CCM acheni mzaha


editor's picture

Na editor - Imechapwa 15 April 2008

Printer-friendly versionSend to friend
Maoni ya Mhariri

MUAFAKA uliotarajiwa kuwa mwanzo wa hatua muhimu za kuleta ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar, umekwama.

Muafaka huu, uliotokana na mazungumzo yaliyohusisha viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), umekwamishwa na CCM tena kwa makusudi.

Ushahidi upo. Badala ya CCM kuidhinisha makubaliano yaliyomo kwenye Muafaka, kama walivyofanya CUF, wamezua hoja mpya ambayo haikutarajiwa: Kura ya maoni kabla ya kusonga mbele.

CCM walikusudia kufanya kukwamisha Muafaka. Vitimbi vilianza mapema. Ni CCM waliokataa kuwasilisha hoja za kujadili na kulazimisha wapewe zile za CUF ili wakazijadili kwanza.

Ni CCM walioomba, mara mbili, wasubiriwe kuendelea na vikao vya majadiliano kwa kisingizio cha kukabiliwa na mikutano muhimu ya chama.

Hii ilihusu kutawazwa kwa Kikwete kuwa Mwenyekiti wa CCM katikati ya mwaka 2006, na uchaguzi wa viongozi wa ngazi ya juu uliofanyika Novemba mwaka jana.

Hii ilikuwa wakati vyama hivi vinajenga hali ya kuaminiana kwanza, kabla ya kuamua ajenda zenyewe za mazungumzo. CUF walikubali visingizio vyote hivyo.

Sasa majadiliano yameisha na makubaliano yanahitaji saini, mdipo CCM wanaleta hoja mpya. Hii maana yake nini kama si kwamba wameazimia kukwamisha Muafaka?

Tunajiuliza, hivi CUF hawakuwa na uwezo wa kutaka marekebisho yoyote kwenye makubaliano waliyofikia na CCM?

Tunaambiwa hata wajumbe wa Baraza Kuu la Taifa la Uongozi la CUF, walitoa kasoro, lakini waliambiwa "hakuna tena nafasi ya marekebisho."

Leo, Kikwete anasema Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, ilikuwa na haki na ndio utaratibu wake kujadili mambo na kuyafanyia marekebisho pale inapobidi.

Uko wapi uadilifuwa CCM? Si ulaghai huu kwa Watanzania na walimwengu waliokuwa wanasubiri kwa hamu muafaka usainiwe? Sasa umekwama.

Tunaona Watanzania hawawezi kusubiri, bali mkwamo ndio uondolewe, kwani waliahidiwa ufumbuzi utakaokuwa na manufaa kwao na kwa taifa lao.

Je, kura ya maoni wanayoitaka CCM, na ambayo tayari CUF wameikataa, ndio ufumbuzi wa mpasuko ambao kiongozi wao aliahidi?

Lazima CCM wajirudi na waangalie maslahi ya taifa kuliko ya chama chao pekee ambacho ndicho chimbuko la mgogoro. Tatizo lao ni kutothamini maoni yaw engine na kutokubali misingi ya demokrasia.

0
No votes yet