CCM imelogwa na CCJ

KATIKA siku za hivi karibuni tumeshuhudia vituko na maajabu, na sitashangaa iwapo siku si nyingi zijazo tutaona miujiza.
Kwa mfano, inawezekana vipi chama ambacho hakijapata hata usajili wa kudumu, hakina viongozi wenye majina makubwa, hakina ofisi ya kueleweka na waanzilishi wake ni watu ambao hawakuwa wanajulikana, kikawa mwiba mkali kwa chama ambacho kimekuwa madarakani kwa takribani 50 sasa?
Inawezekana vipi wanasiasa wakongwe waliobobea katika siasa za nchi hii wake chini na kuzungumzia chama ambacho hakipo? Ukweli ni kuwa haingii kichwani kuwa Chama cha Jamii (CCJ) ambacho kimepata usajili wa muda majuzi tu, kikiweweseshe Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwangu, haya ni maajabu!
Inapotokea CCM kikalazimika kutoa maelezo marefu dhidi ya chama ambacho hakijapata usajili wa kudumu hadi kufikia hatua ya viongozi wake kuwasihi wananchi wasitishike na ripoti za magazeti yanayokipamba chama hicho - chama ambacho hakina uhakika wa kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu - ni lazima hapa kuna walakini.
Hata uamuzi wa kukisajili uko mikononi mwa CCM yenyewe inayohodhi ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Ikisema CCJ kisajiliwe, itakuwa hivyo, maana hata John Tendwa mwenyewe ni mwana CCM. Tendwa hana ubavu kutenda kinyume cha maagizo na matakwa ya CCM.
Huu ndiyo msingi wa maelezo ya Tendwa kwamba CCJ hakitashiriki uchaguzi mkuu ujao. Hapa ndipo watu makini wanajiuliza: Kuna nini kati ya Tendwa na CCJ?
Kwanini CCJ kijikute kinatupiwa madongo hata na wapinzani wa CCM, kwa vile tu kunakisiwa kuwa endapo kitatokea jinsi inavyotarajiwa, basi hata upinzani utaathirika?
Sababu zipo. CCJ kinatabiri kuanguka kwa mfumo wa utawala wa kifisadi (MUK) – hata kabla hakijakomaa.
Kimsingi CCJ kinawaumiza kichwa watawala kwa kuwa ni chama ambacho kinaweza kuleta mwamko mpya.
Ndiyo maana wangependa kujua sana ni kina nani wako nyuma ya chama hicho. Nina uhakika kwamba kama wapo Watanzania waliokuwa wanasubiri kuzaliwa kwa chama kipya, wanajiuliza kama ndicho hiki.
Binafsi ninajua majibu baadhi ya maswali hayo. Nakiri kwamba mwaka huu CCM hakiwezi kushinda uchaguzi kama kilivyozoea. Inabidi kifanye hila za kutosha ili kishinde hivyo.
CCM ni chama ambacho, kwa sababu za kihistoria, kinakubalika na kinadai kimekumbatiwa na Watanzania zaidi ya milioni nne. Kimeshika hatamu na utamu wa taifa letu kwa miongo minne na nusu sasa; kimejikita katika fikra, mawazo, maisha na mioyo ya Watanzania kiasi kwamba wazo la chama kingine chenye uwezo kama huo ni kama haiwezekani.
Hata hivyo, ukweli ambao unatuangalia mbele yetu kama simba aliyekutana na swala njiani ni kuwa CCM kilivyo sasa hakiwezi kuendelea kutawala. Kwa vile tumeshaona kwa mara nyingine kuwa maslahi ya CCM yako juu ya maslahi ya taifa, pole pole Watanzania wameanza kuzinduka.
Na kwa vile dalili zote zilizopo sasa hivi zinaonyesha kuwa CCM haiwezi kujisafisha (kwa sababu haikubali kuwa imechafuka), na kwa vile ni wazi kwamba juhudi zozote za ndani za kukisafisha haziwezi kufanywa na watu ambao hawakubali kuna uchafu, ni wazi kuwa ujio wa CCJ unatisha kwa chama tawala, maana kinajua wananchi wanahitaji chombo mbadala – ambacho kinaweza kuwa chochote (hata CCJ).
Naomba niwe wa kwanza kuwahakikishia kuwa CCJ itapata usajili wa muda na wa kudumu na kinyume cha maombi za kina John Chiligati na Yusuf Makamba. CCJ kitashiriki uchaguzi mkuu mwaka huu.
Wagombea wake watashiriki uchaguzi mkuu aidha kwa kupitia chama hicho au kama wagombea huru . Siyaamini maneno ya Philip Marmo; kutakuwepo wagombea huru mwaka huu.
Mwanzoni nilikuwa nafikiria sana uwezekano wa mabadiliko ya kweli kutokea kwenye uchaguzi wa 2015, lakini sasa hivi nimeamua kusahihisha mawazo yangu kwani dalili zote zinaonyesha kuwa nafasi pekee ambayo Watanzania wanayo kuleta mabadiko kwa taifa lao itakuwa ni mwaka huu.
CCM nao wanalijua hili, ndiyo maana wanahaha kuzuia vyama vingine kuzaliwa na kukua. Ndiyo maana wanakisakama CCJ hata kabla hakijapata usajili wa kudumu.