CCM mnasikitisha


editor's picture

Na editor - Imechapwa 29 February 2012

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MWENENDO wa uongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unasikitisha mno. Masikitiko yenyewe ni yale yanayotokana na utamaduni mbaya wa kuujua ukweli, halafu kwa makusudi, viongozi wakaamua kuudharau.

Viongozi wa kitaifa wa CCM wamejenga mazoea mabaya ya kustawi kutokana na kuweka mapenzi mbele ya rushwa.

Ndani ya mfumo wa chama hicho kinachoongoza dola, tatizo la rushwa na ufisadi linafahamika vizuri. Ni tatizo ambalo linakipotezea mvuto chama.

Tena ufahamu mpana wa tatizo hili, unaanzia kwa mwenyekiti wa chama mwenyewe, Rais Jakaya Kikwete.

Yeye amekuwa mara kwa mara akikemea matumizi ya fedha katika uchaguzi ndani ya chama chake.

Alifanya hivyo mwaka 2007 alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa CCM mjini Dodoma.

Hapo, alionyesha kuguswa sana baada ya kuelezwa na wasaidizi wake kuwa wapambe wa wagombea walikuwa wakitembeza fedha nje ya ukumbi kuvutia kura kwa wagombea wao wakati wanaochagua walikuwa ukumbini akiwahutubia.

Kwa jumla, Rais Kikwete anakataa wanachama kutumia fedha (rushwa) kupata uongozi.

Lakini, tunaona kinachofanyika kwenye vikao anavyoviongoza kinasaliti dhamira yake hiyo ya kukemea rushwa.

Kamati Kuu ya chama hicho Jumatatu jioni ilisikiliza tuhuma nzito za rushwa zilizokabili makada walioomba kugombea ubunge jimbo la Arumeru Mashariki.

Hata hivyo, pamoja na ushahidi imara kuwasilishwa, na mjumbe wa CC kutajwa kuwa amesaidia rushwa, hakukubadilika kitu.

Rais Kikwete alikubali wawili walioongoza kura za maoni wapigiwe tena kura ili apatikane mshindi kwa kuwa hakuna aliyefikia nusu ya kura zilizopigwa.

Ina maana, CCM imeachia watuhumiwa wa rushwa wapitishwe kugombea ubunge.

Huko ni kuachia dhambi iendelee; utamaduni usiokubalika.

Kama viongozi wa CCM wanaamini kuwa hawawezi kukomesha rushwa katika chama chao, basi angalau pale wanapoithibitisha kutendeka, wasiivumilie.

Ni bahati mbaya fikira za viongozi hawa zimeshachoka. Hazifanyi kazi tena na haziwezi kubadilisha baya likawa zuri. Ni fikira muflis.

Hivi Kamati Kuu wangeamua kufuta wagombea wote na kuitisha wapya wakapigiwa kura, wangepoteza nini? Kumbe hata heshima wanaichukia.

Kwa hali hiyo, njia iliyobaki ni moja tu: Viongozi hawa wakubali kukaa pembeni; kuliko kujing’ang’aniza madarakani.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: