CCM itamke ufisadi sera yake


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 25 August 2009

Printer-friendly versionSend to friend
Tafakuri

UNAHITAJI kichwa kilichotulia kuchambua kwa mapana yaliyojiri kwenye vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) vya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hii ni kutokana na kutosadiki kwamba watu wazima wanaweza kujipanga kushambulia muhimili wa dola wakielekeza mashambulizi yao kwa mtu mmoja tu, Spika wa Bunge, Samwel Sitta.

Inakuwaje Spika peke yake tu awe kichwa ngumu kuzidi kila mtu kwenye Bunge hadi NEC ifikiri ndiyo yenye uwezo wa kukabiliana naye?

Nitajitahidi kufafanua. Kwanza Bunge ni taasisi; lina taratibu na kanuni za kuendesha mambo. Kuna Spika mwenyewe, kuna Katibu wa Bunge, lakini kuna wakurugenzi wengi tu.

Mbali na hayo kuna kamati ya uongozi ya Bunge ambayo hupanga nini kifanyike bungeni na kwa wakati gani. Wapo makamishna wa Bunge.

Kamati ya uongozi ni kiungo muhimu. Katika vikao vyake vyote wenyeviti wote wa kamati za kudumu za bunge ni wajumbe, pia mnadhimu mkuu wa serikali naye huhudhuria vikao hivi; bila kusahau Waziri Mkuu ambaye ni kiongozi wa shughuli za serikali bungeni.

Ukiacha kikao hicho ambacho kwa hakika ndicho chenye wajibu wa kuamua nini kipelekwe bungeni kujadiliwa na kwa wakati upi, serikali bungeni imejaa, tena imejaa tele.

Kuna safu nzima ya baraza la mawaziri wakiwamo mawaziri na manaibu wao. Yupo mwanasheria mkuu wa serikali, lakini kuna kiranja wao mkuu, Waziri Mkuu.

Bunge hilihili tunalolifahamu sisi, wabunge wa CCM ni zaidi ya asilimia 80. Sasa mtu anajiuliza katika utitiri wote huu, hivi kweli Spika amejitwalia madaraka kiasi cha kuumiza serikali na chama chake?

Kama Sitta ameweza kufanya hivyo, binafsi namsifu kwa sababu ni mtaalam wa thabiti katika kupoka madaraka na kujiendeshea mambo atakavyo.

Baada ya kuona ukweli kuhusu Bunge lilivyo, hebu sasa tutazame madhambi aliyotwishwa Sitta kiasi cha kuamsha hasira ya wananchi kwamba sasa NEC ya CCM inataka kuliasi Bunge; ili liwe butu, lenye woga na hivyo kusaidia kulinda mawaa ambayo hata asiyeona anaweza kuyapapasa na kuyatambua.

Eti Sitta anahukumiwa kwa kuumiza kundi moja bungeni. Hili si jingine bali ni lile lenye tuhuma za ufisadi. Kwamba amekuwa akipanga watu wake kuwashughulikia watu hao, hivyo kuipa shida serikali na chama chake, CCM.

Kwa mwenendo huo, Sitta anadaiwa kwamba hakisaidii chama chake, amekuwa mpinzani na kwa hivyo watu wenye ‘uchungu’ na serikali na CCM walitaka anyang’anywe hata kadi aliyonunua kwa fedha zake mwenyewe.

Hawa ni pamoja na wale ambao waliwahi kukimbia CCM na kujiunga na vyama vya upinzani kabla ya kuharibikiwa zaidi na kurejea chamani baada ya kuitukana sana CCM, tena hadharani, kwa matusi ya nguoni.

Hawa wanamuona Sitta kama ni mpinzani zaidi ndani ya CCM; ni ‘kikulacho ki nguoni mwako,’ kwa hiyo anastahili kukomeshwa kwa kumfukuza uanachama.

Sasa ukitafakari sana kwa mapana utagundua kitu kimoja tu katika mpango huu mzima wa kumkandamiza Sitta ambao umesukwa na kundi lililoapa kwamba cheo si dhamana, bali ni nafasi ya kujinufaisha wao na wale wa nyumbani kwao.

Hawa walikula njama, wakatumia fedha kupanga watu wao, wakapenyeza hoja yao ndani ya vikao vya chama kuanzia Kamati Kuu hadi NEC ili kumlazimisha Sitta akubali kwamba ufisadi ni sehemu ya maisha ya CCM. Kama hataki ang’oke.

Tuanze kuwatazama hawa wanaomwandama Sitta. Bila kutafuna maneno yupo majeruhi namba moja wa makali ya Bunge. Huyu ni Edward Lowassa.

Yupo mtuhumiwa wa ufisadi wa rada, Andrew Chenge. Kuna Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, ambaye anatajwa kwenye kila korongo la tuhuma ya ufisadi, kuwa ama anahusika au amelinda wahusika.

Yupo Rostam Aziz anayetajwa kwenye sakata za Richmond na EPA; yupo rais mstaafu Benjamin Mkapa, “mzee msafi” aliyejichafua mwenyewe.

Wapo akina Nazir Karamagi kwenye sakata la Richmond na Ticts; lakini yupo mzee Kingunge Ngombale-Mwiru, ambaye amepoteza mwelekeo – kutoka mjamaa aliyekubuhu hadi bepari asiye na mwelekeo thabiti.

Hawa ni baadhi tu ya watu wenye tuhuma nzito na kubwa. Hata siku moja si CC wala NEC iliyopata kutamka kwamba mwenendo wa mmoja wao unachafua chama, unaleta ukakasi kwa wananchi na hivyo angalau wakaripiwe ili wajirekebishe.

Hapana, hawaguswi na wala hawaonekani kuwa ni tatizo kwa chama, bali wale wanaotaka watuhumiwa wajisafishe ndio wanasakamwa na kuundiwa njama. Ndiyo, njama!

Hapo ndipo vikao vya juu vya Chama Cha Mapinduzi – CC na NEC vilipojifikisha. Kwamba kulaumu ufisadi au kupambana na ufisadi ndani ya CCM ni lazima kufanywe kwa kiini macho.

Kwamba kupambana na ufisadi sasa sharti uwe mchezo wa kuigiza; ukifanya kweli unakiuka maadili, unaumiza wengine unakiharibia chama, unachafua wengine na kuikosesha raha serikali.

Kwa NEC kubariki kusakamwa kwa Sitta kwa kiwango kile, ni sawa kabisa na kutangaza wazi kwamba ufisadi uliokuwa sera ya uficho ya CCM sasa ni rasmi kwa sababu yeyote anayepiga vita ufisadi sasa anakikosea chama na anainyima amani serikali!

Hasira za juzi juu Sitta ni matokeo ya kukwama kwa taarifa ya serikali juu ya Richmond na Kiwira katika mkutano wa Bunge wa 16. Ni hasira za mafisadi kuona kwamba njia zao za kujitakasa kupitia bungeni zimekwama na sasa wanamwashia ishara ya hatari Sitta; ama awe upande wao au ang’oke.

Hasira za NEC ni kielelezo cha nguvu za kifisadi zilizoteka CCM kiasi cha kulazimisha kikao muhimu kama NEC kumjadili mtu mmoja hadi kujikuta ikiingilia uhuru wa Bunge na madaraka yake.

Lakini wakati hali hii ikiendelea hadi ngazi ya kuunda kamati ya watu watatu, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Abdulrahaman Kinana na Pius Msekwa, kuchunguza kulikoni bungeni na kwenye Baraza la Wawakilishi, umma unashindwa kujua hivi ni wapi NEC inapata madaraka ya kuchunguza Bunge.

Hivi Bunge ni sehemu ya CCM? Hivi kuchunguza mwenendo wa wabunge au wajumbe wa baraza la wawakilishi ndani ya vikao rasmi vya Bunge au Baraza la Wawakilishi inakuwaje kazi ya NEC? Nini kimepata taifa hili kiasi cha kupotoka hivi?

Kweli ufisadi una nguvu. Watuhumiwa wa ufisadi wamepambana hadi wameteka nyara NEC na sasa wanaitumia kulazimisha watu wawasafishe; watu wanyamaze na Bunge liwaogope.

Nina shaka kama viongozi wa CCM wanafahamu madhara ya walichofanya juzi. Hata kama ulikuwa ni mkutano wao wa ndani, ukweli umetoka nje na sasa umma unajua kwamba CCM na mafisadi ni chanda na pete, katu hawatengani.

Hii ndiyo maana hadi sasa huwezi kuona kishindo chochote cha kushughulikia mafisadi. Wengi ni wajumbe wa vikao vya Kamati Kuu na NEC na ndio wanaoamua taifa hili liende wapi.

Kwenye hali kama hii, mtu anajiuliza CCM ina uhalali gani basi ya kuendelea kubaki madarakani? Kama inapambana na ufisadi, kwa nini Sitta atoswe kwa sababu tu ametenda haki ya kutozuia wabunge kuzungumza kwa uhuru katika mambo yenye maslahi kwa taifa hili?

Baada ya vikao viwili vya wiki iliyopita vya Kamati Kuu na NEC vya CCM ni bora sasa chama hiki kikatangaza wazi kwamba ufisadi ni moja ya sera zake na kwa maana hiyo, wananchi wasitarajie vita dhidi ya ufisadi kuleta tija yoyote.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: