CCM ikubali kushindwa


editor's picture

Na editor - Imechapwa 29 December 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

TANGU kumalizika kwa uchaguzi mkuu nchini matukio mengi yametokea ikiwa ni mwendelezo na utamaduni uliozoeleka kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuamini katika mabavu.

Kama ilivyokuwa katika maeneo ambako chama hiki kilionekana kushindwa uchaguzi, ambapo kilichochoea vitendo vya vurugu, ndivyo ilivyofanya katika uchaguzi wa umeya.

Pale ilipoona wagombea wake hawawezi kushinda kutokana na idadi ndogo ya madiwani, viongozi wao waliamua kuvuruga utaratibu ili kubeba chama chao.

Mfano hai, ni halmashari za Manispaa za Arusha na Mwanza ambako kilikabwa koo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Katika Manispaa ya Arusha, viongozi wa CCM pamoja na kutambua wazi kwamba mbunge wa Viti Maalum kutoka mkoani Tanga, Mary Chatanda, hakuwa na sifa ya kisheria ya kupiga kura, walilazimisha ashiriki uchaguzi.

Naye, bila aibu mkurugenzi wa Manispaa, Estomii Chang’a alikubali kutumiwa na chama hicho kubariki uvunjaji huo wa sheria.

Ni hatua yake hiyo ilizusha zogo ambapo kila mmoja analiona leo. Kwamba mkoa wa Arusha na taifa kwa jumla linakabiliwa na hatari ya kutokea machafuko ya kisiasa.

Mkoani Mwanza, Wilson Kabwe, mkurugenzi wa manispaa hiyo amefanya yanayofanana na yale ya Arusha.

Umekuwa utamaduni wa CCM kuhadaa ulimwengu kwa kuhimiza viongozi wa upinzani kukubali kushindwa, wakati ambapo wao vinara wa kucheza rafu na kuvunja taratibu.

Ni lazima viongozi wa CCM wajue kwamba demokrasia inahitaji uvumilivu wa kisiasa kuonyeshwa na kila mshiriki. Haiwezi kuhubiri amani, wakati inatenda vita.

Hivyo basi, tunachukua fursa hii kuwahimiza viongozi wakuu wa CCM wajifunze kutoka kwa mataifa mengine ambayo tayari yamejitumbukiza katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Na kwa kuwa ndani ya taifa hili, hakuna mwenye hatimiliki ya utawala, tunalaani kwa nguvu zote vurugu zote zinazotokea. Tunasisitiza, tena na tena, kwamba ni lazima maoni ya wananchi yaheshimiwe.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: