Bunge lililojaa wateule, haliwezi kuwa na meno


Joseph Mihangwa's picture

Na Joseph Mihangwa - Imechapwa 19 August 2008

Printer-friendly versionSend to friend

KATIKA hotuba yake ya kwanza mbele ya Bunge, 30 Desemba 2005, Rais Jakaya Kikwete alisema uongozi wake utazingatia, kuheshimu na kutekeleza dhana ya utawala bora na utawala wa sheria.

Alisema atahakikisha “mihimili mikuu mitatu” inayojitegemea katika utawala inafanya kazi bila kuingiliwa au kuingiliana.

“Lengo hapa ni kuhakikisha demokrasia inashamiri nchini,” alisema rais. Mihimiri hiyo ni Bunge, lenye mamlaka ya kutunga sheria, Serikali yenye jukumu la kutekeleza sheria na Mahakama yenye mamlaka ya utoaji haki.

Mihimili yote mitatu inatakiwa kuwa na uzito sawa katika kuendesha shughuli zake. Bunge kama chombo cha kutunga sheria, ndiyo chimbuko la uongozi katika nchi.

Ni jukumu la Bunge kusimamia serikali kwa niaba ya wananchi kwa misingi ya uhuru, haki, udugu na amani. Ni jukumu lake pia kuihoji na hata kuiwajibisha kwa niaba ya walioiweka madarakani.

Katiba yetu iko wazi kuhusu aina ya Bunge linaloweza kutekeleza jukumu hili. Sehemu ya “utangulizi” ya Katiba inasema, “…misingi hii (ya uhuru, haki, udugu na amani) yaweza kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia ambayo Serikali yake husimamiwa na Bunge lenye wajumbe waliochaguliwa na linalowakilisha wananchi…”.

Kwa maana hii, ili mbunge astahili kusimamia Serikali lazima awe mbunge wa kuchaguliwa kuwakilisha wananchi na si mbunge wa aina nyingine, awe wa kuteuliwa au vinginevyo.

Mhimili wa utawala ndiyo serikali inayoongozwa na rais, Baraza la Mawaziri na Watendaji wengine. Wote hawa kazi zao ni kusimamiwa na Bunge lenye wajumbe waliochaguliwa.

Hivyo mbunge aliyechaguliwa anapoteuliwa kuwa waziri huingia katika mhimili wa utawala (unaosimamiwa na Bunge) na kuwa mwakilishi na msemaji wa serikali, hivyo hukoma kuwa msemaji wa wananchi na mtetezi wao.

Kwa mantiki ya kawaida, mbunge wa kuchaguliwa anapoteuliwa kuwa waziri hapaswi kuitwa mbunge; jimbo lake linastahili kupata mbunge mwingine wa kuwasemea watu, maana huyu tayari amekuwa mtawala.

Wabunge wa kuteuliwa hawawakilishi wananchi kwa sababu anayewateua (rais) si sehemu ya mhimili wa bunge. Mtindo wa kuchomeka wabunge wa kuteuliwa unalipunguzia Bunge nguvu na sauti ya kwa umma.
 
Mtindo huu ulipata upinzani mkubwa bungeni ulipoanzishwa miaka ya 1960. Mbunge wa Iringa Kusini, mheshimiwa Chogga, aliwasilisha hoja kwa kusema, “mheshimiwa Spika, siafiki kabisa mtindo huu wa kuteua wabunge; siuamini na unanikera.”

Alisema, “Inapotokea mtu mmoja (rais) kumteua mtu mwingine kuingia katika chombo cha uwakilishi kisichomhusu, anayeteuliwa lazima atafuata, atawakilisha na kuzingatia ya yule aliyemteua. Nani asiyejua usemi ya kwamba, amlipaye mpiga zumari ndiye achaguaye wimbo?” (Hansard, 12 Julai 1968).

Choga na wabunge wenzake wanne walifukuzwa ubunge kwa kuhoji mfumo huo potofu ambapo ni wazi kwamba ilikuwa haki yao ya kikatiba kufanya hivyo.

Kufukuzwa kwa wabunge hawa ulikuwa udikteta wa mhimili wa utawala kwa lengo la kulidhibiti Bunge na demokrasia ya uwakilishi kwa ujumla.

Kazi ya Mahakama kwa upande wake ni kutafsiri sheria, kuziba au kusahihisha mapungufu ya sheria. Ni kazi ya mahakama kuzuia matumizi mabaya ya sheria kwa watawala na kwa Mahakama hiyo kuitumia sheria bila woga au kuingiliwa na mhimili mwingine.

Mfumo huu wa mhimili mmoja kutoruhusiwa kuingiliwa utendaji kazi wa mhimili mwingine huitwa “mgawanyo wa madaraka.”

Mwanafalsafa Montesquieu anabainisha kwamba haki na uhuru wa mtu utakuwa hatarini iwapo mtu mmoja ataachiwa kutekeleza mamlaka yote, yaani kutunga sheria, kuzitekeleza, kuzitafsiri na kuhukumu.

Mwandishi bingwa katika sheria za Katiba A. Dicey, anasema Bunge ni chombo cha kutunga sheria, ni mhimili mkuu katika serikali.

Dhana ya “mgawanyo wa madaraka” lazima iheshimiwe maana ndiyo hati miliki pekee kwa utawala bora na utawala wa sheria.  
Lakini pamoja na serikali kuweza kuipenyeza dhana hii katika Katiba (Ibara ya 4), sambamba na kuridhia Mkataba wa Kimataifa juu ya Haki za Binadamu (Bill of Human Rights), kuna vioja vingi vya demokrasia vinavyojitokeza ndani ya Bunge.

Kwa mfano, baadhi ya wabunge hukemewa na mawaziri, au serikali inawasilisha miswada ya sheria kwa hati ya dharura, ambapo huwanyima wabunge muda mzuri wa kuipitia.

Mambo haya yanaonyesha jinsi utawala unavyoimba demokrasia na utawala bora ki-kasuku kwa lengo la kuvutia misaada kutoka kwa wafadhili.

Hadi hapo tayari imedhihirika kwamba mbunge anapoteuliwa kuwa waziri anakuwa si mwakilishi wala hawajibiki tena bungeni kwa wananchi waliomchagua.

Hiyo ni sawa na kusema kwamba jimbo lake linakuwa halina mwakilishi. Hakika, uteuzi wa mawaziri, pamoja na ule wa “wabunge wa kuteuliwa” ni kuteka nyara demokrasia ya Bunge kwa kujaza wabunge wasiowakilisha wala kuwajibika kwa wananchi.

Udhaifu huu upo pia kwa nafasi ya Spika wa Bunge. Tunaambiwa, Spika lazima awe mbunge au mtu yeyote mwenye sifa ya kuwa mbunge na atokane na chama cha siasa.

Kwa nini atokane na chama cha siasa wakati Bunge si chombo cha siasa bali ni cha kutetea katiba ya nchi iliyo juu ya Katiba za vyama?

Demokrasia haina chama cha siasa. Sharti la Spika kwamba atokane na chama cha siasa ndicho chanzo cha malumbano ya kiasiasa na uchama usiotakiwa bungeni, unaoua umakini wa wabunge katika kuwasemea wananchi kwa sababu ya kulinda maslahi ya vyama.

Mtindo wa kuwateua wabunge kuwa wenyekiti wa mashirika au asasi za umma nao ni ugonjwa mwingine sugu unaodhalilisha hadhi ya bunge, licha ya kwamba mtindo huu ni kinyume cha katiba ya nchi inayotaka bunge kuwa msimamizi wa serikali katika utekelezaji wa sera zikiwamo taasisi za umma.

Je, itawezekanaje kwa mbunge ambaye ni mkuu wa asasi ya umma kuiwajibisha asasi anayoiongoza? Yote hayo yanaonyesha jinsi tabaka la watawala lilivyopania tangu enzi za uhuru kufifisha harakati za wananchi za ujenzi wa demokrasia ya kweli.

Chini ya dhana ya demokrasia ya kiliberali ambayo tunaitekeleza, Bunge na Mahakama ni mihimili inayofanya kazi kama “checks and balances”- yaani “kidhibiti mwendo” kwa Serikali ili mwenendo wake usiwaumize wananchi.

Ni kwa misingi hii, ili Bunge lionekane kuwa sauti ya umma, ni vema katiba yetu ikarekebishwa ili kulifanya kuwa mshauri wa rais ili aweze kutenda kwa maslahi ya wananchi.

Vivyo hivyo, Mikataba yote ikiwamo ile ya Kimataifa na uwekezaji, lazima ipate kibali cha Bunge kabla ya utekelezaji.

0
No votes yet