CC imedandia mgongoni mwa wabunge


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 02 May 2012

Printer-friendly version

KWA sababu za kishabiki tu watu wanaweza kusifu maamuzi ya Rais Jakaya Kikwete kwenda kuisikiliza Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) juu ya utendaji wa mawaziri wake, na kisha kutolewa taarifa kwamba CC imebariki kung’oka kwa mawaziri wanane wanaotuhumiwa ama kwa wizi au uzembe katika kutekeleza majukumu waliyopewa.

Kusifu huku kunatokana na vitu viwili vikubwa, mosi, upeo mdogo wa kufikiri wa watu, wakiamini kuwa CC ya CCM ina nafasi katika madaraka ya kikatiba ya Rais. Pili, watu hawa wamefunikwa mno kimaono kiasi cha kufikia mahali pa kushindwa kujua madaraka ya rais ya kutimiza wajibu wake yanatoka wapi.

Kwa faida ya wasomaji wa safu hii nitafafanua kidogo juu ya madaraka ya Rais na chimbuko lake.

Madaraka na wajibu wa Rais wa Tanzania yanafafanuliwa kuanzia ibara ya 33 hadi ya 46B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Mambo mengi mno yamefafanuliwa. Baadhi ni kuwapo Rais, kuwako serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Utekelezaji wa madaraka ya serikali yalivyoelekezwa chini ya  rais; uchaguzi wa rais; sifa za kuwa Rais; haki ya kuchaguliwa tena kuwa Rais; utaratibu wa uchaguzi wa Rais; wakati na muda wa kushika madaraka ya Rais; madaraka ya kutangaza vita; uwezo wa kutoa misamaha kwa wafungwa; kinga dhidi ya mashtaka; mamlaka ya Bunge ya kumshitaki Rais na wajibu wa viongozi wakuu wa vyombo vya mamlaka ya utendaji katika kudumisha Muungano.

Katika mlolongo huu wa madaraka, haki na wajibu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano, hakuna popote si chama chake wala kamati yoyote ya chama hicho, vimetajwa kuwa vinaweza kumshauri na yeye akakiri hadharani kwamba ameshauriwa na hivyo kueleza kuwa anawajibika kufanya mabadiliko ya mawaziri wanaotuhumiwa.

Hawajibiki kutenda hivyo kwa sababu, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 55  imefafanua kwa uwazi jinsi ya kuwapata mawaziri, kwamba atashauriana na Waziri Mkuu kuwateua.

Ibara ya 57 (1) , (2) (a) hadi (g) inafafanua kwamba watashika madaraka ya uwaziri isipokuwa tu lolote kati haya litokee; kufariki dunia, kupoteza ubunge, ikiwa Rais atatengua uteuzi, iwapo atachaguliwa kuwa Spika wa Bunge, iwapo Waziri Mkuu atajiuzulu au kiti chake kibaki wazi kwa sababu yoyote ile, ukiwadia muda wa Rais mteule kushika madaraka ya Rais basi mara tu kabla ya Rais Mteule hajashika madaraka hayo, iwapo Baraza la Maadili litatoa uamuzi unaothibitisha kwamba amevunja sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Katika mtiririko huu, kuitumbukiza CC ya CCM kama chombo cha kuulizwa au kushauri kama mawaziri husika waondoke au la haikuwa sawa kuwa jambo la kufanywa na kuwekwa hadharani kwamba ndiyo msingi wa maamuzi ya kuwaondoa mawaziri wanane.

Wabunge wana madaraka haya kwa mujibu wa ibara 63 (2) kwamba kwa niaba ya wananchi litaisimamia na kuishauri serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vyombo vyake katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba.

Lakini ukakasi unaingia pale wajibu huo sasa unapochukuliwa kwa njia za panya, kiasi cha kuonekana kuwa ni jambo la chama zaidi, kama walivyoanza wabunge wa CCM chini ya kamati ya wabunge wa chama hicho, kisha kufikishwa kwa Kamati Kuu.

Njia hii inajenga kitu kilichokuwa kinaitwa zamani “party supremacy” (chama kushika hatamu). Huku ni kukengeuka kukubwa, lakini pia ni njia za kutaka kupata sifa na heshima ambazo hazistahili kwa vyombo hivi nje ya mfumo rasmi wa kibunge.

Tukumbushane kwanza; kwamba katika mkutano wa saba wa Bunge la 10 ambao uliahirishwa Aprili 23, mwaka huu, hakuna siri wabunge kwa ujumla wao, waliishambulia serikali na kwenda mbali zaidi kwa kutaja majina ya mawaziri kwa majina juu ya udhaifu wao.

Hawa walitajwa kutokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2009/10 na taarifa za Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Walionekana wazi kupwaya. Walitajwa majina, walielezwa walivyozembea katika nafasi zao wengine walielezwa wazi walikuwa wamekalia ofisi za umma wakichumia matumbo yao!

Katika mazingira kama haya, hakuna ubishi wala chembe ya shaka kwamba eti Rais hakupata kwa undani hisia za wabunge ambao walikuwa wanatekeleza wajibu wa kikatiba; kwamba eti Rais hakupata maamuzi ya Bunge, ambayo ni maamuzi ya kikatiba juu ya ripoti hizo.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati akiahirisha Bunge Aprili 23, 2012 jioni alionyesha wazi kuwa serikali imesikia maamuzi ya Bunge na kuahidi kuwa yatafanyiwa kazi. Haya ni maamuzi ya kutaka kuwajibika kwa mawaziri waliozembea.

Nimetumia muda mwingi kujenga hoja juu ya kutaka kuweka mambo katika mstari. Nia ni kutaka kujulisha umma ujue kuwa CC katika sakata hili imechomekwa ili kupata sifa na heshima ambayo kimsingi si yake katika kuisimamia serikali. Ni muhimu sasa tuanze kujenga uwazi katika kuendesha mambo yetu.

Nimesema hapo juu kwamba kikatiba hakuna mahali Rais anapowajibika kutafuta ushauri wa CC kiasi cha kuwekwa wazi kwamba ndiyo inamshauri hivyo.

Angeliweza kukutana nayo kuzungumza yanayowakabili mawaziri wake, na kisha iwe ni hivyo, mkutano wa ndani, lakini kutoa makubaliano hayo hadharani ni juhudi nyingine za kutaka kufufua kukubalika kwa CCM katika kipindi ambacho chama hiki kimefikia kiwango cha chini kabisa cha uwajibikaji na uwezo wa kufikiri katika kusaidia taifa hili litoke katika mkwamo mkali unaoliandama kwa sasa.

Sitaki kufurahia mbinu hizi hata kama mwisho wa yote baadhi ya mawaziri wataondolewa kwenye nafasi zao kutokana na uwajibikaji dhaifu. Ningependa sifa hizi zibaki kuwa za wabunge,  ni heshima kwa ofisi ya CAG ambayo mwaka baada ya mwaka imekuwa ikitoa ripoti za ulaji, ufujaji na kutokujali kwa watendaji wa umma kwa kiwango cha kutisha katika matumizi ya fedha za walipakodi.

Isitoshe ingependeza kama Rais Kikwete angechukua mamauzi hata kabla ya wabunge kuichanachana serikali yake bungeni.

Rais Kikwete ni wa kwanza kupewa ripoti ya CAG kabla ya kufikishwa bungeni, anafahamu madudu yote yanayotokea, mwenye uwezo na mawaziri ambao ni wasaidizi wake wakuu ni yeye, hata hao wakurugenzi wa serikali katika maeneo mengine ni uteuzi wake pia.

Kwa maana hii madudu haya yanayopigiwa kelele, ulaji na ufujaji, aliyajua mapema, lakini alichukua hatua gani? Hapa ndipo Watanzania wanatakiwa kudai uwajibikaji pia. Rais awe rais, anonyeshe madaraka, asisubiri kutafuniwa; ana meno yaliyojaa atafune mwenyewe na kumeza. Amepewa madaraka hayo na ayatumie sasa.

0
No votes yet