.

Lakini hii huleta utulivu wa muda mfupi tu; wakati huohuo kuwezesha watawala kujipanga upya kwa nia ya kuendeleza madaraka.

Uchaguzi si kila kitu ingawa una maana kubwa. Ila mazoea ya demokrasia yanaimarika taratibu. Yalianza mwaka 1991 nchini Benin, miongo minne baada ya nchi nyingi kupata uhuru; kwamba kiongozi yeyote akubali kuondoka madarakani kwa amani kupitia uchaguzi iwapo atashindwa.

Tangu hapo, hata hivyo, angalau viongozi tisa wamekubali mazoea hayo – ambayo ni rekodi nzuri, kulinganisha na ilivyo katika bara Arabu.

Demokrasia ni zaidi ya uchaguzi. Inahitaji mahakama huru, utumishi wa umma usiopendelea chama tawala, taasisi huru za kijamii kama kanisa na vyuo vikuu; utawala wa sheria na haki ya kumiliki mali; vyombo huru vya habari; ufuataji katiba; na zaidi utamaduni wa uwazi na uvumilivu, hususan kwa walio wachache.

Lakini uwezo wa wapiga kura kukataa serikali iliyo madarakani bado ni mtihani mkubwa.

Uzuri, unafiki uliozoeleka sana Afrika unabainika. Moja ni serikali za kidikteta na za chama kimoja zinafanikiwa kujenga nidhamu katika kubadilisha uchumi. China ni mfano mzuri, wengine wanasema.

Utafiti uliobainishwa hivi karibuni na wasomi wawili wa Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza, unabeza mtizamo huo, siyo tu kwa Afrika.

Utafiti huo unasifia mwenendo mwingine mzuri Afrika, wa kuweka mfumo wa ukomo wa uongozi. Utaratibu mwingine wa kuchochea demokrasia imara, unaokubalika na nchi nyingi Afrika, ni wa kuweka wazi mienendo ya kiutendaji ya serikali na makampuni makubwa wanayoshirikiana nayo.

Kuna safari ndefu kwa nchi nyingine kuifikia Botswana. Tuzo ya Mo Ibrahim inayotolewa kwa kiongozi bora mstaafu Afrika, imekosa wa kupewa mwaka huu wa 2009. Ni tuzo iliyolenga kuinua utawala bora Afrika ikiwa imeanzishwa na tajiri mzaliwa wa Sudan, Mohammed Ibrahim.

Bado Waafrika wengi wanaamini kupata fursa ya kuchagua viongozi wao si kitu kikubwa katika kuifanya nchi ipate demokrasia na uchumi bora. Lakini Botswana imeonyesha kinyume.

            *Makala hii imetafsiriwa na Mwandishi Wetu, kutoka Shirika la Habari la Kifaransa - AFP.

0
No votes yet