Bunge hai, mijadala moto na vijembe

LINAWEZA kuitwa "Bunge moto." Mijadala ilikuwa mikali. Mawaziri waling'ang'aniwa. Kila mbunge aliyepata fursa ya kuzungumza, bungeni au nje ya bunge, alikandia serikali.
Kilichosikika zaidi kutoka kwa wabunge, pamoja na hasira dhidi ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, ni serikali kutotekeleza ahadi alizotoa Rais Jakaya Kikwete wakati akitafuta urais na baadaye.
Hakika Mkutano wa 16 wa Bunge, uliochukua siku 40 na kumalizika mwishoni mwa wiki, ulikuwa wa sura tofauti kwa maana ya wabunge kuwa jasiri na serikali kuonyesha uvumilivu wa aina yake.
Baadhi ya wabunge walitoa laana kwa baadhi ya mawaziri na wa kwanza kuonja "joto la jiwe" alikuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo pale alipowasilisha bajeti ya serikali.
Kutokana na mjadala wa bajeti kuwa mkali lakini makini, Mkullo alilazimika kubadilisha baadhi ya vipengele katika bajeti ili kukidhi matakwa ya wabunge.
Kwa mfano, alifuta msimamo wake wa awali wa kutaka kuondoa misamaha ya kodi kwa taasisi za kidini.
Ni uelewa wa haraka wa kusoma nyakati wa serikali na waziri Mkullo, katika maeneo yaliyokuwa yakipingwa, ambao ulisaidia bajeti ya serikali kupita bila vizingiti zaidi.
Hata hivyo kulikuwa na minyukano hapa na pale. Makundi mawili makubwa ndani ya Bunge yalitafutana bila kificho. Haya ni lile linalotuhumiwa ufisadi na lile linalopinga ufisadi.
Makundi haya yalijithibitisha pale mbunge wa Viti Maalum, Injinia Stella Manyanya wakati alipokuwa akijadiili ripoti ya maoni ya kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.
Alisema, "Orodha ya wachangiaji ilipokuwa inatajwa, kulisikika minongono ya 'ah…ndiyo haohao.' Na kweli tutabaki sisi wachache wenye uchungu na nchi…"
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, hakubaki salama. Aliambiwa "analea watoto wa kufikia." Huyo alikuwa John Shibuda (Maswa) wakati wa kujadili taarifa ya maoni ya Kamati ya Nishati na Madini kuhusiana na mgodi wa mkaa wa Kiwira.
Alisema mawaziri wameshindwa kazi, lakini hawawezi kusema; hivyo wafukuzwe kazi. Aliongeza kuwa "hata mtoto si riziki hupeleka posa."
Katika hatua nyingine, Pinda alibanwa mbavu kuhusu suala la Muungano na bila kutarajiwa, alilieleza bunge kuwa ili kuondokana na chokochoko za sasa, afadhali "tuwe na serikali moja. Yote yatakwisha."
Ni kauli hii ambayo iliwasha moto ndani ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambapo wajumbe walimtuhumu kwa kile walichoita "kuhatarisha Muungano."
Naye Fred Mpendazoe alisema kawaida watu "huzunguka mbuyu," lakini yeye anathubutu kuukumbatia. Akitaka viongozi wa awamu ya tatu wanaotuhumiwa ufisadi, wajitokeze na kuomba radhi kwa umma.
Baada ya Mpendazoe kumalizia hoja yake, Spika Samwel Sitta alisema, hatua ambayo mbunge anapendekeza "ni sawa na kufunga zizi wakati ng'ombe wote tayari wameibwa."
Hakika, pamoja na udhaifu uliopo kwenye baadhi ya kanuni za Bunge na kile kinachoitwa, "wabunge kuweka mbele maslahi ya vyama kuliko taifa," lakini angalau mkutano huu umeonyesha umakini kwa kuweka mbele maslahi ya taifa.
Wabunge hawakuacha kutupiana vijembe. Mbunge wa Kasulu Magharibi, Kilontsi Mporogomyi alimtuhumu mbunge wa Singida Kusini, Mohammed Misanga kwa kumtuhumu utovu wa uadilifu, Mkurugenzi wa Baraza la Mitihani la Taifa, Dk. Joyce Ndalichako kutokana na kuvuja mara kwa mara kwa mitihani na kuwafukuza wafanyakazi kinyume cha taratibu.
Misanga alijibu mapigo kwa kusema Mporogomyi alilipotosha bunge kwa maslahi yake binafsi na kudai kuwa Mporogomyi na Dk. Ndalichako ni ndugu, wanatoka mkoa mmoja na kwamba Dk. Ndalinacho alikuwa mwanafunzi wa Mporogomyi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Je, nini kiini cha haya yote? Kuna majibu mengi. Kwanza, hali hii imetokana na baadhi ya mawaziri walioteuliwa kutokuwa na uwezo wa kutenda kazi zao. Mifano ni mingi.
Hata sakata juu ya taarifa ya serikali katika kushughulikia mkataba wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya Richmond limetokana na uelewa na uwezo mdogo walionao baadhi ya mawaziri.
Zimwi la Richmond lilirudishwa bungeni wiki mbili zilizopita na Adam Malima, naibu waziri wa wizara ya nishati na madini.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Malima alitangaza uamuzi wa serikali "uliobeba" viongozi wawili waandamizi serikalini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Edward Hoseah.
Ilitarajiwa kabla ya taarifa hiyo kuwasilishwa bungeni, serikali ingeiwasilisha kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.
Hata kama utaratibu unaruhusu kupeleka taarifa kama hiyo bungeni bila kushirikisha Kamati, kwa mazingira ya suala la Richmond, haikuwa busara kwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kulipeleka suala hilo bungeni kabla ya kwanza kulipitisha kwa Kamati.
Kwa kushirikisha Kamati makosa mengi ambayo yalikuwamo ndani ya taarifa, yangeweza kuonekana na hivyo ama taarifa ingeondolewa au ingefanyiwa marekebisho.
Kwa mfano, taarifa iliyowasilishwa haikuwasilishwa bungeni kwa kupitia ofisi ya waziri mkuu kama ilivyokuwa huko nyuma. Pili, taarifa haikuwa imesainiwa.
Si hivyo tu, taarifa haikuwa na jina lililokamilika. Iliitwa, "Taarifa ya Serikali kuhusu mkataba wa Richmond" badala ya "Taarifa ya serikali juu ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu mkataba baina ya Tanesco na Richmond Development Company LLC."
Kasoro hizi na nyingine ndizo ziliipa nguvu Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini. Kuna madai kwamba wajumbe wa Kamati walitumia upungufu huo kujenga hoja za kisheria kupinga taarifa ya serikali.
Iliilazimu Kamati kumuita waziri Ngeleja, kwanza ili kuthibitisha iwapo taarifa iliyopelekwa bungeni na naibu wake, ilikuwa yake. Kisha ikithibitika kuwa ni yake, basi akubali kuisaini. Ngeleja alithibitisha kuwa taarifa ni yake na hivyo akakubali kuisaini.
Hata kule kuondoa kifungu cha mswaada wa sheria wa marekebisho ya sheria mbalimbali, ikiwamo ya iliyotaka kuruhusu uchimbaji madini katika mbuga na hifadhi za taifa, kulitokana na udhabiti wa wabunge.
Hata suala la ubinafsishaji wa mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya, ambapo serikali ilishikwa koo na wabunge, kumetokana na wabunge wengi kusukumwa na maslahi ya taifa.
Ukiacha hilo, kuna hili la baadhi ya mawaziri kutohudhuria vikao vya bunge inavyostahili. Wengi waliacha majukumu yao kwa manaibu wao.
Kuna taarifa kwamba waziri mkuu Pinda alitoa maagizo kwa mawaziri kutoondoka bungeni, labda pale ambapo kuna sababu za msingi. Lakini wengi walionekana kutoitikia wito huo.
Mfano, Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurance Masha aliondoka bungeni na kwenda Dar es Salaam ambako alionekana kwenye mashindano ya kumtafuta mrembo wa Kinondoni. Taarifa zinasema ndiye alikuwa mgeni rasmi.
Wakati Masha akishindwa kuhudhuria vikao muhimu vya Bunge ikiwamo upitishaji wa miswaada ya sheria ya serikali, wabunge wote watatu wa wilaya ya Kinondoni, Idi Azan, Ritha Mlaki na Charles Keenja walibaki bungeni.
Matokeo yake, naibu waziri Khamis Kagasheki, alilazimika kubeba mzigo wa kujibu tuhuma za vitambulisho lililoanzishwa na Masha.
Kagasheki alijikuta akikabiliana ana kwa ana na wabunge waliokuwa wamechachamalia serikali kwa ucheweshaji wa mradi huo. Kimsingi Kagasheki alionekana kujitoa kafara kwa jambo asilolijua.
Aidha, ufinyu wa muda ulichangia kuzorotesha kazi za bunge. Tofauti na mkutano wa bajeti wa mwaka jana (6 Juni 2008 hadi 25 Agosti 2008); mkutano uliomalizika mwishoni mwa wiki, ulichukua siku chache.
Hii ina maana kwamba wabunge wengi waliotaka kuchangia kwa hotuba, hawakupata nafasi. Hata wizara nyeti kama ya elimu ilipangwa kujadiliwa kwa siku moja na kupitishwa siku hiyohiyo. Katika bajeti ya mwaka jana, elimu ilijadiliwa kwa siku tatu.
Iliwalazimu wabunge kumchachamalia Naibu Spika, Makinda ili aruhusu kuongezwa muda wa ziada. Mbunge wa Viti Maalum, Diana Chilolo, ndiye aliyewasilisha maombi ya wabunge. Hatimaye muda uliongezwa hadi siku mbili kutoka moja ya awali.
Hata hivyo, kutokana na wabunge wengi kutaka kuchangia wizara hii, hata muda huo ulioongezwa haukutosha. Kati ya wabunge 78 waliojiandikisha, ni wabunge 40 tu waliopata nafasi ya kuchangia.
Hali kama hiyo ilitokea pia katika sakatala la Richmond na mgodi wa Kiwira. Wengi wa wabunge walioomba kuchangia hawakupata nafasi. Haya yamefanyika kutokana na serikali kushindwa kupata fedha za kulipia gharama za vikao.
Bunge la mwaka huu, lililazimika kufanya shughuli zake hadi Jumamosi. Hili lilipunguza umakini na kurejesha bunge katika nafasi ya "kupiga muhuli" tu kwa mtindo wa "liache liende."
Kama bunge haliwezi kuwa na fedha za kutosha za kujiendesha, kuna umuhimu gani wa kuongeza idadi ya wabunge?
Kama dhamira ni kuwa na Bunge linalosimamia serikali, basi hakuna umuhimu wa kuongeza idadi ya wabunge. Ni muhimu kubaki na idadi iliyopo sasa, au hata kupunguza; lengo likiwa ni kuboresha uwezo wao ili waweze kutimiza majukumu yao.