CCM Mwanza nako kwafukuta

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mwanza hakiko salama. Kimegawanyika. Mgawanyiko umeibuliwa na makundi yanayokinzana ndani ya Umoja wa Vijana wa chama hicho (UV-CCM).
Ni mgogoro wa aina yake. Kwa kiwango kikubwa unafanana na ule ulioibuka Dodoma mwezi uliopita, ambapo wabunge wa chama hicho walifikia hatua ya “kuvuana nguo” hadharani.
Makundi mawili, moja likiwa na nia ya kusafisha ufisadi na lingine likitetea na kulinda maslahi binafsi ya baadhi ya viongozi.
Tayari Baraza Kuu la UV-CCM la mkoa limemsimamisha uongozi mwenyekiti wa vijana wa mkoa, Boniphace Magembe. Katibu wa UV-CCM wilaya ya Nyamagana ambaye ni kaimu katibu wa mkoa wa umoja huo, Mobutu Malima naye yuko katika mkumbo huo.
Malima na Magembe wanatuhumiwa kutafuna zaidi ya Sh. 9.3 milioni. Sambamba na kusimamishwa nyadhifa zao, viongozi hao wa baraza wanataka uongozi wa juu wa UV-CCM kuwachukulia hatua zaidi za kisheria wahusika.
Hata hivyo, jitihada hizo tayari zimeingia doa. Katibu wa CCM mkoa wa Mwanza, Rajabu Kundya, ametangaza kutoyatambua maamuzi hayo. Anasema ni batili. Kwamba yamekiuka taratibu na kanuni za UV-CCM.
Anaonekana dhahiri kachukizwa na maamuzi ya baraza. Kundya anasema: “Baraza halina mamlaka ya kusimamisha viongozi hao, ambao uteuzi wao wa mwisho hufanywa na Halmashauri Kuu ya Taifa. Walipaswa kupeleka hoja yao kwa chama mkoa.”
Kujiingiza kwake katika mgogoro huo kunatokana na kuhofia mageuzi kama hayo kumkuta katika nafasi yake kutokana naye kuhusishwa katika kashfa ya nyumba za CCM ambazo mapato yake yamekuwa yakizua tafrani.
Kundya anasema kanuni za UV-CCM zinamtaka katibu wa umoja huo kushauriana na mwenyekiti wake. Iwapo mwenyekiti na katibu ndio watuhumiwa na hivyo hawataki kuitisha kikao, basi wajumbe wanapaswa kupeleka hoja ya kuomba mkutano kwa CCM mkoa ili kiweze kuusimamia.
Kuna tuhuma nyingine. Hizi zinamgusa Katibu Mkuu wa UV-CCM, Martine Shigela. Kwamba anawabeba viongozi wanaotuhumiwa.
Hata hivyo, mgogoro huo huenda ukachukua sura ya mwaka mmoja uliopita, yaani Septemba, 2008. Kulikuwa na mpasuko mkubwa ulioibuliwa na Nape Nnauye, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), baada ya kubainisha kuwa kulikuwa na ufisadi katika mradi wa ujenzi wa jengo la kitega uchumi la UV-CCM makao makuu, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa muda wa baraza lililowasimamisha viongozi hao katika kikao cha wiki iliyopita ni Alexander Mnyeti. Anasema wanazo nguvu kisheria kuutetea uamuzi huo. Kwamba waliazimia kuwasimamisha uongozi wa UV-CCM mkoa wa Mwanza, kwa kuzingatia kanuni na taratibu za umoja huo.
Kanuni ya UV-CCM inayotajwa ni ya toleo la 8 la mwaka 2008 ibara ya 7 (1). Kanuni hiyo ndiyo iliyotumima kumwadhibu mwenyekiti, Bonphace Magembe na katibu Mobutu Malima. Lengo ni kupisha uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha za umoja.
Kwamba, viongozi hao wanapaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa kanuni za umoja na katiba ya CCM kwa kuhusika na tuhuma za ubadhirifu wa Sh. 9, 324,416, ambazo ni mali ya UV-CCM, huku wakijua kuwa jambo hilo ni kinyume cha kanuni ya UV-CCM toleo la 8 la 2008, ibara ya 80 (b).
Katika kuonyesha kama asiye na dhamira ya kupambana na ubadhirifu huo, Kundya amemzuia mjumbe wa UV-CCM, Ibrahim Hamis, ambaye ameteuliwa kwa muda na kikao hicho cha baraza, kukaimu nafasi ya katibu wa umoja mkoa mpaka hapo uchunguzi utakapo kamilika. Ibrahimu Hamis ni katibu wa umoja huo wilaya Sengerema.
Katibu Mwenezi na Uhamasishaji wa UV-CCM mkoa wa Mwanza, Manyasi Bandoma, anasema baada ya Kamati ya Utekelezaji ya UV-CCM mkoa kubaini ubadhirifu huo, iliwaomba viongozi hao kuitisha vikao vya ngazi ya mkoa kujibu tuhuma hizo, kwa kuzingatia kanuni ya UV-CCM toleo la 8 la 2008, ibara ya 131 (d), lakini walishindwa kutekeleza jambo hilo wakihofia kusulubiwa.
Kutokana na kushindwa kwao, 30 Oktoba, mwaka huu, kamati ya utekelezaji ilipokutana, iliazimia kulifikisha suala hilo katika Baraza Kuu la UV-CCM mkoa, ambalo lina mamlaka. Lilikutana mosi Novemba, na kuazimia kuwepo na kikao kingine kabla ya 15 Novemba, mwaka huu, ambacho watuhumiwa watajieleza na kujitetea. Hadi 10 Novemba pamoja na kupata taarifa na maelekezo ya baraza, walikaidi kufanya hivyo.
Mgogoro unakomaa taratibu. Unaibuka kutokana na wanachama na viongozi wa CCM mkoa kuhasimiana katika uchaguzi wa wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji baada ya kujijengea kambi.
Kambi zilizoibuka katika uchaguzi huo zinatokana na makatibu wa CCM wa matawi kuengua waliokuwa wameandaliwa na wabunge na madiwani na kupitisha watu wengine kwa faida ya kambi moja kati ya zile zilizokuwa zikihasimiana.
Katika mgogoro huo wa UV-CCM, mbali na ubadhirifu, mwenyekiti amekuwa akituhumiwa kutumia fedha za umoja huo kwa ajili ya maandalizi ya kugombea ubunge jimbo la Magu, linalowakilishwa na Festus Limbu. Mwenyekiti anaungwa mkono na Kundya.
Mpasuko umeanzia wilayani Magu, anakotoka Magembe. Huko kumeibuka makundi hasimu ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji.
Katibu wa chama hicho wilayani Magu, Hamida Mbogo, anauzungvumzia mpasuko huko. Anaufananisha na ule wa viongozi wa juu wa CCM. Kwa upande wa Magu anauona kuwa umepunguza ushindi wa wagombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa,vijiji na vitongoji.
Hamida anasema makundi yameigawa CCM katika makundi mawili, ambayo yanaweza kuleta mpasuko mkubwa na kukivuruga chama. Kwamba unatokana na taswira ya CCM inayoendelea, ambapo viongozi wa juu wamegawanyika.
“Makundi haya hayaishii juu yamekuja hadi huku. Baadhi ya maeneo yamesababisha CCM kupoteza viti katika serikali za mitaa. Ni kutokana na kuharibiana katika kampeni na kujikuta upande mmoja ukiamua kusaidia upinzani kwa lengo la kukomoa upande mmoja,” anasema Mbogo.