CCM kama ilivyo sasa haiwezi kuokoleka

KUNA watu ambao kwa makosa ya fikra zao na kiburi cha utamu wa madaraka, hasa wale waliopigwa ganzi ya "utukufu wa kisiasa," wanaamini kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitadumu madarakani milele.
Hawa, wamejiaminisha katika upotovu wao kuwa CCM kitadumu milele na kitaendelea kuwa kama kilivyo sasa. Hawa ni wa kuwekewa mikono na ikibidi kupepewa huku wanavutwa masikio.
CCM ni mazao ya binadamu, ni chombo kilichoundwa na wanadamu; kimeongozwa na kinaongozwa na binadamu na kutokana na hilo tu peke yake, CCM kinakuwa ni chombo kinachoweza kuharibika, kuvunjika, kuporomoka na kwa hakika kabisa chaweza kuzama.
Hakuna ustadi wa mwanadamu unaoweza kufanya kazi zake zisiwe na makosa milele. Katika uelewa wetu huu mdogo wa kibinadamu ni kazi za Mungu tu ambazo hazina makosa.
Hivyo ninaposikia mtu anasema kwamba CCM itatawala milele, na kumtumbulia macho kama mjusi aliyekoswakoswa na mlango. Na pale ninaposikia kuna wana poropaganda wa CCM ambao "wanaitetea CCM kuwa ni chama safi na kina mafisadi wanne tu," ninafumba macho yangu kwa mshtuko.
Kama ningekuwa karibu na mtu huyo, ningemtingisha ili atoke katika usingizi wake uliochanganyika na ulevi wa madaraka.
Malumbano tunayoyasikia sasa na kugongana kunakoendelea hivi sasa ndani ya chama hiki na tutashuhudia zaidi miezi michache ijayo, yanatoa ushahidi wa jambo moja kubwa kuwa CCM kiko matatani na hakuna mtu wa kuiokoa.
Wale wanaogongana ndani ya CCM leo hii, hawagongani kwa sababu ya tofauti za kiitikadi (karibu wote hawana); wanagongana zaidi kuhusu maslahi yao ndani ya chama. Makundi yote yaliyopo ndani ya CCM leo yanatuhakikishia kuwa hayawezi kudumu ndani ya chama hichohicho yakiendelea kuongeza upana, ukali na uzito wa tofauti zao.
Mstari ulichorwa kwenye ripoti ya Richmond, wanahistoria watakapokaa chini kuandika juu ya kuvunjika/kumeguka kwa CCM, bila shaka watalielezea hilo kwa kuangalia mwitikio wa wanasiasa mbalimbali wa chama hicho baada ya ripoti hiyo kutolewa bungeni na kusababisha serikali kujiuzulu. Tukio lile limebakia na linaendelea kubakia kama mstari unaozitenganisha kambi hizi mbili.
Wale wabunge waliosimama bungeni kuunga mkono ripoti ile na kutaka wahusika wote wawajibishwe au wajiwajibishe, akiwemo Edward Lowassa aliyekuwa waziri mkuu, ndio hao leo hii wanaoonekana wakiongoza vita dhidi ya ufisadi.
Kundi hili bila ya shaka lina watu kama Dk. Harrison Mwakyembe, Lucas Selelii, Anne Kilango, Said Mkumba, Aloyce Kimaro na wengine. Ni hao ambao utawaona wamekuwa wakisimama kidete dhidi ya uozo mwingine kama Dowans, Kiwira na EPA.
Kundi lile la wabunge waliosema Lowassa hakutendewa haki, leo hii wanaonekana ni watetezi wa ufisadi kwani wamegoma kabisa kujiunga katika kulaani na kupiga vita ufisadi ule ambao umelimeza taifa.
Hawa hawajasimama kusema lolote kuhusu Kagoda, Kiwira, wala Dowans na wanaonekana ni kama wanajaribu kufafanua mambo haya lakini hawataki kuonekana wako upande wa kundi hilo la kwanza. Wako wapi akina Rostam Aziz, Peter Serukamba, Kingunge Ngombale Mwiru na Yusuph Makamba juu ya masuala haya?
Kutokana na makundi hayo mawili ndani ya wabunge wa CCM, nazo kambi mbili kubwa zimeibuka katika wanachama wa CCM, zikifuata kabisa mwelekeo wa nani alichagua upande gani kwenye suala la Richmond.
Wanachama wanaoamini kuwa Kamati ya Mwakyembe ilifanya kazi vizuri na ripoti yao ni ya mfano wa kuigwa, wanajikuta ndio wanapigia kelele vita dhidi ya ufisadi, wakati wengine wako upande wa pili.
Kwa kadiri siku zinavyozidi kwenda mbele, kambi hizi mbili zinazidi kwenda pande mbili mbalimbali. Kutokana na tofauti hizo, moto wa uchaguzi utakapoanza kuiva, ndivyo pande hizi mbili zitatofautiana zaidi na kupania kuangushana; matokeo yake yatakuwa kuvunjika kwa CCM.
Chukua mfano wa mpira utengenezao manati. Una kiasi chake cha kuvutika. Kuna mahali inafikia ule mpira utakatika. Utavuta lakini hautavutika zaidi. Utakatika. Hivyo ndivyo itakuwa pia kwa CCM.
Pamoja na jitihada za kujaribu kutafuta mapatano kati ya pande hizi mbili, ukweli utabakia kuwa pasipo kutengana mapatano hayo hayawezi kufikiwa. Mapatano yoyote ndani ya CCM ya sasa kati ya pande hizi mbili yatakuwa ni mapatano ya kinafiki.
Lakini kuna jambo jingine kubwa litakalosababisha pande hizi mbili kutengana. Uongozi wa juu ni dhaifu kuliko wakati mwingine wowote ule.
Ni udhaifu wa misimamo na mitazamo. Unawaweka mahali pagumu sana kupatanisha pande hizi mbili na kuiokoa CCM inayozama. Siyo vikao vya chama wala matamko ya chama yanayoweza kukiokoa CCM hivi sasa. Tuwaangalie baadhi ya vigogo hao.
Rais Jakaya Kikwete ana majukwaa mawili ambayo yangetakiwa kumpa nguvu: Urais wa nchi na uenyekiti wa chama chake. Bahati nzuri au mbaya, Kikwete anajikuta amedhoofishwa katika pande zote mbili.
Kwa upande uenyekiti, Kikwete anakabiliana na uasi wa wazi ndani ya chama chake ambao umebatizwa jina la "demokrasia." Uasi huu unaongozwa na kundi la viongozi ambao waliathirika katika sakata la Richmond na ambao wanahusishwa na vitendo kadhaa vya ufisadi.
Bahati mbaya ni kuwa baadhi ya waliomo katika kundi hili ndio walimsaidia kupata urais. Hilo linamuweka rais mahali pabaya na pagumu; ni kama kujaribu kuchagua kuangukiwa na chuma au mwamba.
Hivyo, kwa Kikwete kujaribu kuwapigia kelele hawa itakuwa ni kama kuwanyoshea wao kidole kimoja, huku vitatu vikinyoshwa kwake na dole gumba kwa Mungu kama shahidi. Kikwete hawezi kupambana nao kama jemedari; anachoweza kufanya ni kutegemea mkakati wa "kiufundi" yaani kuacha "liwalo na liwe."
Hii ndiyo sababu Kikwete hajafanya juhudi za kufunua na kufumua tuhuma za Meremeta, Dowans na Kagoda.
Jingine ambalo Kikwete anakabiliana nalo, ni kwamba wakati mwingine Waziri Mkuu Mizengo Pinda anasimamia sheria jinsi zilivyo na mara kadhaa amekuwa akitoa maelekezo ambayo yanagongana na sheria zetu na hivyo kujiweka kwenye mstari mwembamba.
Ndani ya CCM, Pinda hana nguvu kama alizokuwa nazo Lowassa. Siyo mwanasiasa hasa na yawezekana ndiyo sababu ya kuteuliwa kwake kwani ni mtendaji zaidi kuliko mwanasiasa. Hivyo, anahofiwa kwenye masuala ya utendaji lakini siyo kwenye masuala ya kisiasa kwani hana ule ubavu wa kuweza kuiokoa CCM.
Lakini kuna kubwa zaidi. Hili la CCM kutokuwa na katibu mkuu mwenye sifa. Katibu mkuu wa sasa, Yusuph Makamba ameonesha uongozi dhaifu mkubwa.
Wengi wetu tunamfahamu Makamba kutokana na staili ya utawala wake akiwa ameshika nafasi mbalimbali za kiutendaji; kuanzia akiwa mkuu wa wilaya hadi mkuu wa Mkoa. Kuanzia akiwa Tanga, Kigoma na hata Dar es Salaam. Tunamfahamu kwa vichekesho vyake, nukuu zake za Kurani na Biblia na ufuatiliaji wake wa jambo hadi kuona mwisho wake.
Makamba yeye ni "mkanaji." Kwake yeye CCM ni safi, hakuna matatizo, na ni chama ambacho kinaongozwa na sera safi na watu wasafi. Kwa maoni yake mtu yeyote anayeonesha mapungufu ya CCM ni mwongo, mzushi na apuuzwe kwani anataka kupandikiza "chuki" dhidi ya chama.
Hivyo haya malumbano ya kina Kingunge na Malecela na wengine ni "demokrasia" wakati kila mtu anajua ni "domoghasia," yaani ghasia zifanywazo kwa mdomo.
Pius Msekwa – Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara – naye ni miongoni mwa wataalamu mahiri wa mambo ya Bunge na itikadi ya CCM. Hata hivyo ameingia katika nafasi hiyo akiwa hajui kama yeye ni mnyama au ndege. Kwa vile anafanya kazi kama makamu wa mwenyekiti basi nguvu zake na shughuli zake zinamtegemea sana mwenyekiti. Siyo mwanasiasa mahiri.
