CCM ina shahada ya kuzomea


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 28 December 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

BILIONEA Henry Ross Perot alitikisa Marekani alipojitokeza kuwania kiti cha urais akiwa mgombea binafsi mwaka 1992 na 1996.

Perot mwenye utajiri unaomfanya ashike nafasi ya 99 nchini Marekani, alisisimua kwa kauli, ushauri na siasa huru.

Kuhusu uchumi alisema, “Udhaifu wa shilingi ni ishara ya uchumi dhaifu, na uchumi dhaifu unadhoofisha taifa.”

Aliongeza, “Bajeti lazima iwe kamilifu, hazina ijazwe ‘minoti’, deni la taifa lipunguzwe na maringo ya maafisa wa serikali yadhibitiwe.” Je, kuna la kujifunza?

Juni mwaka huu, baada ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo kusoma Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/2012, kambi ya upinzani ilisema serikali ya CCM imepotosha.

CHADEMA, wanaoongoza kambi, walisema “bajeti si kamilifu, haina urari katika tarakimu, Hazina mufilisi na wanachoambiwa wananchi si kilichomo vitabuni.”

Wabunge takriban wote wa CCM, baada ya kuona serikali imeachwa uchi, waliacha kujadili bajeti; dakika tano walipongeza ‘wapenzi’ na ‘totoz’ halafu dakika 10 kuponda maandamano ya CHADEMA.

Miezi sita baadaye walichosema CHADEMA kimedhihiri. Serikali imeagiza ajira serikalini katika mwaka wa fedha 2011/2012 zipunguzwe kwa asilimia 50 na imepunguza upandishaji vyeo kwa asilimia 50. Kisa? Serikali haina fedha.

Wakichangia bajeti CHADEMA walisema wakati serikali imetaja kipaumbele cha kwanza cha bajeti kuwa ni kumaliza tatizo la umeme na kwamba imetenga Sh. 537 trilioni, upembuzi waliofanya kwenye vitabu vya bajeti (Kitabu Namba II na IV) vilivyotolewa na serikali yenyewe, walibaini kuwa Wizara ya Nishati na Madini imetengewa Sh. 402,402,071,000 kwa mujibu wa fungu la 58.

Walisema fedha hizo zimegawanywa katika mafungu ya matumizi, kawaida Sh. 76,953,934,000 na kwa upande wa maendeleo zimetengwa Sh. 325,448,137,000.

Pia CHADEMA walisema, wakati serikali inawaaminisha Watanzania bajeti imeongezeka kuliko mwaka uliopita, ukweli hakuna ongezeko lolote.

Walisema bajeti iliyopita ilikuwa Sh. 11.6 trilioni wakati mwaka huu bajeti ya jumla ni Sh. 13.525 trilioni. Kati ya fedha hizo, kiasi cha Sh. 1.901 trilioni sawa na asilimia 14.06 ya bajeti yote, kitatumika kulipia deni la taifa.

Kwa mantiki hiyo, fedha kwa ajili ya kuendesha serikali pamoja na kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ni Sh. 11.624 trilioni, sawa na fedha za bajeti ya 2010/2011.

Katika eneo la tatu la upotoshaji, kambi ya upinzani ilisema wakati waziri akisema bajeti itapunguza posho kama sehemu ya mkakati wa serikali kubana matumizi, ukweli katika bajeti hiyo zimetengwa Sh. 2.987 trilioni, (asilimia 13 ya bajeti yote), kama posho.

Kwa hiyo, walipinga madai ya Waziri Mkulo kwamba serikali itapunguza posho na wakataka Watanzania waone ghiliba za serikali.

CCM wakatumia ‘shahada yao ya heshima ya kuzomea’ na hadi Bunge linaisha upotoshaji ukashangiliwa. Lo! Novemba wabunge wakaongezewa posho hadi Sh. 200,000. Halafu wamekata ajira walizoahidi na nusu ya wafanyakazi hawatapandishwa madaraja.

CCM walibisha nini CHADEMA waliposema “bajeti si kamilifu, Hazina haina ‘minoti’ na deni la taifa limeongezeka sana?”

Magazeti yaliandika: “Ni Bajeti ya kuwabebesha mzigo Watanzania”, “Zitto, Mnyika wafichua upotoshaji bajeti ya Mkulo”, Bajeti imelenga watawala au wananchi?”

Angalizo, polisi wapya 1,351 watamwagwa mitaani. Mimi simo!

0658 383 979, Jmwangul@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: