CCM inakimbilia siasa za maangamizi

MWAKILISHI wa chama kilicholeta uhuru Kenya, Kenya African National Union—KANU, akitoa salamu za chama chake kwenye mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dodoma mwaka 2005, aliwaasa CCM jambo moja zito.
Alisema: “Ndugu zangu msithubutu kupoteza madaraka.”
Alisema hayo akielezea masahibu yaliyokuwa yamekipata chama hicho kilichotawala Kenya tangu uhuru mwaka 1963 hadi mwaka 2002 kilipopoteza madaraka kwa NARK yaani umoja wa vyama vya wapinzani.
Ni katika uchaguzi huo, Rais Mwai Kibaki aliingia madarakani chini ya mwavuli wa Nark. Hata hivyo, mwaka 2007, umoja huo ulikuwa umekwisha sambaratika na kuwako vyama vingine vilivyoingia kwenye uchaguzi mkuu; Kibaki akiongoza chama cha PNU na hasimu wake mkuu, Raila Odinga akiongoza Orange Democratic Movement (ODM).
Ni uchaguzi wa mwaka 2007 ndio umebadili kabisa siasa za Kenya kufuatia vurugu zilizotokea mwaka huo kutokana na matokeo ya uchaguzi huo kuchezewa.
KANU iliwasilisha kwa CCM tahadhari hiyo kwa sababu walikwisha kuonja machungu ya kuwa chama cha upinzani. KANU ilipoteza madaraka, si kwa sababu ya kitu kingine chochote, ila kubweteka.
Kuzoea kutawala, kuzoea kuwa chama tawala, na kuamini kwamba kutawala ni haki yao ama ya kuzaliwa au kutoka kwa Muumba.
Ndiyo maana KANU, kwa kuamini kwamba wana hati miliki ya kuongoza Kenya, haikujali hisia wala haki za wengi katika kufikia maamuzi. Ilikuwa kazi ya mwenyekiti wa KANU, wakati huo, Rais Mstaafu Daniel Arap Moi, kuamua nani awe nani au asiwe nani.
Ni kwa maana hiyo, aliamua kumpendekeza Uhuru Kenyatta, mtoto wa Rais wa Kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta, kuwa mgombea urais wa KANU mwaka 2002 na kuishia kubwagwa vibaya.
Leo hii, miaka mitano baada ya ushauri wa KANU kwa CCM, kila nikitafakari na kutazama nyuma najiuliza kama walijua maana ya ushauri waliopewa na chama hicho rafiki.
Kwa jinsi nilivyomwelewa yule mwakilishi wa KANU, hakusema CCM ing’ang’anie madaraka, hakusema ifanye vitimbi na vibweka katika kubakia madarakani, bila shaka alikuwa akiwaambia “chonde chonde msifuate njia yetu; yaani acheni ubabe kama mnaofanya, acheni mizengwe kama ipo, acheni kuonea baadhi ya wanachama kama mnawaonea, na mwisho acheni kukifanya chama kuwa mali ya viongozi.”
Mchakato wa kura ya maoni uliomalizaka wiki hii ndani ya CCM umeacha somo moja kubwa. Kwamba bado CCM ni chama mali ya viongozi wachache; kwamba kikundi kidogo cha watu wanaweza kuamua watakalo na wengine walie tu, waende wapi wakati chama ndicho kinatawala?
Hisia hizi ndizo zilijionyesha wazi Jumapili wiki iliyopita wakati baadhi wa wanachama waliponyimwa fursa yao ya kutumia haki yao ya kidemokrasia kuamua nani awe mgombea wao.
Kuna matukio ya aibu na ajabu; wanachama kufutwa majina yao kwenye rejista ya wanachama tawini, wanachama kuwekewa mizengwe kwamba hawajulikani kwenye matawi yao, lakini baya zaidi viongozi wa matawi kuwa na majibu ya kiburi na jeuri kwa wanachama.
Kwa kiwango kikubwa, maeneo mengi, ukiacha mbinu chafu za matumizi ya fedha kununuana, viongozi wa ngazi za chini; matawi, kata; wilaya na mkoa; walionyesha kutokujali kwa kiwango cha juu.
Ni kama imekubalika kwamba viongozi wa CCM wana uwezo wa kucheza na haki za wanachama na bado wanachama hao wabakie kuwa na imani na chama hicho. Kwa maneno mengine, wanachama hao wanachukuliwa kama mali ya chama, hawawezi kuondoka au kukiadhibu chama chao! Ni mali binafsi.
Jeuri au kiburi hicho ndicho alikijenga Moi miaka na miaka akiamini kwamba KANU itaendelea kubakia imara hata kama mfumo mzima wa kulinda, kuheshimu na kusikiliza wanachama kwa uadilifu ulikuwa ama haupo kabisa au ni dhaifu mno.
Kila nikitafakari matukio kama ya wanachama wachache waliothubutu kujitokeza wazi Dar es Salaam na Tanga (karibu 1,000) kutangaza kujiengua CCM, ninaona kama moja ya vielelezo vya kubweteka kwa chama.
Ni dalili ya kushindwa kwa chama kutambua kwamba kipo kwa kuwa kina wanachama na kila mwanachama ni muhimu kwa chama husika na anastahili kuheshimiwa.
Ukiachilia mbali suala la ghilba na hila za wazi katika mchakato wa uchaguzi huo, pia CCM imeanza kujifunua katika sura mpya iliyojificha ndani yake.
Kwamba inawezekana vipi wanachama wa chama kimoja, wenye nia moja kujiingiza katika uhasama mkali kama ambao umeshuhudiwa?
Jaribu kufikiria tukio la Mwanza ambalo watu wanathubutu kuchukua mapanga na marungu kuwacharanga wenzao; kisa kura za maoni ndani ya chama kimoja!
Ukitafakari kwa kina zaidi matukio kama haya, utagundua kwamba chama hiki si mkusanyiko wa watu wenye mawazo yanayofanana, walionuia kuyaunganisha kwa malengo makuu ya kukamata madaraka ya dola tu, ila ni makundi ya magenge yasiyo na makubaliano ya pamoja, kila genge likijitahidi kutimiza mradi wake.
Chama chenye magenge ya namna hii ikitokea kwa bahati mbaya au nzuri kimepoteza madaraka ya dola, hata kwa mwezi mmoja tu, hakitakuwa kama KANU ya sasa, ila kitafutika katika uwanja wa siasa.
Kitafutika kwa sababu kinachowaunganisha ni maslahi ya kimagenge, hili likipambana na lile, na kila mmoja akitafuta kummaliza mwenzake.
Kwa mwendo huu, hata ile mitandao na makundi yaliyoundwa ndani ya chama hiki, sasa inaanza kujitokeza katika picha pana zaidi kwamba si bure ni mwendelezo wa siasa za kimagenge.
Inawezekana CCM haioni kwamba inakimbilia kwenye maangamizi, mchakato wa kura za maoni, kuanzia harakati za kuhongana fedha, kuhujumiana kwenye orodha ya majina ya wanachama katika ofisi za matawi na hata vitendo vya vurugu na aina zote za uhuni, ni vitendo vinavyoonyesha kwamba chama hiki kinazidi kujiondoa kwenye fungamano la itikadi kuwa magenge na maslahi ya mtu mmoja mmoja.
Hadi leo, ujumbe wa mwakilishi wa KANU haujafanyiwa kazi na CCM. Kura za maoni za mwaka huu zinaacha maswali mengi zaidi juu ya mustakabali wa chama hiki.