CCM imemteua Raza, imejinusuru


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 18 January 2012

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

WAKATI huu ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanya kile walichokitarajia wananchi wa jimbo la Uzini, wengine wananuka.

Nimesimuliwa kuwa wapo viongozi waliochukizwa na nilichokieleza wiki iliyopita. Tatizo hawa ni wachache mno – hawajai hata mkono. Hawa ni viongozi maslahi na wazibaji riziki kwa wengine.

Katika jimbo la Uzini, wapo viongozi waliojaa woga wa kuadhirika. Wao wamekuwepo kwa miaka mingi, hawajasaidia wananchi. Hawawajali. Bali bado wanatamalaki madaraka.

Viongozi hawa wamewaingiza mkenge wananchi wanyonge kwa kuwatumia katika walichodai “Barua ya Wazi kwa Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete.”

Hawajui mwenzao ana mtandao mkubwa. Anasoma alama za nyakati. Amechoka kuingizwa mjini kila siku na wapuuzi, wakiwemo makada wa CCM waliochoka kama hawa wenye maslahi jimboni Uzini.

Eti wanajimbo hao wamejigamba kuwa wanaenzi mapinduzi ambayo wazee wa jimbo walichangia sana kuyafanikisha. Kutaka Raza achinjiwe baharini kihila kama alivyopata kufanyiwa Adamjee jimboni Kawe, ni kuenzi mapinduzi!

Ninaamini Haji Juma Kibwana anayetajwa kutoka kijiji cha Uzini; Omar Haji Moh’d anayetajwa kutoka Umbuji; Kassim Juma Khatib anayetajwa kutoka Mgeni Haji, Selemani Bakari Bushiri anayetajwa kutoka Tunduni, Fatma Herezi Said anayetajwa kutoka Bambi na Mustafa Khamis Mustafa anayetajwa kutoka Kiboje hawakujua athari za walichotumwa kukifanya.

Kama walijua, waseme, leo hii wanajisikiaje kuwa ile kampeni dhaifu waliyoianzisha kwa siri, ya kuwasiliana na Mwenyekiti Kikwete imefika wapi? Hawajui siasa zinazingatia upepo. Uendapo kusini huwezi kugeuka jiwe ukataka kulazimisha dau lako liende kaskazini tena kwa kasi.

Wananchi wanyonge hao sita pamoja na wakubwa zao waliowatuma kujihangaisha, wamesahau haijawahi kutokea mtu akatoka shujaa baada ya kupiga ngumi ukuta. Ukweli wa mambo, mwisho wa ngumi zake, ni mtu huyo kuumia mkono na kuanguka pwaa.

Wanajimbo hao na wakubwa zao wameanguka pwaa. Hawana pa kushika, kupita na kutamba sasa. Hawana. Wanaona haya tu. Na kwa namna walivyotupwa, hawatamani kuhangaika tena.

Hawajui kupigana. Mike ‘Iron’ Tyson alipomkata sikio mshindani wake Evander Holyfield sekunde tu tangu walipoanza kupambana ulingoni, hakufanya vile kwa bahati mbaya. Alijua lile jamaa lina nguvu na ufundi kumzidi. Alijua isingekuwa rahisi kumshinda.

Mohamed Raza alipoamua kuchukua fomu kuomba CCM imteue kugombea uwakilishi Uzini, alijua anaingia kibaruani kwelikweli. Hakutania, wala hakutenda fitna. Alijua fitna mbaya hazina haya.

Ameamua kuzama mifupani mwa siasa za uongozi baada ya kutumia siasa za kishabiki. Raza amekua sasa. Anajua kuwa huu ndio wakati hasa ambao anapaswa kuutumia kuonesha dhamira yake kwa maslahi ya wanyonge.

Raza amekuwa karibu na wananchi muda mrefu lakini ilionekana zaidi akibeba viongozi. Pale alipotembelea majimbo yote 50 ya Zanzibar, alikuwa akiimarisha wakubwa kisiasa zaidi kuliko kujiimarisha yeye.

Alipogawa zana za kilimo – mapanga na majembe katika majimbo hayo – alikuwa anajenga taswira kuwa wananchi wanahitaji nyenzo za kupata maendeleo siyo fedha za siku mbili tatu ambazo angeweza kuwapa.

Raza anarudi kwenye siasa halisi. Sasa anataka kutumikia wanyonge moja kwa moja bila kupitia mgongoni mwa mtu yeyote.

Anataka kufanya hivyo kwa kutumia fedha alizonazo ambazo amekuwa akisema zimetokana na majaaliwa ya muumba maana kama ni nguvu za mwili tu, kila mtu anazo. Basi kila mtu angekuwa tajiri.

Raza anajua siasa za kelele hazina tena nafasi Tanzania. Anajua viongozi waliochaguliwa huko nyuma wengi ni wapigaji kelele bila ya kuonesha moyo wa kusaidia wananchi kupata huduma bora.

Na ni viongozi haohao waliojiotesha majimboni lakini hawajasaidia ujenzi wa barabara, vituo vya afya, vituo vya kulelea watoto fukara, kusaidia kupeleka watoto sekondari za kisasa pamoja na vyuo vikuu akianzia na kuzipatia zana za kisasa maabara katika sekondari.

Hizi ndio changamoto mbichi zilizoko jimboni Uzini ambazo kwa miaka mingi viongozi maslahi wameziona, wakaishi nazo na wakashindwa kuzitafutia ufumbuzi. Bado wamebaki viongozi.

Raza ameamua kuingia kuzifanyia kazi. Ziara aliyoifanya kwenye vijiji vya jimbo wakati akitafuta kura za maoni ndani ya chama chake, ilimpa fursa nzuri ya kuona matatizo ya msingi yanayokabili wananchi.

Kuna tofauti kubwa ya makada wa CCM waliojiotesha majimboni na Raza ambaye hajapata kuwa kiongozi mwakilishi jimboni. Wale wanajisikia yeye anakumbuka fadhila.

Wananchi wa Uzini hawahitaji kiongozi shupavu tu kwa kumuona akitunisha mishipa ya uso na shingo wakati akihutubia. Wanataka kiongozi mweledi, mwenye huruma na anayependa watu.

Wanahitaji kiongozi aliyetayari kutumwa, na siyo kila siku kuwa mbali huku akiishi kwa kutoa maagizo na maelekezo kupitia wasaidizi wake.

Raza alianza kutajwa sana alipoanzisha duka la vifaa vya michezo. Akaja kupanda majukwaani wakati Dk. Salmin alipokuwa rais. Baadaye aliteuliwa na waziri aliyehusika na michezo kuwa mwenyekiti wa kamati ya Saidia Zanzibar Ishinde (SAZI).

Jukumu kubwa lilikuwa kuiandaa timu ya taifa Zanzibar.

Nguvu zake katika majukumu ya kamati zilichangia kuiwezesha Zanzibar kutwaa kwa mara ya kwanza Kombe la Challenge, kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati mwaka 1995.

Wakati huohuo, Raza ndiye aliyekuwa mfadhili mkuu wa timu ya Shangani iliyoshiriki kwa mafanikio michuano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, nchini Sudan.

Pia alisaidia ushiriki wa timu ya soka ya vijana ya Zanzibar katika michuano ya Afrika Mashariki na Kati iliyokuwa ikiundwa na kina Sabri Ramadhan China.

Sambamba na kufadhili soka, Raza alitia pesa nyingi pia kwenye netiboli. Alizisaidia timu binafsi na za taifa. Timu za michezo mingine, zikiwemo za vikosi vya ulinzi zilinufaika.

Wakati akifanya hayo michezoni, katika siasa, Raza alijenga matawi na maskani nyingi za CCM Unguja na Pemba. Alijenga misikiti mingi maeneo ya nchi.

Raza aliteuliwa na Dk. Salmin kuwa mshauri wa mambo ya michezo. Aliweka nguvu kubwa katika kukuza michezo ngazi ya taifa.

Wapo wanaoamini kuwa sehemu kubwa ya fedha alizotumia kufadhili michezo na CCM ilitokana na faida kubwa kwa biashara alizofanya huku akikingiwa kifua na serikali.

Miaka ya nyuma, alikuwa muagiziaji wa vyombo vya usafiri kama vespa na magari, mengi akikopesha kwa watumishi serikalini.

Mpaka sasa, Raza anajishughulisha na biashara ya uzalishaji viwandani na anamiliki kwa ubia kampuni ya upakiaji na utoaji mizigo kwenye uwanja wa ndege iitwayo ZAT.

Nguvu zake zilipungua pale alipotengwa na serikali iliyoongozwa na Amani Abeid Karume, baada ya uchaguzi wa 2000. Kipindi chote hicho hadi sasa, Karume amebaki makamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar.

Lakini kwa muda wote, Raza amebaki kada wa CCM. Amesaidia kwa hali na mali alipoitwa kutia nguvu. Raza ana sababu nyingi za kujinasibisha na CCM. Chama hicho ndicho kilimtoa mbali, hawezi kukipuuza.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: