Bunda walalamikia kiwanda


Anthony Mayunga's picture

Na Anthony Mayunga - Imechapwa 30 November 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

KIWANDA cha kutengeneza mafuta cha Bunda Oil Industries kimepenyeza rupia kuondoa udhia uliokuwa unakizingira kiwanda hicho.

Wananchi wamekuwa wakilalamikia kiwanda hicho tangu kilipoanzishwa tarehe 26 Agosti 2009.  Kufuatia malalamiko hayo, Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC) liliandika barua kuiagiza menejimenti ifanye mambo mawili; kwanza isimamishe shughuli zake halafu isimike mtambo wa kuchuja maji. NEMC ilikipa kiwanda hicho miezi minane kushughulikia suala hilo .

Wakati NEMC wanaandika barua ya kufunga kiwanda kwa barua yenye Kumb NEMC/04/VOL.12/30 walitumia sheria ya mazingira ya mwaka 2004 kifungu cha 81 kifungu kidogo (1)-(4).

Lakini NEMC haohao, tarehe 4 Novemba 2009 miezi mitatu tu, waliandika barua nyingine kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kutengua uamuzi wa awali na kuruhusu kiwanda kuendelea na kazi zake.

Barua ya kuruhusu shughuli yenye kumb, NEMC /04/ VOL.12/39 ilitiwa saini na Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Robert Ntakamulenga kwa madai kiwanda kimejitahidi kurekebisha matatizo.

Matokeo yake, tarehe 6 Novemba 2011 maji ya magadi aina ya caustic soda yalivuja na kuingia kwenye mashamba ya mpunga na mtama ya wakazi wa Migungani na Tairo. Ekari 54 zimeharibiwa.

Vilevile, maji hayo yanayochoma yaliingia katika Mto Kyandere ambao ni chanzo cha maji kwa matumizi ya binadamu na mifugo kwa wakazi wa vijiji hivyo na mwishowe humwaga maji  hayo katika Ziwa Victoria .

Sababu zilizoainishwa mwaka 2009 ndizo zilizochangia maji kuvuja safari hii. Kwamba mabwawa yanayotakiwa kuhifadhi maji hayo ya sumu yalijaa na kuvuja kwenda kwenye mashamba ya watu.

Hakuna madhara yaliyobainika kwa binadamu na mifugo lakini mashamba yaliyoathiriwa yanamilikiwa na Marwa Gikaro, Kichere Gikaro, Rhobi Nyikondo, Max Gikaro, Makoye Laurent, Nyerere Gikaro, Felix Sura Kichere, Samo Gikaro, Marwa Nyamatwi, Matinde Juma, Bhoke Gikaro, Mhere Marwa na Bhoke Range.

Katika ukaguzi uliofanywa tarehe 2 Julai 2009 wataalamu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, kanda ya Ziwa Victoria , Anna Mdamo na Afisa Mazingira, Edika Masisi walibaini kiwanda hicho hakikuwahi kufanyiwa tathmini ya athari ya mazingira (Environmental Impact Assessment (EIA) tangu kuanza kwa uzalishaji, wala Uhakiki wa Mazingira (Environmental Audit).

Wakazi wa vijiji hivyo wamekuwa wakikilalamikia kiwanda hicho tangu mwaka 1997 wakati kikiitwa Virian (T) baadaye Varerian na sasa Bunda Oil Industries.

Mwaka 2004 vijiji viliandika barua kwa mkuu wa wilaya vikidai maji yenye caustic soda yamesababisha mifugo yao kufa:  ng’ombe 536, mbuzi 212 na kondoo 171. Barua hiyo ya tarehe 3 Januari 2004 ilikuwa na Kumb. Na MIGMIG/197/04/26.

Pamoja na mamlaka zote za wilaya kupata majibu ya uchunguzi wa maji hayo kutoka maabara ya maji Mwanza, Laboratory No.337/2002 yaliyowasilishwa kwa mkuu wa wilaya hiyo tarehe 7/3/2002 ikionyesha kuwa maji hayo hayafai kwa matumizi ya viumbe hai, bado hawakusaidiwa na serikali yao.

Hivi sasa vijiji hivyo vinaomba Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira itembelee kufanya ukaguzi na kufanya tathmini juu ya madhara wanayopata kutokana na uwepo wa kiwanda hicho.

Hakuna kiongozi wa halmashauri aliyefika kukagua mashamba hayo zaidi ya kuishia kiwandani.

Kiwanda, kikitumia udhaifu huo, kililipa fedha baadhi ya wananchi  kupitia mwenyekiti wa mtaa, Robert Gikaro.

Ofisa Mazingira wa halmashauri hiyo Nashon Mirumbe alikiri bwawa la maji hayo kupasuka kutokana na kujaa, kwa madai hayajawahi kutolewa pamoja na kuagizwa hivyo na NEMC.

“Ni kweli maji yamevuja kwa wingi, nimeona bwawa limepasuka kwa sababu yamejaa, nimeagiza wazibe haraka kwa kuchimba mengine. Kuhusu madhara tunafuatilia ili sheria iweze kuchukua mkondo maana kila leo matatizohaya haya na watu wanaumia,” alisema.

Mdamo alipoulizwa kuhusu bwawa lile lile walilosema wameridhika na kuruhusu uzalishaji, alisema “Imetokea tena sikuwa na taarifa.”

Akaongeza;  “Hata hivyo hatuna usafiri wa kufika huko, watu wa halmashauri wanatakiwa kufuatilia. Mbona watu wangu walikuwepo huko?” alihoji.

Mkurugenzi wa kiwanda hicho Rajesh Savla alikiri kiwanda kuvujisha maji ya sumu na kuwa ilitokana na mvua nyingi kunyesha na maji yakajaa kwenye mabwawa.

“Imekwishaongea nao mwenyekiti yao imechukua Sh. 4.5 milioni kwa watu 22 kama fidia hii mambo iishe, halafu tunachimba pond ingine sisi. Hii mambo si nzuri kuandika maana mimi tayari sasa kwishamalizana nao,” alisema.

Alipotakiwa kueleza ameshirikisha wataalamu gani wa maji na amewafidia nini maana wafugaji wanaenda ziwani sasa alisema, “Sisi imeongea na mwenyekiti kwishaelewana mambo yote ya nini hayo?”alisema.

Mwenyekiti wa kitongoji hicho Gikaro alikiri kupokea kiasi hicho cha fedha kama fidia. Hata hivyo hakusema alizingatia nini na aliwashirikisha wenye mashamba.

“Tumeamua kufanya kirafiki tu sisi hatukutaka mambo mengi, lakini wengine wamekataa kuchukua fedha kwa kuwa ni kidogo,” alisema.

Haya yanatokea katika kipindi ambacho Watanzania wanasherekea miaka 50 tangu Tanzania Bara ipate uhuru. Lakini thamani ya maisha ya binadamu ni ndogo kuliko fedha za wawekezaji.

Mei mwaka 2009 maji yenye sumu yalivuja katika mgodi wa dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya African Barrick Gold ya Canada. Hadi leo serikali imekataa kutoa ripoti ya tathimini kiafya kwa wakazi walioathirika.

0
No votes yet