CCM ina siri gani na Wakuu wa Wilaya?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 15 February 2012

Printer-friendly version

YALIKUWA malumbano makali bungeni. Kila upande – chama tawala na kambi rasmi ya upinzani – ulijenga hoja na kung’ang’ania msimamo wake. Mwisho wa mjadala hoja zao ziliwekwa kando, wakaamua kukubaliana yaishe kwa staili iliyoelezwa kuwa sawa na “kufunika kombe mwanaharamu apite”.

Hali hiyo ilijitokeza wiki iliyopita wakati wa mjadala wa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011. Pamoja na mambo mengine, jambo lililoibua malumbano hayo ni kipengele cha kutajwa kwa wakuu wa wilaya katika tume ya katiba, itakayoundwa na Rais kwa mujibu wa sheria hiyo.

Sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge na kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete Novemba mwaka jana, iliwataja wakuu wa wilaya, kuwa wanaweza kutumiwa na tume ya katiba kuandaa mikutano ya kukusanya maoni.

Wadau wa katiba, wakiwamo viongozi wa CHADEMA, walipokwenda ikulu kuonana na Rais Kikwete baada ya sheria kusainiwa, walipendekeza kifungu hicho kiondolewe kwa kuwa kinakwenda kuifanya katiba isimamie maslahi ya kisiasa, kwa kuingiza makada wa chama kinachotawala – yaani wakuu wa wilaya.

Kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977,  tangu chama hicho kilipoanzishwa, wakuu wa wilaya wamekuwa wajumbe wa vikao vyote vikuu vya CCM katika ngazi ya wilaya.

Kwa mfano, ibara ya 76(1)(c) ya Katiba ya CCM toleo la 2010, mkuu wa wilaya ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wa wilaya; ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya wilaya (ibara ya 78(1)(c); na ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM ya wilaya (ibara ya 80(1) (c).

Kuwapo kwa wakuu wa wilaya katika mchakato wa katiba kumewatia hofu wadau wa katiba hiyo, na hasa wabunge ambao hawatokani na CCM. Wanaona kuwa wakuu hao wa wilaya watakwenda kusimamia maslahi ya chama chao kwenye mchakato wa katiba badala ya maslahi ya umma.

Lakini kwa wabunge wa CCM waliochangia hoja hiyo, hawaoni tatizo hilo. Wao wanawakumbatia wakuu hao kwa gharama yoyote ile. Kwa jinsi wanavyozungumzia suala hilo, utadhani bila kuwapo wakuu wa wilaya katika tume katiba haiwezi kukamilika.

Ingawa wabunge wa CCM hutofautiana katika mambo mengi, hasa vita dhidi ya ufisadi, lakini hili la wakuu wa wilaya liliwaunganisha.

Mathalan, michango ya Anna Kilango, mbunge wa Same Mashariki na Christopher Ole Sendeka (Simanjiro) kwa upande mmoja, na Andrew Chenge (Bariadi Magharibi) kwa upande mwingine, inadhihirisha kuwa chama hicho kina maslahi fulani na wakuu wa wilaya kwenye mchakato wa katiba.

Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu anasema kuwa “kuna hofu kubwa sana juu ya nafasi ya wakuu wa wilaya katika mchakato wa katiba mpya kama ilivyowekwa na Sheria hii.”

Anaongeza kuwa “hofu hiyo si ya kubuni, bali ya wazi, kwa kuwa tangu sheria hiyo itungwe mwaka jana, wakuu kadhaa wa wilaya wamenukuliwa na vyombo vya habari wakitishia kuamuru wawakilishi wa mashirika ya kiraia yanayoendesha elimu kwa umma juu ya mchakato wa katiba mpya, wakamatwe kama watafanya programu za elimu hiyo katika maeneo yao.”

Wabunge wa CCM wanatambua msaada wa wakuu wa wilaya katika maeneo yao, kwamba wanalinda maslahi ya chama chao. Wanatambua kuwa kwa nafasi zao za kiserikali na kichama, wana uwezo wa kushuka hadi ngazi ya wajumbe wa nyumba 10 wa CCM na watendaji wa vijiji na kata, kutoa maelekezo na vitisho ili kuhakikisha wananchi wanatoa maoni yanayolinda maslahi ya chama.

Wabunge hao wanaelewa fika, na wameeleza hivyo katika michango yao bungeni, kuwa wakuu wa wilaya kama wawakilishi wa rais wilayani, ndio wakuu wa kamati za ulinzi na usalama, na ndio wanaosimamia polisi katika maeneo yao.

Kwa nafasi hizo, ma-DC wanao uwezo wa kuwaagiza polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, wawabane wapinzani au wanaharakati wengine, wawatwange virungu na kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya chama chao, chama ambacho wanasiasa hao ni makada.

Inaelezwa baada ya rais kushauriwa na wadau, alikubali marekebisho ya sheria hiyo yapelekwe bungeni kabla hata sheria haijaanza kutumika.

Katika makubaliano iliamriwa badala ya wakuu wa wilaya waingizwe wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, kwa kuwa si wanasiasa, ni watumishi wa serikali wenye watendaji wengine chini yao, kama vile watendaji wa kata na vijiji.

Mapendekezo hayo ndiyo yaliyotibua nyongo wabunge wa CCM. Hayo ndiyo yalisababisha waje juu na kuonyesha rangi halisi ya siri yao na wakuu wa wilaya. Wote waliochangia mjadala huo, walipinga kifungu hicho na ‘kusimamia vidole’ kuhakikisha wakuu wa wilaya wanarejeshwa kwenye sheria hiyo.

Kilango ndiye aliwasilisha jedwali la marekebisho kupinga marekebisho ya serikali. Aliungwa mkono na wabunge wenzake wa chama hicho, akiwamo mleta hoja, Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Ushirika uliooneshwa katika kifungu hicho ulidhihirisha kuwa walikuwa na makubaliano ya kichama juu ya suala hilo.

Wabunge wa upinzani wakitambua athari za kuwamo wakuu wa wilaya katika mchakato wa katiba, walipinga kifungu hicho hadi Spika Anne Makinda akakiondoa bungeni kukirejesha kwenye Kamati ya Bunge ya Sheria na Utawala.

Makinda ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM, alichukua uamuzi huo kwa lengo la kutafuta maelewano baina ya pande mbili, ili suala hilo lisifikie hatua ya kupigiwa kura na kuonekana kubwa mbele ya Watanzania.

Pamoja na hoja zote zilizotolewa na pande zote,  kiliporejeshwa bungeni siku iliyofuata, kwa wingi wa wabunge wa CCM, kama ilivyo kawaida, walishika mpini na wapinzani wakakamata makali – wapinzani walizidiwa nguvu na kulazimika kulainika.

Kiongozi wa upinzani bungeni, Freeman Mbowe, kwa shingo upande aliafikiana na walio wengi, kwa kile alichoita “funika kombe mwanaharamu apite” ili kumaliza mabishano. Hata hivyo, alitumia nafasi hiyo kuonya kuwa utamaduni huo utalifikisha taifa mahali pabaya.

Mjadala huu mkali uliotokea bungeni unathibitisha wazi kwamba wakuu wa wilaya si muhimu kwa shughuli za serikali tu bali uhai wa CCM – kusimamia mikutano ya siasa ya CCM pia kutisha na kuwanyima fursa wapinzani.

0
Your rating: None Average: 2 (1 vote)