CCM imeshindwa: Kwa nini hatuamini?


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 13 July 2011

Printer-friendly versionSend to friend

NAKUMBUKA kisa cha mbeba magunia mmoja maarufu kwenye Soko la Makorola mjini Tanga miaka mingi iliyopita. Toka enzi za ujana wake alikuwa anajulikana kwa uwezo wake kwa kuinua na kubeba magunia na hata mizigo mingine ambayo ilikuwa ni mizito sana kwa watu wengine. Kutokana na uwezo wake wa kupakia na kupakua mizigo mbalimbali alijulikana pale sokoni kwa jina la bingwa.

Bingwa alikuwa analipwa ujira tofauti na wabeba magunia wengine na ilikuwa kwamba ukitaka mizigo yako itoke au ifike salama sokoni basi uliza tu kwa jina hilo na Bingwa hakuchelewa. Miaka mingi ya kazi hiyo ya kunyanyua viroba, magunia, na mizigo pale sokoni ilianza kumchosha na kwa kadiri umri ulivyozidi kwenda ndivyo alivyoonekana kama “superman” kwani bado aliwashinda vijana wengi kwa kazi ile ile. Alikuwa bingwa kweli. Alitungiwa wimbo na kuitwa “nambari wani”, yaani yeye wa kwanza hakuna mwingine.

Siku moja nilipeleka machungwa yangu pale sokoni nikitokea Muheza na asubuhi na mapema wakati watu wanashusha mzigo wangu nikasikia sokomoko upande kidogo tu wa pale nilipokuwepo. Nikimuacha kijana kufuatilia nilisogea nami kushuhudia ni kitu gani kimewavuta watu hisia na akili zao asubuhi ile. Ndugu zangu, ilikuwa ni siku ya kihistoria sokoni pale; Bingwa aliangusha mzigo wa mteja. Mzigo uliowashinda vijana na kuamua kuomba msaada wa Bingwa.

Bingwa alipokuja kama kawaida yake bila makeke wala mbwembwe nyingi aliwabeza vijana kiutani na kuwaambia “kaeni pembeni niwaoneshe kazi”. Kweli zigo likawekwa mabegani pake lakini lahaula lakwata! Bingwa kayumba. Akajaribu kuliweka vizuri mabegani miguu ikanesa kidogo. Watu wakaguna. Akajiweka sawa. Akajaribu kupiga hatua moja mbele, Bingwa kashindwa. Akalitua limzigo chini, puu!!

Wapo walioguna lakini wengi waliangusha kicheko. Vijana wakaanza kumtania na kumuambia “mzee staafu sasa”. Lakini Bingwa alikuwa Bingwa. Akaanza kujitutumua, kutunisha misuli huku akiwatania kuwa alikuwa anawafurahisha tu na mzigo ule angeweza kabisa kuubeba. Akautikisa tikisa kidogo akawaambia vijana wamsaidie kuuweka vizuri nzigo ule mgongoni “kwani ulikuwa haujakaa sawasawa” pale mwanzo.

Bila ajizi vijana wakasimama pande mbili mzee akachutama kidogo wakamtwisha zigo. Pembeni kundi la mashabiki wake wakawa wanapiga makofi “bingwa bingwa, nambari wani nambari wani”. Miluzi na vigelele vya kumtia moyo vikasikika. Toba salaleh! safari hii akaenda nalo chini na kuulamba udongo.

Sauti ikasikika ya chizi mmoja ikisema, “Mtamuua huyu mzee.” Bingwa akaulizwa swali “umeshapata kifungua kinywa, isije kuwa njaa.” Mzee akasema bado. Kwa vile sasa ilikuwa ni drama ya kulinganisha uwezo wa Bingwa na mteja, hakuwa na haraka maana ilikuwa ni soga soko zima asubuhi ile.

Kwa karibu miaka thelathini mzee Bingwa hajawahi kuonekana kuangusha zigo la mteja. Habari zikaanza kuvuma “Bingwa kaangusha mzigo.” Marafiki wake wakajitokeza, vijana aliowafundisha wakaja kwa haraka, kuja kushuhudia. Bingwa akaomba udhuru aende kupata kifungua kinywa kwanza. Huku nyuma vijana wakaamua kupunguza uzito wa ule mzigo, wakaufungua kwa haraka na baada ya kupunguza vilivyokuwemo wakajaza vitu vingine vyepesi na kuufunga na kuaacha pale pale chini.

Muda kidogo mzee karudi tena. Hajui kilichotokea zigo likimngojea. Kelele za kumtia moyo, miluzi ya kumpa shime, akaomba tena vijana wawili wamsaidie. Vijana wakajipanga mzee kachuchuma zigo likawekwa begani, likatulia. Mzee akalitikisa kidogo likatulia. Akapiga hatua ya kwanza, na ya pili; huku anashangiliwa. Mzee wa watu akaubeba mzigo hadi kwenye gari la mteja, huku akishangiliwa, mwenyewe tabasabu juu. Aliporudi akawaambia wale vijana washibe kwanza kabla ya kazi. Wote wakamuitikia.

Miezi ilivyopita alijikuta anapata shida kuinua hata mizigo aliyoweza miezi michache nyuma. Alijua kuwa asingeweza na kazi hiyo tena. Akabakia mmoja wa wapiga stori pale Makorola kwa muda mrefu. Watu walimtania na kumkumbushia siku ile huku yeye mwenyewe akiwaelezea na kujisifia jinsi alivyoweza kuwaumbua vijana. Miaka michache ilipita Bingwa alifariki dunia; alifariki akiwa na imani kuwa alikuwa kweli Bingwa. Siri yake ilikuwa inajulikana. Siku ya mazishi yake watu walisimulia kisa kile, na kucheka na kutabasamu.

Ndugu zangu, CCM ni chama kilichoshindwa zigo. Wana CCM na uongozi wao miaka nenda wameliaminisha taifa kuwa wanaweza. Wamepiga magoti kila baada ya miaka mitano tuwabebeshe zigo la maendeleo na maisha ya watu wetu. Na sisi tukiamini kuwa wanaweza tumeshindwa kabisa kugundua kuwa wamepoteza uwezo wao wa kuliongoza taifa. Wamepoteza nguvu walizokuwa nazo miaka hamsini iliyopita. Wamezeeka kama chama na sasa wamebakia kujitutumua.

Yaliyotokea uwanja wa taifa siku ya Jumapili, na kukatika kwa umeme karibu nchi nzima (kwa kisingizio chochote kile) ni dalili tu ya kushindwa kwao. Ndugu zangu, upungufu wa chakula na tishio la njaa linalokabili robo tatu ya taifa letu havijatokea kwa bahati mbaya. Sisi wengine katika wazimu na kukosa kwetu uzalendo (kama wakosoaji wetu wanavyotuita) tuliangaliza juu ya hilo miaka mitatu iliyopita. Hatuna sababu katika aTanzania ya kwanini kuna upungufu wa chakula wala kwanini kuna tatizo la umeme.

Vyote hivi ni dalili ya chama kilichopoteza uwezo wake, kilichopoteza maono yake na sasa kimebakia kutukumbushia historia yake ya sifa ya huko nyuma. Wamebakia kuimba nyimbo, wakitoa tambo kwa majigambo kwa maneno matamu kama ulimbo. Napo wengine pembeni wanawashangilia, wanacheka nao, wakiamini kuwa labda watanyanyua zigo hili. Ndugu zangu, niwe mbebaji wa habari mbaya, zigo haliendi popote.

Wanaoingalia CCM kama suluhisho la matatizo na siyo chanzo cha matatizo hayo watahukumiwa na historia. Ndugu zangu, CCM imejitahidi - hili halina shaka. Wamebebea mizigo mbalimbali - hili halina mjadala.

Lakini jamani hii siyo CCM ile. CCM siyo TANU (isipokuwa kwa kuangalia picha tu).  Watanzania wanatakai waamke na kutambua kuwa tunahitaji mbebaji mwingine mwenye uwezo; mbebaji ambaye anajua uzito wa tatizo.

Naam, huyo mbebaji yupo na anaweza kusema yuko njiani kuja na kusimama kubebeshwa zigo hilo. Je, tuko tayari au tunataka CCM wavue na mashatii na kukunja misuli tuamini kuwa labda “safari hii wataweza”. Inasemwa asiyekubali kushindwa si mshindani; CCM ikubali kushindwa. Iombe msaada wa kutawala, wa mawazo, wa fikra labda - labda - itaweza kupiga hatua mbili tatu mbele.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu:
mzee mwanakijiji unazungumza ukweli mpaka inakua shida kwa watawala wenye dhamana kuyakataa. Natumaini wanaupata ukweli na chachu ya maovu yao.