CCM ndio wavivu wa kufikiri


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 19 October 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

NDIVYO alivyo Rais mstaafu Benjamin William Mkapa. Akitaka kujisafisha kutokana na tuhuma nzito zinazomkabili, hudai “watu wavivu wa kufikiri na hufanya mambo kwa hisia.”

Walengwa wa kauli hiyo inayokirihisha masikioni huwa si wengine bali wakosoaji wake au wapinzani.

Hata alipozungumza wiki iliyopita katika kongamano la kumbukumbu ya miaka 12 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere lililofanyika Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Mkapa alirudia kauli hiyo.

“Watanzania wengi ni wavivu wa kufikiri badala yake wanaruhusu hisia zao kutawala….”

Tujiulize maswali mepesi. Je, wavivu wa kufikiri lazima wawe raia wa kawaida tu? Je, hawawezi kuwa ni viongozi wa serikali na chama tawala?

Je, wanaoshupalia suala la yeye kujibinafsishia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya, na kuanzisha kampuni ya kibiashara akiwa bado Ikulu, jambo ambalo ni kinyume na maadili ya uongozi wa umma, nao ni wavivu wa kufikiri?

Tukitazame chama alicho – Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mwaka 2008 kipindi kama hiki cha kumuenzi Mwalimu Nyerere, viongozi waliingiwa na uvivu wa kufikiri. Waliposoma habari katika MwanaHALISI iliyokuwa na kichwa “Njama za kumwangusha Kikwete zabainika” wakaitaka serikali ifikiri kwa niaba ya CCM.

Aliyekabidhiwa jukumu hilo alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika. Akavaa miwani yake, akafinyafinya macho, akapulizia mvuke miwani na akafuta. Alipojiona anaona vizuri maandishi, akasoma habari ile huku akitetemeka. Akajiuliza cha kufanya. Hivi gazeti linaweza kubaini njama hizi? Je, huku si kudhalilisha Polisi, Usalama wa Taifa au Jeshi la Wananchi?

Majira ya Saa 5.00 asubuhi ya tarehe 14 Oktoba 2008, akiwa amejiridhisha alikuwa ameielewa vema habari ile, Mkuchika akatuhumu MwanaHALISI wameandika uchochezi.

Habari ile ilifichua mpango wa baadhi ya makada wa CCM kukwamisha uteuzi wa Rais Kikwete kugombea tena urais mwaka 2010. Pia iligusia mkakati wanaopanga kushawishi kutengenishwa kofia ya urais na uenyekiti wa chama.

Makada hao walikuwa wanadai Rais Kikwete ameshindwa kuimarisha chama. Mjadala huo ndio unaitesa CCM hadi leo.

MwanaHALISI tulisikia, tukafuatilia na tukahoji watu maarufu na waliotajwa kuwa nyuma ya mkakati na tukaelezwa sababu zake. Baada ya kujiridhisha na vyanzo vyetu mbalimbali, tukachapisha habari tukiamini tunaizindua CCM.

Tuliamini tunasaidia Sekretarieti ya Kamati Kuu (CC) yake kufuatilia kipelelezi.

Lakini badala ya intelijensia yake kuchunguza, wakamtuma Mkuchika afungie gazeti lililosaidia CCM. Kweli, akafungia MwanaHALISI kwa miezi mitatu eti limeandika uchochezi.

Kwa uvivu tu wa kufikiri, CCM wakaamini wamekwepa na kuficha ukweli. Kwa uvivu tu wa kufikiri wakataka jamii iamini CCM ingali imara, haijapasuka, haina makundi. Tatizo ni MwanaHALISI. Wakapakazia tunataka kuchafua amani na utulivu wa nchi.

Habari hizi zilipotua kwa aliyekuwa Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, naye kwa uvivu tu wa kufikiri, akasema wale wanaofikiria kutenganisha kofia ya urais na uenyekiti wa chama ni wahaini.

Miaka mitatu kamili tangu MwanaHALISI liadhibiwe kwa kufichua njama za ‘uasi’, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye amethibitisha kilichofichuliwa na MwanaHALISI.

Tatizo lilikuwa dogo mwaka 2008. Leo, kwa uvivu tu wa kufikiri limekua na linawashinda kuliondoa. Wanavuta shuka kumekucha. Ukweli, linahatarisha uhai wa CCM kama chama dola.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: