Butiku akana madai ya Sabodo

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku amesema hataki malumbano na mfanyabiashara Mustafa Jaffer Sabodo wa Dar es Salaam.
Amesema madai ya mfanyabiashara huyo kuwa hajui matumizi ya kile alichoita “fedha nilizochangia MNF,” kinahitaji kujibiwa kwa usahihi ili kuondoa ukungu ambao Sabodo amenyunyizia.
“Sijui madai haya yanatoka wapi. Sijui chanzo chake. Bali, ni kweli kwamba tulishirikiana na Sabodo kuendesha mchezo wa Bahati Nasibu,” anasema Butiku.
Huku akionyesha kuwa na huzuni, Butiku anasema, “Ni mimi niliyekwenda kwake kuzungumza naye jinsi ya kupata fedha za kuendesha baadhi ya kazi za taasisi yetu. Tulipofika na kumueleza hilo, yeye akapendekeza tuanzishe bahati nasibu na ifunguliwe na rais. Tukafanya hivyo.”
Anasema ni Sabodo aliyependekeza iundwe kamati kuendesha bahati nasibu na kwamba kamati iliundwa na majina ya wajumbe yakatolewa na Sabodo mwenyewe.
Desemba mwaka jana, Sabodo alitoa matangazo katika baadhi ya magazeti kueleza kile alichoita, “matumizi katika taasisi ya Mwalimu Nyerere” na kutaka taasisi hiyo itoe mchanganuo wa matumizi ya Sh.1 bilioni alizoichangia.
Katika tangazo lake aliloandika kutetea Kikwete na kutuhumu taasisi, Sabodo alisema, “Nilichangia Sh. 1 bilioni katika mchezo wa bahati nasibu iliyokuwa inaendeshwa na taasisi ya Mwalimu Nyerere. Mbali na mimi, watu wengi pia wamechangia katika mfuko huo. Fedha zote walizochangiwa zipo wapi? Waseme walichofanya, waseme walichopoteza," alieleza katika taarifa yake.
Maelezo ya Sabado yaliibuka siku chache baada ya taasisi ya Mwalimu Nyerere kuendesha kongamano ambapo washiriki waliibuka na hoja ya kutaka Rais Jakaya Kikwete atende kazi zake kwa mujibu wa katiba kwa kuchukulia hatua za kisheria watuhumiwa wa ufisadi nchini.
Akijibu madai hayo, Butiku anasema, “Kwanza, ni vema ukafahamu kuwa hakuna fedha ambayo Sabodo ametupa. Tulichokubaliana ni kuendesha mchezo wa bahati na nasibu.”
Lakini pili, Butiku anasema, “Hata katika kuendesha mchezo, Sabodo alitoa Sh. 774,670,905 na siyo Sh. 1.bilioni kama anavyoeleza. Sisi katika fedha hizo hatukuhusika na lolote.
“Bahati nasibu ilikuwa na bodi yake. Mwenyekiti alikuwa Cleopa Msuya. Alikuwapo Jaji Joseph Warioba, Philemon Luhanjo, Bob Makani na Nimrod Mkono. Mratibu wa mradi alikuwa Christopher Mramba. Mimi nilikuwa mjumbe tu,” anaeleza.
Anasema baada ya uteuzi huo wa bodi, waliteuliwa watiasaini kwenye hundi. Anaeleza, “Signatory (mtia saini) A walikuwa Msuya na Sabodo. Signatory (mtia saini) B alikuwa Luhanjo na Warioba. Sisi kama taasisi hatukuhusika na lolote hapo. Sekretarieti ilikuwa haina uwezo wa kutumia hata senti tano bila kuomba kwenye kamati.”
Akiongea kwa kuonyesha uchungu, Butiku anasema, “Hawa wote waliteuliwa na Sabodo mwenyewe. Yeye alikuwa kila kitu. Alikuwa na hata veto (uwezo) ya kuamua nini kifanyike na nini kisifanyike. Hakuna malipo ambayo yalifanyika bila kupatikana idhini yake; fedha nyingi zilichukuliwa na Sabodo mwenyewe.”
Mchanganuo wa fedha unaonyesha kwamba Sh. 30 milioni zilitengwa kwa ajili ya kuchapishia tiketi, Sh. 600 milioni kwa ajili ya zawadi, Sh. 36 milioni kwa vipepurushi, Sh. 29 milioni kwa mabango ya matangazo, Sh. 6.3 milioni kwa simu aina ya Nokia na Sh. 23.1 milioni ndizo zilizotengwa kwa ajili ya kutunisha mfuko wa taasisi. Jumla ya fedha zote ni Sh. 774, 670, 905 tu.
Kuhusu taasisi yake ilivyoendesha mradi huo, Butiku anasema baada ya kukubaliana na wazo la Sabodo, walikaa na kujadili nani aendeshe mradi huo.
Anasema, “Makampuni mawili yakajitokeza. Naye ndiye aliyependekeza kampuni ya kuchukua na moja akakataa hata kuilipa. Kampuni ya pili, ilikuwa ya kihindi. Nayo akaifukuza.”
Anasema, “Kisha ndiyo wakajitokeza hawa Posta (Shirika la Posta), wakaleta mpango wa kuendesha. Mkataba ukafungwa. Utaratibu wa zawadi ukawekwa. Kulikuwa na zawadi nyingi tu. Kulikuwa na jembe la kukukotwa na ng’ombe, kulikuwa na friji, simu, baiskeli na vingine vingi.”
Anasema mara baada ya mkataba kufungwa, ukaibuka mgogoro wa chini kwa chini juu ya zawadi zitakazotolewa. Wakati taasisi ilipendekeza zawadi zinunuliwe mikoani ambako washindi watapatikana, Sabodo alitaka zinunuliwe Dar es Salaam na kupelekwa kule ambako washindi watapatikana.
“Sisi tuliona kwamba gharama za kusafirisha zawadi, zitakuwa kubwa. Tukasema zawadi zitanunuliwa pale ambapo mshindi atapatikana. Hii ingesaidia kupunguza gharama za kusafirisha zawadi na kuzihifadhi,” analeza Butiku.
Anasema, “Lakini mwenzetu akakataa. Akampa kazi hiyo mwanawe na zawadi zote zikanunuliwa Dar es Salaam. Utaratibu wa zawadi ukawa mgumu na matokeo yake watu wengi hawakuchukua zawadi zao.”
Alipoulizwa kama kuna washindi wa bahati nasibu ambao hawakuchukua zawadi zao na ziko wapi zawadi hizo hivi sasa, Butiku haraka alijibu, “Nyingi amezichukua Sabodo mwenyewe. Amekataa kuzirudisha. Anasema zake.”
Anasema kwamba gari lililonunuliwa kwa ajili ya kulitoa zawadi kwa msindi, nalo limezua mtafaruku baada ya mshindi kulalamika kwamba amepewa gari lililotumika.
Anasema taasisi yake wala haijui kiasi gani kilipatikana. Haijui zilitumikaje; wala hakuna hata shilingi iliyokabidhiwa kwao. Hata Rais Jakaya Kikwete ambaye amezindua bahati nasibu hiyo hajapelekewa ripoti.
Anasema, “bali tumeambiwa kwamba kuna Sh. 200 milioni zilizopatikana. Hizi zimehifadhiwa BOA Benki; lengo ni kuanzisha mfuko wa akiba.”
Akizungumzia mustakabali wa kisiasa, Butiku anasema bado anaamini kwamba CCM kinahitaji mabadiliko makubwa ili kiweze kurudisha heshima yake ya awali.
Anasema hadi pale CCM itakapoamua kufuata katiba yake ndipo atakaponyamaza; lakini kwa sasa hakuna mwenye uwezo wa kumyamazisha. “Ndani ya CCM, viongozi wameshindwa kusimamia katiba. Fedha ndizo zinazochagua viongozi,” anaeleza kwa masikitiko.
Anasema, “Ushahidi wa hili ni viongozi wenyewe wa CCM baada ya kila uchaguzi hulalamika. Viongozi wetu wanalijua hili.”
Alipong’ang’anizwa kueleza CCM imefikaje hapo ilipo, Butiku alicheka na kusema, “Nami nikuulize wewe, tumefikaje hapa? Nadhani kila mtu anajua tumefikaje hapa. Tumefikishwa na baadhi ya viongozi na wanachama wenzetu wa CCM; wale ambao waliamua kutumia fedha kupata madaraka.”
Butiku aliwahi kunukuliwa akisema kwamba mwaka 1995 wakati wa kuchuja wagombea wa urais, ndipo CCM ilipoanza kujenga msingi mbaya kwa kuruhusu mwanachama mmoja kutumia fedha kuingia madarakani.
Butiku anaamini kwamba kwa sasa ni Rais Kikwete pekee mwenye uwezo wa kuirudisha CCM katika mstari wake kutokana na madaraka aliyonayo.
“CCM haifuati utaratibu, wanachama wake wanazomeana, wanatukanana. Katika mazingira haya, mtu anaweza kusema kwamba pale hakuna chama. Watu wenye kujiheshimu hawazomeani, mkizomeana mnakuwa kundi la wahuni. Viongozi wanajadili na kutafuta suluhu ya matatizo,” anasema.
Anaongeza, “CCM hapo ndipo ilipofika. Ni Rais Kikwete pekee kwa sasa mwenye uwezo wa kuinasua.”