Hana sauti ndani ya chama ya kumfanya atiliwe maanani na hivyo mara nyingi amekuwa akipuuzwa. Kosa lake kubwa lilikuwa ni lile la kugeuka ahadi yake mwaka 2005 kwamba hatagombea tena nafasi ya spika wa bunge; kitu ambacho kuna wana CCM hawakumsamehe na wakafanya mbinu ya kumuangusha.
Yeye, kama Makamba ni mkanaji. Anakana matatizo yaliyoko ndani ya CCM akiamini kuwa siyo ya kimfumo au kimuundo bali ni ya mtu mmoja mmoja. Ninakumbuka kauli yake aliyotoa Afrika Kusini ambako alikana kuwa mpasuko wa ANC (uliozaa COPA) hauwezi kutokea CCM.
Wakati akiisifia CCM huko Afrika ya Kusini kuwa ni chama kilichopita mambo ya kikabila, leo hii tunaweza kuona sumu kali ya udini ikikinyemelea chama hicho kama mumiani wakati wa ajali.
Hata hivyo, tukimuuliza kuhusu udini huo nina uhakika hawezi kukubali kwa sababu yeye ni mkanaji kama Makamba.
Rais Amani Karume – Makamu Mwenyekiti wa CCM (Visiwani): Kwenye siasa za chama kitaifa Karume yuko pembeni sana. Zaidi ya kuitwa kwenye hafla za hapa na pale na kuonekana kwenye dhifa mbalimbali, Karume hana sauti ya sera wala itikadi. Yuko kimya kama aliyejitenga na siasa za kitaifa.
Lakini zaidi pia, Karume mwenyewe anasumbuliwa na siasa za "Upemba na Uunguja" na hivyo anajikuta anabanwa na siasa za Visiwani kuliko kwingine. Leo hii kunakotokea matatizo ya uandikishaji huko Pemba, serikali yake inafura na kuwa mkali kukosolewa.
Kwa muda wote huu uliopita anafuata staili ya uongozi wa Kikwete ya kuwaletea watu "vitu" badala ya "utu" kwanza. Hivyo, wanajenga barabara, shule na hospitali Pemba wakiamini kwa kufanya hivyo wanawavutia wapenzi wa CUF na CCM. Kumbe Wapemba wanasema, "Hospitali tutakwenda, barabara zenu tutatumia, lakini katu hawaichagui CCM.
Samwel Sitta, Spika wa Bunge la Jamhuri, huyu ana nguvu ambayo wengine hawana. Ana nguvu ya cheo cha uspika na hivyo kumpa sauti ambayo hakuna mbunge mwingine wa CCM anayo. Kutokana na maamuzi yake mbalimbali amejitengenezea maadui wazito sana ambao hawajamsamehe hadi leo hii kuanzia suala la Richmond na wamepania kumuangusha.
Ili watuhumiwa wa ufisadi waweze kushinda mwaka 2010 na kuendelea kututawa, ni lazima Sitta aangushwe. Sasa hivi anategemea zaidi huruma na hisani ya rais na waziri mkuu, kwani hao wawili wakionesha tu kutoridhishwa na Sitta, basi wimbi la mashabiki wake bungeni linapeperuka kama vipepeo waliokosa maua.
Kati ya viongozi wote wa CCM ni rais mstaafu Benjamin Mkapa anayeonesha kunyong'onyea zaidi. Tuhuma zilizomwandama kwa miaka miwili hivi, zimemdhoofisha na kauli atakayotoa yaweza kuzua maswali mengi.
Edward Lowassa, aliyekuwa waziri mkuu na anayeendelea kuwa mbunge wa Monduli, angekuwa shujaa wa nchi hii baada ya kujiuzulu, lakini alijipenda yeye zaidi kuliko taifa lake; akapenda urafiki wake na ushirika wa wenzake kuliko kuwachukia maadui wa taifa hili.
Na yeye kama wengine ni mkanaji. Hadi hivi sasa hajakubali kuwajibika kwa suala la Richmond na bado anaona kuwa alionewa.
Makanusho ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu na Katibu Mkuu KiongoziPhilimon Luhanjo yamezidi kumuweka mahali pabaya zaidi Lowassa. Yeye hawezi kukinyoshea CCM kidole isipokuwa kama kwa manung'uniko ya kuonewa.
Wapo wanasiasa wengine kama kina Rostam Aziz, Andrew Chenge, na wengineo ambao wote ni dhaifu tu ndani ya CCM. Wanasiasa hawa pamoja na mashabiki wao, wanaendelea kuonesha kuwa chama hiki hakiokoleki pasipo mabadiliko makubwa.
Kwa vile tofauti yao ni ya mambo ya binafsi na siyo ya kiitikadi, ni wazi kuwa hawawezi kukaa pamoja. Ni sawa na kujaribu kuanzisha maisha ya "kijamaa kati ya chui, mbuzi na majani" kwenye zizi moja.
Hivi sasa CCM haisafishiki, haiteteeki, haisalimiki na haiokoleki. Heri unabii ambao niliuzungumzia miaka minne iliyopita: "Bora chama kimoja kife (CCM) kuliko taifa zima kuangamia."