CCM na dhambi ya uraia


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 18 August 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Tafakuri

MWAKA baada ya mwaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) bila kujijua kina utamaduni wa kujirudia katika madhambi yake.

Wakati utawala wa awamu ya tatu unaelekea ukingoni baada ya Rais Benjamin Mkapa kutetea kiti chake cha urais vizuri mwaka 2000, mwaka 2002 CCM ilifanya uchaguzi wake mkuu kama ilivyo ada.

Matokeo ya kura hizi yalizua malalamiko mengi kwani yaliakisi kitu kilichobatizwa jina la ‘kura za itifaki’.

Kwa maana kwamba walioongoza kwa idadi kubwa ya kura za kuwania nafasi ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ndio hao hao walikuwa viongozi wakuu wa kitaifa ama serikalini au kwenye chama.

Kura hizo kwa wadadisi wa mambo waligundua kwamba zilichezewa, na wakati huo wapo watu waliumizwa na ‘uhuni’ huo, mmojawapo wakati huo alikuwa Rais Jakaya Kikwete.

Ni katika moja ya mikutano ya juu ya chama iliyofanyika Zanzibar Kikwete kwa kujiamini aliamua kuwaga “nyongo” jinsi alivyokuwa anaandamwa kwa majungu na mchezo ‘mchafu’ wa kummaliza kisiasa.

Haya yote yalifanyika kwa kuwa tu alikuwa na ndoto za kuusaka urais. Waliokuwako kwenye kikao hicho wanakumbuka kwamba hali ilikuwa tete kwa maana ya neno hilo .

Lakini maana ya kura za itifaki ilikuwa ni nini? Ilikuwa ni kuwapa ushindi watu wasiostahili, kuwajengea kukubalika ndani ya chama kwa kutumia mkono wa nguvu za dola, kama wanausalama, huku wengine wakihujumiwa.

Hii ilikuwa ni dhambi mbaya na kuna ushahidi kwamba Rais Mkapa wakati huo akiwa Mwenyekiti wa CCM aliikemea sana, na huenda ndiyo ilikuja kuwatafuna mahasimu wa Kikwete kwenye mchakato wa kuwania kuteuliwa kugombea urais miaka miwili baadaye, yaani 2005.

Lakini mbali na dhambi hii ya kucheza na kura za watu, kama ambavyo imetokea huko Moshi Mjini, Iringa Mjini, Nzega na Njombe Magharibi, safari hii ile dhambi ya rangi, kubaguana kwa ‘gia’ ya uraia imejirudia tena.

Hakuna asiyekumbuka jinsi mwanasiasa na mwandishi mwandamizi, Jenerali Ulimwengu, ambaye si tu alijitoa mhanga kuhakikisha Rais Mkapa anashinda uchaguzi wa mwaka 1995, bali pia alitumia vyombo vyake vya habari wakati huo, magazeti ya Rai na Mtanzania, lakini akiambulia shukrani ya punda.

Alikuwa ni Jenerali aliyekuja kuwa adui mkubwa wa utawala wa Mkapa kiasi cha kunyang’anywa uraia wake pamoja na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Timothy Bandora, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kagera, Anatory Amani na Naibu Katibu wa Itikadi na Uenezi Zanzibar, Moudiline Castiko.

Si nia yangu kujadili sababu za kila mmoja kunyang’anywa uraia miongoni mwa hawa, ila itoshe tu kusema ni matokeo ya kumalizana ama kisiasa, kulipizana kisasi au kunyamazishana.

Hatua za kunyang’anywa uraia pia ilipata kumpata waziri wa zamani wa utawala wa Mwalimu Nyerere, Austin Shaba; na aliyewahi kuwa Waziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Aboud Maalim. Wote hawa walifikwa na hayo kwa sababu moja tu, kutofautiana na wakubwa!

Tukirea kwenye maamuzi ya CC ya CCM kumtangaza kada wao si raia akiwa pia kiongozi wa Umoja wa Vijana, Hussein Bashe, huwezi kukimbia nje ya sababu zile zile za miaka yote. Kushughulikiana, kudhibitiana, kukomoana au kunyamazishana!

Ni vigumu kuamini kwamba miaka takribani 50 baada ya uhuru, bado tunashikamana na hisia za uraia katika bara la Afrika lilikatwa vipande vipande na wakoloni mwaka 1884/85 huko Berlin Ujerumani ili watulawale.

Lakini ni ajabu zaidi kwamba Tanzania ambayo wimbo wake wa taifa unasifu Uafrika wetu, na imani ya TANU ambayo CCM ilirithi kwamba Afrika ni Moja, vinadhihirika kuwa ni kauli za mdomoni tu ambazo hazigusi kwa njia yoyote mioyo ya watawala wetu.

Tanzania ilikuwa kimbilio la Waafrika wote, wanaobaguliwa au kunyanyaswa kwao kwa sababu ya mitizamo yao ya kisiasa, ndiyo maana chini ya utawala wa Mwalimu watu wengi walipewa makazi, na rasilimali nyingi za taifa kutumika kuwatunza. Walihesabiwa kuwa ni raia.

Kwa mfano, Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, mara zote huwa hafichi ukweli huu wa masimamo wa Tanzania wakati ule, kwamba baba yake, Jaramog Odinga, alipata kumtuma kwa Mwalimu Nyerere ambaye alimpatia hati ya kusafiria kwenda Uingereza kusoma baada ya serikali ya kikoloni kumnyima hati hiyo nchini Kenya.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba katika zama za sasa bado siasa chafu za kutumia uraia kama silaha ya kuangamizana inatumika kwa yeyote anayeonekana ama kuwa na ujasiri wa kukataa kukubaliana na mambo fulani ‘machafu’ yanayotokea na kupewa baraka na wakubwa.

Lakini kinachoumiza zaidi ni pale hatua kama hizo zinaposimamiwa au kufanywa mbele ya wale waliolalamika kuhujumiwa kwa njia ambazo si haki kama zile kura za itifaki za mwaka 2002.

Ni vigumu kuzungumzia ‘kukatwa kichwa’ kwa Bashe bila kutazama ugomvi wa madaraka na mivutano ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), ni vigumu kumtazama Bashe nje ya mkono uliomshughulikia aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM,

Hamad Yusuf Masauni; lakini pia ni vigumu kukubali kwamba Bashe anaweza kuwa tu alishughulikiwa kwa bahati mbaya huku ‘haki’ kama hiyo ikimpita kando Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, ambaye kundi la wazee kutoka Kilosa liliwasilisha tuhuma zake, lakini kwa sababu yumo kwenye mstari na wakubwa amesafishwa.

Ni kwa maana hii mtu anashindwa kufikia hitimisho kwamba CCM haina dhambi ya msimu ambayo hujirudia kila wakati.

Haya yalimpata Jenerali, kada asiyetiliwa shaka kwa kazi za CCM alizofanya, dhambi hiyo hiyo iliachwa imtafune Castiko, Amani na sasa Bashe.

Lakini wahenga walisema ukiishi nyumba ya vioo usiwe wa kwanza kurusha mawe, na kila kiendacho mbali, hurejea. Silaha ya uraia itaendelea kuitafuna CCM miaka mingi ijayo.

Tatizo la CCM ni kwa wale walioko madarakani kusahau kwamba ni nafasi za kitambo kidogo tu na baadaye watarejea kuwa watu wa kawaida kama wengine tu. Ni vema wakachukua hadhari kwa sababu laana ina tabia ya kufuata ukoo hadi kizazi cha tatu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: