CCM chanzo cha kukwama kwetu kama taifa


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 07 July 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Tafakuri
Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete

TAFAKARI ya kina juu ya rafu zinazoendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaacha ujumbe mmoja dhahiri; kwamba tatizo kubwa la kimaadili linalokabili taifa kwa sasa kiasi cha nchi kugeuka kuwa ya watu wanaoishi kwa ghilba, ubazazi, ‘misheni town’ na kila aina ya mbinu chafu zilizopotoka kimaadili, ni CCM!

Kila kukicha ndani ya CCM kuna malalamiko ya kutisha, yote kwa ujumla wake yanaonyesha ni kwa kiwango gani chama hicho kinaendeshwa kwa mbinu chafu.

Tujikumbushe kidogo, katika mkoa wa Dar es Salaam yameripotiwa matukio ya kuvuliwa uongozi kwa zaidi ya makada watano wa CCM, wote hawa ni wale wa ngazi ya chini, yaani tawi.

Kisa cha hatua hizo, moja, ni ama walitimuliwa kwa kukataa kukubaliana na mipango haramu ya kugawa kadi feki kwa nia ya kufanikisha ushindi wa baadhi ya wagombea ubunge na udiwani, au wameonekana kuwa vizingiti kwa baadhi ya wagombea; kwa hiyo zengwe limepikwa hadi likaiva.

Lakini pia kuna wanaofukuzwa kwa sababu ya kuonyesha dhahiri kutokufurahishwa na harakati za kuandikisha mamluki katika daftari la wapigakura, ukiwa ni mkakati pia wa kujipatia kura nyingi za urais, ubunge na udiwani kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Malalamiko kama haya yamesikika Iringa, Ruvuma, Dodoma, Arusha, Tabora na maeneo mengi kutaja hayo kwa uchache tu.

Wakati malalamiko hayo ya kununua wapiga kura kwa maana ya kugawa kadi feki, na hata kufanya mbinu chafu za kuandikisha watu katika daftari la wapigakura, pia kuna mbinu nyingine chafu za kumwaga fedha katika majimbo ya uchaguzi kwa kisingizio cha kuimarisha chama.

Wapo wabunge walioko madarakani wakitumia nafasi zao wamepita huko na huko wakiwahonga wanachama wenzao kwa kutoa fedha taslimu, nguo, baiskeli, simu za mkononi kwa nia moja tu, kuwarubuni ili wawakumbuke kwenye kura za maoni.

Kwa bahati mbaya mno, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ni kama imepata baridi, miguu imejaa ganzi hawataki kuchukua hatua za kweli kuthibitisha kwamba kwa vyovyote itakavyoelezwa vitendo hivyo ni viashiria tosha vya rushwa, tena ya mchana kweupe. Takukuru wana woga usioelezeka kushughulikia makada wa CCM, kisa chama tawala!

Ni kwa nini CCM wanaendesha vitendo hivi vya ukiukaji wa maadili kweupe tena mchana? Hakuna sababu nyingine yoyote isipokuwa ni kielelezo cha kuwepo kwa maelekezo kutoka juu, kwamba iwe iwavyo, wajibu wa kwanza wa watendaji wa serikali, iwe ni maofisa wa Takukuru, polisi, na watendaji wengine serikalini wakiwamo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ni kujenga mazingira ya ushindi wa kimbunga kwa CCM. Halali au haramu!

Ndiyo maana kila malalamiko ya ukikaji wa sheria yanaporipotiwa kwa kina na vyombo vya habari, husikii kauli ya Takukuru au huoni hatua zozote za maana zikichukuliwa kwa sababu kufanya hivyo ni kukwaza ushindi wa kimbunga unaoandaliwa ili tu kuwe na ushindi hata kama kuna mambo ya msingi wananchi wanaidai CCM kulingana na ilani yao ya uchaguzi ya mwaka 2005-2010 ya maisha bora kwa kila Mtanzania inawezekana!

Wakati vitendo kama hivi vikiruhusiwa kuendelea, vikifumbiwa macho na vyombo vya dola vyenye dhima ya kudhibiti kushamiri kwake, vikiangalia pembeni na kujenga taswira kwamba kila kitu kiko sawa wakati ukweli ni kwamba mchakato ndani ya chama tawala umethibitisha pasi na shaka yoyote, vitendo vya rushwa na kila uchafu, inakuwa ni vigumu kutambua kwamba hao viongozi watakaochaguliwa Oktoba mwaka huu watakuwa na wajibu gani wa kimaadili (moral authority) wa kupiga vita rushwa na machafu yote ndani ya serikali?

Ni kiongozi gani anaweza kujitwika wajibu wa kimaadili kupigana na rushwa, uonevu, ubazazi, na kila aina ya ghilba ndani ya serikali kama mchakato aliopitia kufikia ofisi ya umma ilijaa vitendo hivyo?

Je, huku si ndiyo maana ya kuhalalisha rushwa na uchafu wote katika ofisi za umma?

Je, kiongozi ambaye alitumia fedha zake za mfukoni kununua wanachama wake wakampigia kura kwenye mchakato wa kura ya maoni; na baadaye kutumia fedha hizo hizo kununua shahada za wapigakura kwa sahani ya ubwabwa au fulana, au kofia, hivi anawajibika vipi kwa wapiga kura wake ambao aliwanunua?

Na ni kwa nini awajibike wakati alichaguliwa kwa sababu ya mbinu zake chafu na si kwa sababu ya uwezo wake wa kuwa kiongozi bora kati ya wagombea wote waliojitokeza?

Kwa wale watumiaji wa kompyuta wanatambua neno –GIGO- yaani Garbage In Garbage Out – kwa tafsiri rahisi (taka zinazoingia ndizo zinazotoka) ukifafanua zaidi katika uhalisia wa maisha yetu ya kila siku ni kwamba mtu huvuna kile apandacho.

Aina ya uongozi tunaoupata kuanzia ngazi ya kata (madiwani) na baadaye majimboni (wabunge) na pengine hata ngazi za juu zaidi, ni matokeo ya mchakato mchafu wa kuchujana si kwa ubora ila kwa hila, mbinu chafu na kila aina ya ghilba.

Ni kwa nini diwani au mbunge aliyetumia mamilioni kusaka kura aumize kichwa juu ya kukosekana kwa maji safi mtaani kwake, au kuzagaa kwa taka ngumu au majimaji mtaani kwake?

Hawezi kuwaza hayo kwa kuwa akili yake imetopea katika uovu, katika kuvuruga kanuni, taratibu na sheria; kwake kinachomsumbua ni kwa jinsi gani umimi wake utatumikiwa na si kutumikia umma.

Kwa hiyo tunaposaka majibu ya kiini cha kukwama kwetu kama taifa hata katika mambo mepesi sana ya kutekeleza tu wajibu wa kawaida mno, inatubidi kutafakari ni njia ipi basi tunapata viongozi wetu?

Je, ni mfumo unaochuja mabazazi na kuleta kile kilicho bora zaidi au ni kinyume chake? Kwa hakika bila kutafuna maneno, ubazazi ndio umefunika ubora wa kila kitu.

Unapokuwa na chama tawala kinachoruhusiwa kuendesha mambo kana kwamba usimamizi wa sheria na kununi za kusimamia nchi zimeahirishwa, basi ujue wazi kwamba huo ndio mkondo wa kutuletea madarakani watu wasiofaa.

Ni kwa maana hii hautakuwa uchimvi kusema kwamba kwa mchakato wa ndani ya CCM chama ambacho kinashinda viti vingi vya ubunge, udiwani na hivyo kuunda serikali kuu na halmashauri nyingi za majiji, manispaa, mija na wilaya, utatuwekea madarakani viongozi waliotumia rushwa na kwa maana hiyo rushwa ni ndugu nao, na ni chanzo cha kukwama kwetu kama taifa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: