CCM ipi imeshinda Igunga?


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 12 October 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

WENGI wameandika juu ya uchaguzi mdogo wa Igunga. wengine wamediriki kusema, “suala la Igunga limekwisha, tusubiri jingine.” Hata hivyo, kwa kuwa nilishiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi huo, nikiwa mwanachama wa CCM, mwandishi na mtafiti, naona ni vema nami nitoe maoni yangu kuhusu uchaguzi ule.

Kwanza, ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wapo wanaodai Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiliiba kura na kupunguza ushindi wao. Lakini pili, wapo wengine wakiongozwa na Nape Nnauye wanaokiri wazi kuwa CCM iliponea chupuchupu Igunga. Kinachogomba katika makundi yote mawili ni juu ya ni CCM ipi wanayoizungumzia hasa?

Waandishi wengi na wachambuzi mbalimbali wamedai CCM haikushinda. Hii haina maana kuwa CCM hawakuwa na kura nyingi kuliko washindani wao, bali wanaamanisha kuwa ukilinganisha na kura walizopata katika uchaguzi mkuu uliopita, ni sahihi kusema kuwa CCM haikushinda bali CHADEMA ndiyo washindi.

Mchambuzi mmoja kati ya wengi walionivutia ni yule aliyeandika nadhani kwa usahihi zaidi pale aliposema, “Ushindi CHADEMA, Ubunge CCM.” Hata baadhi ya wana CCM wanaopenda ukweli wanaukubali mtizamo huu hata kama kwa sababu zilizo wazi hawawezi kukubali hadharani juu ya hali hiyo isiyowapendeza wakubwa wao.

Kwangu mimi naenda mbali zaidi. Iwe CCM ilishinda kwa kura au kushindwa kwa mtizamo halisi wa kisiasa, nazidi kuhoji ni CCM ipi iliyoshinda au hata kuhoji ni CCM ipi iliyoshindwa kisiasa huko Igunga?

Maswali yangu siyo tata kwa sababu CCM tunayoijua si moja tena na hata huko Igunga zilikuwepo CCM nyingi. Kutokana na siasa za makundi zilizosababisha Rostam Aziz kuachia ngazi, CCM si chama kimoja tena. Kilichobaki kimoja, ni jina la chama tu. Hili ndilo linalowakusanya watu wenye maslahi tofauti na kiitikadi tofauti.

Kimsingi, CCM ni mkusanyiko wa makundi mbalimbali na kati ya haya hakuna kundi linaloweza kusimama leo na kudai ndilo lililoshinda au kushindwa Igunga.

Mathalani kimsingi Rostam alijiuzuru kwa kuwa aliitwa fisadi na wapinzani kisha wana CCM wenzake wakadandia agenda hiyo. Pande la kwanza la CCM likiongozwa na “mitume 12” wakazunguka nchi nzima wakimtangaza yeye na wenzake wengine ni mafisadi. Ufisadi uliokuwa unapigwa na wanaotuhumu Rostam, ndiyo huohuo uliokiingiza chama hicho madarakani na hata kumpa Nape Nnauye ukuu wa wilaya na sasa katibu mwenezi wa chama.

Kujiuzuru kwa fisadi Rostam, kukasababisha Benjamin Mkapa, mtuhumiwa mwingine wa ufisadi lakini ambaye Nape na wenzake wanaweza tu kumwita fisadi kwenye vijiwe na kwenye baa lakini si kwenye majukwaa, akaenda Igunga kufungua na kufunga kampeni za chama chake.

Kutokana na ushindi uliopatikana huko, hivi sasa kuna taarifa kwamba Nape na kundi lake wameanzisha kampeni maalum za kuwashawishi wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, kwamba ni bora Mkapa aombwe kuwa mwenyekiti wa chama pale wanaowaita mafisadi watakapokuja na hoja ya kutenganisha kofia ya urais na uenyekiti wa chama.

Hatuna uhakika kama jitihada hizi zina baraka za Mkapa mwenyewe au la, lakini kwa kuwa Mkapa si maskini wa siasa za makundi, ni mapema kupuuza harakati hizi za Nape na “mitume wake.”

Kampeni za Igunga zilimleta pia Philip Mangula. Sura yake ilijaa aibu wakati anaanza kampeni, lakini kadri siku zilivyosonga mbele alipata ujasiri wa kifisadi na hata kufikia kumsifia Rostam ili awavutie wapiga kura wa Igunga. Mangula anajua kwamba ni Rostam ayehinikiza Kikwete kuondokana naye mara baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 kwa kumwona ni kikwazo ndani ya chama.

Ni Rostam Aziz aliyeongoza harakati za kummaliza Mangula kule Iringa pale alipogombea uenyekiti wa mkoa wa chama chake. Baadaye Mangula aliomboleza na kusema, “CCM ya sasa inataka vipeperushwa na si “vipeperushi vya wagombea.”

Akadai hivi “sasa uongozi ndani ya CCM uko mnadani na mwenye fedha ndiye anayeupata.” Tangu hapo alijichimbia kijijini bila kujitambulisha na CCM mpaka juzi alipokurupushwa na tuhuma za CHADEMA kuwa anahusika katika wizi wa EPA.

Mmoja wa marafiki zake ameniambia kuwa kujihusisha ghafla na kampeni za Igunga kunatokana na hasira dhidi ya CHADEMA kwa kumwita fisadi. Kwa hiyo, Mangula alikwenda Igunga si kuinadi CCM, bali kupambana na CHADEMA maana CCM ya sasa bado ile ile aliyosema iko mnadani na “vipeperushwa.”

Baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza Dk. Peter Kafumu kuwa mbunge mpya wa Igunga, baadhi ya makada na viongozi wa CCM, Nape akiwamo wamedai wanaenda NEC kuwashitaki baadhi ya wanachama na makada wanaodai walikihujumu chama chao huko Igunga.

Hili peke yake linadhihirisha ukweli kuwa huko Igunga kulikuwa na CCM nyingi kuliko inavyoelezwa kwenye hotuba za majukwaani. Kitendo cha baadhi ya makada na viongozi kuzuiwa wasiende Igunga na wakatii, ni ishara tosha kuwa ushindi wa Igunga si wa CCM nzima, bali ni ushindi wa CCM iliyoenda Igunga na si ile ambayo haikwenda. Hata kama hili halitajwi hadharani kuwa lipo, ni vigumu sana kwa sasa kusimama hadharani na kudai CCM ni moja tena.

Lingekuwa jambo la afya kama CCM ingekiri hadharani kuwa imegawanyika ili upatikane ujasiri wa kutosha kujipanga tena. Hatua hii ingeondoa kabisa makundi ya chini chini na badala yake makundi yangekuwa wazi na kushughulikiana kwa hoja ili wanachama halisi wa CCM isiyogawanyika waamue mustakabali wa chama chao na wale wasiokubaliana wakatafute chama kingine.

Uamuzi wa kuficha hili na kutaka kutumia vikao ili kufukuzana au kutegeana, hauwezi kukiponya chama hiki hata kidogo. Ugumu wa kufukuzana unatokana na ukweli kuwa ni vigumu kumpata mtu hata mmoja ndani ya CCM asiye na uhusika katika madhambi yanayolalamikiwa ndani na nje ya chama hicho.

Hata ukichukua hoja ya ufisadi, ni vigumu kabisa kumpata mtakatifu ndani yake baada ya Nyerere kuondoka. Wote kwa kujua au kutojua wamejikuta ni madalali na makuwadi wa ufisadi ndani ya chama na serikali. Ikiwa ufisadi umemmaliza mtu kama Kingunge Ngombale Mwiru, nani anaweza kusimama na kuukana ufisadi ndani ya CCM?

Ndiyo maana baadhi yetu tunashindwa kujua ni CCM ipi inayodai imeshinda Igunga? Je, ni ile inayoongozwa na mitume 12 chini ya Nape anayedai kuendesha kampeni, lakini mwenyewe akiwa amezuiwa kwenda Igunga, ama ni ile ya watuhumiwa wa ufisadi?

Je, nani mshindi Igunga kati ya wale waliofanikiwa kupiga marufuku makada wa CCM kuzungumzia kabisa tatizo la ufisadi ndani ya nchi na ndani ya CCM, ama ni CCM ya akina Samwel Sitta, Dk. Harrison Mwakyembe, Anne Kilango Malecela na Christopher ole Sendeka ambao iliwalazimu kununua magazeti ili kujua kinachoendelea Igunga?

Yupi mshindi kati ya mafisadi walioangukiwa na kuombwa fedha za kusaidia kampeni na kukodisha helikopta, ama wale wanaotamba tumeshinda Igunga na uchaguzi umekwisha, au wale wanaongoza serikali kwa sasa?

tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet