CCM itashinda au kushindwa mtihani Zanzibar

HALMASHAURI Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inapokutana kuteua mgombea urais wa Zanzibar kwa ajili ya uchaguzi mkuu, itambue ina mtihani mkubwa.
Inayo majina matatu ya makada wake waliotokana na 11 waliochukua fomu ya kuomba idhini ya chama ili kugombea nafasi hiyo ya juu kabisa katika nchi.
Wakati naandika makala hii, majina hayo yalikuwa bado hayajajulikana kwa kuwa Kamati Kuu (CC) ndiyo ikisubiriwa na jukumu hilo.
CC ilitarajiwa kuchambua majina 11 yaliyowasilishwa na Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui.
Hadi Jumatatu, kinachojulikana ni taarifa kwamba Kamati Maalum ya NEC Zanzibar imetaja makada watano watakaopimwa ingawa pia zipo taarifa nyingine za ndani zilizoeleza kuwa makada wote 11 watapelekwa Kamati Kuu.
Makada watano waliopewa alama za juu baada ya majadiliano marefu na magumu ya Kamati Maalum yaliyofanyika tarehe 3 Julai, ni Shamsi Vuai Nahodha, Dk. Ali Mohamed Shein, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Haroun Ali Suleiman na Ali Juma Shamhuna.
Makada wengine walioingia kiringeni nao, ni Balozi Ali Abeid Karume, Bakari Hamad Mshindo, Omar Sheha Mussa, Mohamed Aboud Mohamed, Mohamed Hassanali Raza na Mohamed Yussuf Mshamba.
Sasa wakati vikao vya CCM vikisubiriwa kutoa uamuzi, watu wakiwemo makada wake, wanaulizana hivi chama hiki kinataka mgombea gani kwa ajili ya Zanzibar?
Ndio kusema mgombea mtarajiwa anategemewa sana kuwezesha wananchi kubashiri hali itakuaje utakapokuja uchaguzi mkuu.
Wachambuzi wa siasa za Zanzibar wanaamini hatima ya maridhiano yaliyoanzishwa na Rais Amani Abeid Karume na Maalim Seif Shariff Hamad inategemea sana mgombea wa CCM.
Ni siasa zenye mantiki. Watu wanatazama hali iliyopo na kuipa picha ya itakavyokuwa baada ya uchaguzi utakaotegemea mgombea huyo wa CCM.
Zanzibar inahitaji kujengwa upya. Wazanzibari wanahitaji Zanzibar mpya. Zanzibar iliyoondokana na siasa chafu zilizoleta gharika na kuleta siasa za maridhiano, zinazoashiria mustakbali mwema kijumla.
Nchi imekuwa katika matatizo makubwa yaliyoirudisha nyuma Kwa sehemu kubwa matatizo hayo yamechangiwa na ukosefu wa uongozi bora. Anahitajika kiongozi bora si bora kiongozi.
Uongozi bora ni uongozi unaojali watu; kuwaheshimu; na kutambua na kuamini katika haki zao na mwisho kuzitekeleza kwa usawa.
CCM isilete mgombea kwa kuhisi “huyu anafaa au anawafaa Wazanzibari.” Anatakiwa mgombea mwenye uwezo na aliye mtulivu kiuongozi. Anatakiwa mgombea ambaye akisimama tu, watu wanamheshimu na kujiandaa kumsikiliza.
Huyu ni mtu anayejiheshimu na kuheshimika. Mtu anayeweza kuwa daraja makini la kuvusha watu kwenda katika maisha mema. Haya ni maisha yenye maendeleo ya kweli.
Maendeleo ya kweli hupatikana kwa kuwepo kiongozi wa juu mwenye uwezo wa kufikiri vizuri. Akishafikiri anasikiliza wenzake na anasikiliza sauti ya wananchi anaowaongoza wanataka nini kuhusu jambo analolifikiri.
Watu hawataki kiongozi mwamuzi kwa njia yake tu. Huyu ni dikteta ambaye ataishia kuwaswaga watu baada ya kuwa ameikanyaga katiba na kuzihalifu sheria za nchi.
Lazima CCM ilete mgombea mpenda sheria na kanuni; na mheshimu katiba ya nchi ambayo ndiyo muongozo wa kuongoza watu.
Zanzibar ilipo inataka kufuta historia mbaya ya migogoro inayotokana na uchaguzi na uongozi mbaya unaochangiwa na mawazo mgando.
Je anayeteuliwa na CCM anayo rekodi ya kuwa mchangiaji mzuri wa umoja na mshikamano kwa wananchi?
CCM itambue itajimaliza iwapo itateua mgombea asiyekubalika. Sauti ya watu ni muhimu katika maamuzi yoyote yanayofanywa na uongozi.
Mwalimu Julius Nyerere (1922-1999) alipata kusema mwaka 1995 kwamba chama chochote kisichoheshimu maoni ya wananchi, kitaanguka kama si leo kesho.
Zanzibar inahitaji mgombea ambaye akitajwa tu wananchi wengi wanasema NDIO. Huko ndiko kukubalika kwake. Akigunwa basi hiyo ni ishara ya kutokubalika.
Uzuri CCM yenyewe ina sifa zake 13 kwa kada wake anayestahili kupewa uongozi wa juu kama urais, ya kukubalika ni mojawapo. Kuna sifa ya mtu kuwa anaheshimu misingi ya utawala bora na haki za binadamu na mwenye kuchukia vitendo vya rushwa. Swadakta.
Zanzibar inanuka rushwa na ufisadi. Wapo watumishi wakubwa kwa wadogo wanadai mlungula kabla ya kushughulikia matatizo ya watu.
Wapo watumishi wanaotumia nafasi walizopewa kujinufaisha binafsi. Tatizo hili lipo kwenye hospitali, mahakama, wizara, idara na mashirika ya serikali.
Rushwa na ufisadi vimetamalaki bandarini, kwenye viwanja vya ndege, polisi, uhamiaji na mahotelini. Ni ugonjwa ulioenea kwingi tu. Athari zake ni kubwa zilizouweka utumishi wa umma kama ni upuuzi mtupu.
Zanzibar inataka kiongozi mwenye utashi wa kutokomeza rushwa na ufisadi. Awe ni kiongozi mwenye historia ya kuchukia hasa maovu haya. CCM ilete mtu wa namna hiyo na siyo mwenye mapenzi nayo.
Maendeleo ya Zanzibar hayawezi kupatikana ndani ya jamii iliyotengana. Rais Karume amekuja na mpango wa kuitoa nchi hapo. Anataka jamii yenye mapenzi na umoja.
Je CCM italeta mgombea mwenye historia ya kushajiisha watu kupendana? Kama hana historia hiyo atakataliwa na wana CCM wenyewe.
Katika kumteua mgombea wake, CCM haitarajiwi kutabiri. Isipige ramli au kubahatisha. Wanachama wenyewe hawatarajii kiongozi wa vikao kutaja mtu anayempenda.
Wajumbe wanamjua mgombea bora. Basi waachiwe watumie haki kumchagua. Kile kilichofanywa na Benjamin Mkapa mwaka 2005 alipokuwa akiongoza mkutano mkuu maalum wa uteuzi wa mgombea urais wa Tanzania – kuelekeza wajumbe nani achaguliwe – hakifai.
Maelekezo yake yalichukuliwa ni amri ya kiongozi mkuu wa dola na chama tawala. Hatimaye wajumbe walipiga kura zao kwa kuzingatia maelekezo hayo. Walimtii.
Mpaka leo, wana CCM wenyewe wanasema wazi kuwa Mkapa alimtaja kinamna Jakaya Mrisho Kikwete kuwa ndiye wa kuchaguliwa.
Wakubwa wa CCM watambue kwamba kwa mgombea watakayemteua, ana kazi ya kushindania kura na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif ambaye ameshapitishwa na chama chake.
Huyu ndiye aliyekaa na Rais Karume kuafikiana kufuta siasa za chuki kwao kama viongozi waliogombania urais mara mbili, na kwao kama wakuu wa vyama vilivyoshindana.
Maridhiano yao yameleta taswira mpya ya mshikamano madhubuti miongoni mwa jamii. Wamesawazisha njia iliyokuwa imejaa matope. Wananchi Unguja na Pemba wameridhia itumike kuwapeleka safari ya mafanikio ya kweli kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.