CCM achieni Zanzibar ijizongoe

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinajenga siasa mbaya. Kwa kinavyoyachukulia baadhi ya mambo muhimu yenye maslahi na taifa, hapana shaka kinaelekea katika kukwamisha maridhiano Zanzibar.
Ni viongozi wakuu wa kisiasa Zanzibar, Rais Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, waliojenga dhamira ya maridhiano walipokutana faragha ikianzia na mkutano wa kwanza wa 5 Novemba mwaka jana ikulu.
Kutokana na hapo, Baraza la Wawakilishi (BLW) – chombo cha kutunga sheria upande wa dola ya Zanzibar kama ilivyo bunge kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – lilipitisha azimio mahsusi lililoweka msingi wa utekelezaji wa maridhiano hayo.
Ingawa azimio hilo lililowasilishwa barazani na kiongozi wa Upinzani, Abubakar Khamis Bakary – mwakilishi wa Mgogoni, Mkoa wa Kaskazini Pemba – lilitokana na CUF, sasa ni azimio la Baraza la Wawakilishi lisilozingatia itikadi ya kisiasa.
Ni azimio la Wazanzibari lililopitishwa na chombo kinachowawakilisha kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Wanasubiri utekelezaji wake ufanywe na serikali kwa vile mapendekezo yalivyo.
Baada ya hatua hiyo nzuri inayoelekea katika kuleta siasa safi, mtu angetarajia, kila mmoja aweke nguvu zake kuwezesha maridhiano hayo kuleta matunda ya kweli.
Watanzania wengi wamekuwa wakihimiza nafasi iliyojitokeza isipotezwe kwani lengo liwe ni kujenga mshikamano wa wananchi wa Zanzibar waliochoka mgawanyiko ulioletwa na siasa za chuki na uhasama.
Vyama vingi vilivyotoa maoni kuhusu maendeleo hayo, vimetaka maridhiano yaendelezwe kwa kupeleka mbele ajenda ya kuwaunganisha Wazanzibari ili wamalize mgogoro uliozorotesha maendeleo yao.
Kumbe CCM wana kinyongo. Utamu wa madaraka unawashughulisha. Viongozi wake wakuu wanaamini bado wana haki ya kutolea maoni azimio la baraza; kwa maana ya kurekebisha maamuzi yake.
Na kwa jeuri, wanatamba eti utekelezaji wake uzingatie maamuzi ya vikao vyao vya juu vilivyofanyika Machi 2008 katika kijiji cha Butiama, Musoma mkoani Mara.
CCM ilipendekeza iitishwe kura ya maoni ili wananchi wa Zanzibar washiriki katika kuamua mabadiliko yaliyojengwa katika Muafaka III uliofikiwa na vyama hivyo.
Hata kama kingekuwa ni kitu kizuri, kura ya maoni ilikuwa jambo jipya. Hata mara moja wajumbe wake katika kamati ya mazungumzo iliyojumuisha pia wajumbe wa CUF, hawakutoa rai hiyo wakati wa vikao.
Kwa namna walivyojenga hoja hiyo kwenye vikao vile, CCM walilenga kuihujumu CUF na Zanzibar. Wenyewe walisema ilikuwa ni mbinu ya kuipiku CUF kisiasa.
CUF ambao walipata nakala ya ripoti ya kamati ya Makamba, walikataa pendekezo hilo na hapo ikawa mwanzo na mwisho wa uliolengwa kuwa Muafaka wa tatu.
Rasimu ya muafaka iliyotokana na majadiliano yaliyoanzishwa katika mpango wa kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kile ambacho Rais Jakaya Kikwete alikiita “Mpasuko wa Zanzibar” yalikoma.
Baada ya kimya kikubwa, ilitokea bahati. Watu wachache mno waliokutana katika msiba wa Shaaban Khamis Mloo, mmoja wa waasisi wakuu wa CUF aliyetoka mifupani mwa Afro-Shirazi Party (ASP), waliulizana, “Hivi tutaendelea kupambana mpaka lini na nchi inazidi kumalizika.”
Swali likawatia simanzi; likawajenga ujasiri na kukubaliana kuchangia ufumbuzi.
Baada ya mambo kadhaa, hatimaye wakawezesha mkutano wa faragha kati ya Rais Karume na Maalim Seif. Alhamdulillah Mwenyezi Mungu ametia baraka dhamira yao njema.
Lakini CCM ni kama ina chuki vile na yanayotokea. Kama si hivyo, basi itakuwa inataka kujitambulisha kama bila ya wao hakuna maendeleo yatakayofikiwa.
Msimamo huo ndio unaokipa chama hiki jeuri kila wanapojadili mambo yanayoihusu Zanzibar. Ndipo hapo CCM wanapata jeuri ya kubadilisha azimio la baraza la wawakilishi.
Ni kweli CCM ni mhimili wa yanayotokea Zanzibar. Ila wakubali pia kwamba ndio chanzo cha mgogoro unaoimaliza Zanzibar. CCM imeshindwa kukubali misingi ya kweli ya siasa za ushindani.
Wazanzibari wanaporidhiana na kutafuta njia ya kufuta siasa za kijambazi, wanatumia haki yao ya kuamua hatima yao.
Baraza la Wawakilishi limeelekeza kura ya maoni ipigwe kabla ya uchaguzi. Linataka kamati ya watu sita – watatu kutoka CCM na watatu wa CUF – ifuatilie haraka utekelezaji wa azimio.
CCM inapokuja na maamuzi kwamba kura ya maoni ije baada ya uchaguzi mkuu inakusudia nini kama si kutaka kukwamisha maridhiano?
Ni kiburi kisicho mbele wala nyuma. CCM imezorotesha maendeleo ya Zanzibar kwa miaka mingi kwa sababu ya siasa-kiritimba. Kinataka kibaki madarakani kwa vyovyote.
Ieleweke kwamba CCM, kuanzia sekretarieti, Kamati Kuu (CC) na NEC, hawana nguvu yoyote kimaamuzi kushinda Baraza la Wawakilishi.
Baraza hili ni chombo cha wananchi kama lilivyo bunge. Lina mamlaka kama ilivyo kwa bunge, lina wajibu kama ilivyo bunge. Linapaswa kuheshimiwa na kupewa uhuru wa kutekeleza majukumu yake.
CCM inapoamua kilicho tofauti na kilichoamuliwa na baraza, inaonyesha tu kilivyo na mapenzi sana na siasa mgando na ubabe.
Ubabe kama huu unaoonyeshwa na NEC ya CCM unajenga utamaduni kwamba Watanzania wote lazima watii kila kinachosemwa na kuelekezwa nacho.
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho anasema: “Hakuna mtu wala chombo chenye ubavu wa kubadilisha maamuzi ya wajumbe wa BLW zaidi ya wenyewe waliopitisha maamuzi hayo.”
Anamaanisha kuwa, nje ya BLW, hakuna wa kubadilisha kilichopitishwa nalo. Si rais wala chama alicho au kingine chochote. Wala si mtu mwingine yeyote hata awe na umbo kubwa vipi.
CCM ni chama kama vingine vilivyohalalishwa kisheria. Wasidhani bado Tanzania ipo chini ya mfumo wa ukiritimba – ule wa chama dola kuamua kitakavyo na watu kulazimishwa kufuata tu.
Mfumo ule wa kishetani ulizuia Watanzania kufikiri na kuamini kinyume na viongozi wao. Uliviza akili zao na ukajenga kundi la wachache kutawala wengi. Wengi wale wakabaki mashahidi tu wa yatendwayo na viongozi.
Hawakuwa na uwakilishi hasa wa mawazo yao, bali kuishi kwa amri. CCM wanataka kubaki hapo. Wanachoamini wakubwa zake ndicho tu chema. Sote tuseme “HAPANA.”
Ukiritimba basi. Tanzania ni ya Watanzania. Zanzibar ya Wazanzibari. Wananchi wana haki ya kuheshimiwa na kusikilizwa. Wanahitaji kupewa nafasi ya kuamua watakavyo.
Zanzibar inahitaji mabadiliko. Watu wanataka maendeleo si malumbano. Wanachukua nafasi yao kuelekea kwenye ujenzi mpya. Binadamu hawa wanatumia Baraza la Wawakilishi kujiamulia hatima yao.
Ni haki yao kuachiwa maana hawafanyi ushetani. Wameamua tu kupatana baada ya miaka ya kugombana. Hapo ndipo pa kuanzia, na wanaendeleza.