CCM karibu ife: Vijana wafuate nini huko?


Mabere Marando's picture

Na Mabere Marando - Imechapwa 06 July 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

GAZETI la Citizen la 20 Aprili 2011, lilichapisha makala ya Ayub Rioba, ikimsifu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilson Mukama, kwamba ni mtu mwenye uwezo wa kukifufua chama hicho.

Aidha, mwandishi ameishauri sekretarieti mpya ya CCM inayoongozwa na Mukama ikirekebishe chama hicho ili kiwe ni chama kitakachovutia vijana kutokana na msimamo wa chama, badala ya vijana hao kufanya kazi kwa matakwa ya wale wanaofadhili chama.

Kimsingi mambo hayo mawili ndiyo yaliyonisukuma kuandika makala hii. Lengo si kumjibu mwandishi, bali kuwapanua mawazo vijana ili waweze kuamua hatma ya nchi yao.

Kuna dalili za kufa kwa CCM. Hii inatokana na hatua ya viongozi wake kutoana macho hadharani. Wanachogombea siyo itikadi, bali ni ugomvi wa chakula. Ni kwa sababu, kundi moja ndani ya chama limefanikiwa kunyang’anya kundi jingine, “mapato” ambayo yanatokana na rushwa.

Siyo kwamba kundi lililobaki halipendi rushwa. Hao wanaotukanwa sasa, waliwazidi wenzao ujanja. Ndiyo chanzo cha vita hivi viliyopewa jina la “kujivua gamba.”

Ugomvi huu ndani ya CCM umesaidia sana kuwafumbua macho wananchi. Kwa muda mrefu viongozi wa chama hiki walikuwa wanasema, chama chao hakina ufisadi.

Sasa wao wenyewe wamekubali kuwa ndani ya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), wamejaa mafisadi. Hii ndiyo mada ambayo CCM wametuletea.

Ushahidi ni kauli ya John Chiligati, naibu katibu mkuu wa chama hicho aliyenukuliwa mara kadhaa akisema, “…ndani ya CCM hakuna ufisadi” na kusisitiza, “Kama viongozi wakuu wa CHADEMA (Chama cha Demokrasia na Maendeleo) wana ushahidi, walete hadharani.”

Naye mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Edward Hoseah, ndiye amekuwa akikingikia kifua mafisadi ili wasishitakiwe.

Pamoja na ufisadi kuwa kosa la jinai, lakini wao kwa wao hawashitakiani, maana ni wenzao ndani ya chama na serikali.

Kimsingi Mukama hana tofauti na mtangulizi wake, Yusuf Makamba. Tofauti ni kwamba Mukama ana shahada, Makamba hana. Lakini sote tunajua kuwa shahada hazibadilishi kitu. Ndiyo maana Rais Kikwete, ambaye ana shahada alimteuwa Makamba kuwa mtendaji mkuu wa chama. Ni kwa sababu wanafanana kiitikadi ndani ya chama.

Nirejee historia. Sisi tuliosoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka ya 1970 pamoja na Kikwete na Mukama, wachache wetu tulikuwa tunakubaliana kwamba kuna uozo na ubabaishaji ndani ya TANU.

Walioingia TANU kwa lengo la ulaji lakini kwa madai kuwa wataleta mabadiliko wakiwa humohumo ndani, wameshindwa kabisa. Matokeo ya wao kuingia katika uongozi ni kuingiza nchi katika mikataba tata ya IPTL, Richmond, Songas na mingineyo na wizi wa fedha za umma kupitia makampuni ya Kagoda Agriculture Limited, Deep Green, Meremeta na ununuzi wa rada ya kijeshi.

Kwa msingi huo, Mukama hana ubavu wa kubadilisha chochote ndani ya chama chao. Hii ni kwa sababu tofauti ziliojitokeza si za hoja, wala itikadi. Ni tofauti kati ya mtu na mtu na ushindani katika ulaji na kutafuta madaraka.

Kwamba kama ni gamba, basi CCM ndilo gamba. Kwamba kwa sera zake na kilivyotekeleza kazi zake, hakiwezi kuwavutia vijana wa kizazi cha sasa. Vijana wengi nchini wamekosa masomo ya juu kwa sababu ya sera mbovu zikiwamo zile zinazotaka kila mzazi masikini kulipia masomo ya mtoto wake.

Matokeo yake, watoto wa wenye uwezo ndio wamepata masomo, huku wale wa kutoka familia masikini, wakiishia kusota mitaani. Hata wale waliobahatika kusoma kwa wazazi wao kuokoteza hapa na pale, wengi wao wanasota mitaani na digrii zao kwa kuwa wamekosa watu wa kuwashika mikono serikalini.

Vijana wengi walioko CCM ni wale wanaotegemea kutumia uongozi kutafuta mali. Bali wale wenye nia njema na taifa hili; wale wenye dhamira ya dhati ya kuondoa nchi katika lindi la umaskini, wamejiunga na CHADEMA.

Vijana wanatambua tofauti za kiitikadi kati ya CHADEMA na CCM. Wakati CCM kinarubuni umma kwa kupindua ukweli, CHADEMA wanasimama katika ukweli.

Kwa mfano, CCM wanasema itikadi yao ni ujamaa na kujitegemea. Lakini ni wao wanaogombana kwa sababu baadhi ya viongozi wake, wakiwamo wale wakuu, wamejitajirisha kupitia nafasi za umma. Wapo wengi waliohifadhi mabilioni ya shilingi katika mabenki ya Ulaya.

Katika kupumbaza wananchi, viongozi wa CCM wameamua kuita mabilioni hayo “vijisenti,” huku mwananchi wa kawaida akishindwa kulipa “mchango” wa Sh. 20,000 kwa mtoto wake katika sekondari ya kata.

CHADEMA kinaamini katika kujenga na kuimarisha uchumi wa soko huru, utakaoheshimu na kulinda haki na mali za raia wake. CCM kinaamini katika uchumi holela, huku kikiwadanganya wananchi kuwa taifa hili, linalotegemea wafadhili hata kwa ujenzi wa vyoo katika shule na zahanati za serikali, linajitegemea.

Ukiangalia vipengele hivyo viwili, utaona kwa nini baadhi ya viongozi wa CHADEMA wanafanya biashara zao kiuwazi na bila kutegemea rushwa au hisani kutoka kwa watawala.

CHADEMA kinatetea rasilimali za taifa yikiwamo madini bila woga, huku CCM wakishirikiana na watu wa nje kuingiza taifa katika mikataba isiyo na tija.

CHADEMA kinaamini katika umuhimu wa uhuru wa kuamini katika kujenga maadili ya jamii bila kuifanya dini kuwa sehemu ya dola. Lakini CCM wamejenga tabia ya kugombanisha madhehebu makuu ya dini nchini hasa katika kila kipindi cha uchaguzi kinapowadia.

CHADEMA kinaamini katika kuwajengea uwezo wazawa kuendesha uchumi wao.

Hii haina maana ya kuzuia wengine wasio wazawa kumiliki vyanzo vya kiuchumi. Lengo ni kuonyesha kwa vitendo tofauti iliyopo kati ya vyama hivi viwili.

Hakuna mahali popote ambapo CCM inatamka uthabiti wake wa kutetea wazawa. Badala yake, kivitendo CCM kinabagua wananchi.

Makampuni mengi aliyoyaacha Mwalimu Nyerere yamegawanywa kwa wageni. Hata mikataba ya ujenzi wa barabara wamepewe wageni. Kuna wageni wanauza hadi vitumbua mitaani.

Kuna tofauti nyingi kati ya itikadi ya CHADEMA na CCM. Kwa mfano, katika kipindi cha kampeni CHADEMA ilisema itasomesha bure, hadi chuo kikuu, kila mtoto atakayefaulu mtihani. Ni tofauti na CCM inayoendesha ubaguzi kwa kulipia wale tu waliofaulu daraja la juu.

Wengi wanaonufaika na utaratibu huu, ni watoto wa vigogo waliosoma kwenye shule zenye hadhi, zilizosheni vifaa vya kufundishia na walimu wenye ujuzi.

CHADEMA kinataka rasilimali za taifa zimilikiwe na wananchi wenyewe ambapo kila mtu, bila kujali asili na hali yake, ataweza kutumia vipaji vyake kutimiza malengo ya taifa.

Hiyo ni kinyume na sera za CCM zinazoruhusu makampuni makubwa ya madini kutoka nje, kukomba raslimali za taifa. Katika mazingira haya, nani anaweza kufaulu kurubuni vijana kukimbilia CCM? Hawatafaulu.

0
Your rating: None Average: 2.7 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: