CCM ni kuchinjana wakose wote


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 15 June 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

CHAMA cha Mapinduzi (CCCM) hakitamaliza harakati zake za kuchinjana. Naam, maandiko yanasema auae kwa upanga naye hana budi kufa kwa upanga.

Niliposikia kauli ya Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, juu ya adhabu walizopewa baadhi ya wanasiasa vijana wakiwamo akina James Ole Millya, Mrisho Gambo na wengine, nilihitimisha kitu kimoja tu, kwamba CCM itaendelea kuchinjana hadi mtu wa mwisho atakapokosa wa kumchinja.

Awali ilijulikana kwamba makundi ni matokeo ya kuwapo harakati za uchaguzi ndani ya CCM.

Kwa bahati mbaya sasa, makundi yamekuwa mchezo mbaya ambao wachache wanatumia kuwamaliza wote waliohisiwa ama walikuwa sababu moja au nyinyine ya kukosa madaraka, ushindi au fursa fulani fulani ndani ya chama na hata serikalini kwa sababu nafasi hizi ziku hizi zimekuwa zawadi.

Mwanasiasa mmoja mkongwe nchini alinisimulia kisa cha jamaa mmoja alivyojisalimisha kwa Mzee Rashidi Kawawa (marehemu) wakati huo akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM juu ya fitina alizofanyiwa hadi akakosa kuteuliwa kuwania ubunge.

Mwanasiasa huyo alisema kwamba Mzee Kawawa alimtazama jamaa alivyokuwa analalamika akitarajia kuwa Kawawa angemhurumia. Lakini kwa mshangao wake, alipata jibu lililomfanya kufikiri mara mbilimbili juu ya kuendelea kubakia katika uwanja wa siasa au la.

“Unanitazama nilivyo?” Kawawa alimhoji jamaa huyo aliyekuwa analalamika kwa machungu ya kifitiniwa. Jamaa huyo alijibu, “Nakuona mzee, kwani kuna nini?” “Unaniona? Mimi nilikuwa nani, makamu wa rais, waziri mkuu, waziri, lakini sasa mimi ni nani?” aliuliza Mzee Kawawa.

Akaendelea, “Hayo yote uliyosema na haya yote yangu ni mikikimikiki ya kisiasa. Hiyo ndiyo siasa. Kupata na kukosa, kuna leo na kesho. Mmoja anapata leo mwingine anakosa. Ipo siku itakuwa nafasi yako.”
Alisema baada ya majibu ya Kawawa jamaa huyo aliondoka huku amejinaamia akiwaza ‘Kumbe siasa ni mikikimikiki, kuna kupata leo kuna kukosa kesho na kinyume chake.’
Ukitazama yanayotokea Arusha, ni kielelezo kwamba zile siasa za kukunja jamvi leo ndani ya CCM kusubiri wakati ujao ni kitu ambacho hakikubaliki tena. Ndiyo maana kuanzia mwaka 2008 hadi 2010, kwa mfano ndani ya CCM ulizuka uhasama mkubwa ambao hakika haujawahi kutokea.

Uhasama huo ndio uliosababisha kuundwa kamati ya upatanisho iliyoongozwa na Mzee Ali Hassan Mwinyi ikiwa na wajumbe Pius Msekwa na Abdulrahaman Kinana, ikiwa na kazi ya kupatanisha makundi yaliyokuwa yanahasimiana vilivyo.

Kundi moja likijipachika kuwa ni wapambanaji dhidi ya ufisadi na jingine likielezwa kuwa ni la mafisadi. Juhudi za kamati ya Mzee Mwinyi hazikuzaa matunda yoyote na hadi sasa bado siasa za uhasama wa kumalizana ni jadi rasmi ndani ya CCM.

Hakuna anayeweza kukataa ukweli kwamba kinachoendelea ndani ya CCM Arusha kwa sasa ni siasa za kuhujumiana miongoni mwa makundi tofauti yenye lengo moja, lakini yakiwa yanapigia upatu watu tofauti – Urais!

Kilichotokea baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 yaani kukataliwa kwa Samuel Sitta kuendelea kuwa spika kwa kipindi cha pili kwa kisingizio cha kutakiwa spika mwanamke ambaye hata hivyo sharti hilo halikuwekwa wazi tangu mwazo ili wanaume wote waliojitosa kwenye nafasi hiyo wasijisumbue akiwamo Sitta mwenyewe, ni moja ya njia hizi za kuchinjana wazi wazi kisiasa bila hata kuwa na subira ya kutafakari mambo haya kwa mapana yake.

Ukijiuliza kwa makini zaidi kilichomfikisha Andrew Chenge, mjumbe wa Kamati ya CCM na mwenyekiti wa kamati ya maadili wakati huo kujitosa kwenye mbio za uspika ni kitu gani kama si mbinu ya ‘tukose sote?’

Lakini hata kabla ya kufikia uamuzi wa kujadili harakati za Chenge dhidi ya Sitta, ni vema pia kujiuliza kuwa Spika wa sasa, Anne Makinda, alipata wapi ujasiri wa kwenda kuchukua fomu kupambana na bosi wake Sitta, (alikuwa Naibu Spika Bunge la tisa 2005-2010)?

Kwa hiyo, mkakati wa kumchinja Sitta ulifanikiwa, na shangwe zilionekana ndani ya Bunge baada ya Bunge la 10 kuanza kazi. Kwa kuangalia jinsi wenyeviti wa kamati za Bunge walivyopangwa ulikuwa mwendelezo ule ule wa kujipanga kulipizana kisasi.

Lakini kama ilivyo ada, mwosha huoshwa, miezi minne tu katika furaha ya kushinda vita ya muda, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM ikatoka na maamuzi ya ‘kujivua gamba’.

Vita ikaanza upya. Waliokuwa wanaamini kwamba wameteka ngome, wakajikuta wakiwekwa kwenye kikaango cha moto mkali zaidi, haya ndiyo yaliwakuta waliobatizwa Mapacha Watatu, Edward Lowassa; Chenge na Rostam Aziz; kwamba wanatakiwa wapime na wajiondoe kwenye uongozi wa chama hicho wakidaiwa kuwa na tuhuma za ufisadi.

Habari za kila aina zimeelezwa juu ya mapacha hao watatu, mara watapewa barua za kuwataka wajiengue kwenye nafasi za uongozi, lakini pia wanadaiwa watapimwa kwenye NEC ijayo kama watakuwa hawajajiengua kwenye nafasi zao. Kila siku mpya inayokuja, mapya yanaelezwa juu ya mapacha watatu, lakini ukitazama kwa kina kinachozungumziwa kwa sasa ni urais wa 2015, mbinu kuchinjana mapema.

Hata Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) umegawanyika katika picha ya urais. Kila mkoa una msimamo wake juu ya rais ajaye; mgawanyiko huu ndio umeifanya Arusha kuwa kitovu cha mvutano na mgogoro ndani ya CCM lakini pia ndani ya UVCCM kwa kiasi fulani.

Kwa hiyo akina Millya na Gambo hawaadhibiwi wao kama makada vijana wa CCM, ila adhabu zao zinaelekezwa kwa wale wanaowaunga mkono; ni mwendelezo wa mnyukano ambao sasa umekuwa utamaduni wa CCM kwamba hakuna kuvumiliana katika harakati za kiasiasa; yeyote unayehisi kuwa ni kikwazo katika njia yako kuelekea  unakokwenda dawa ni moja, chinjia baharini!

Mwaka 2005 aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, ambaye alikuwa amepakaziwa kila aina ya udhaifu na tuhuma za kujilimbikizia mali , alisema kuwa ukiona watu wanaotumia magazeti kuingia madarakani kwa kuwachafua wengine ni lazima uwaogope kwa sababu wakishaingia madarakani watatumia risasi kukaa madarakani.

Utabiri wa Sumaye haujatimia kwa asilimia mia, ila kilichokuja kutokea ni mbinu zile zile za kumalizana kutumika dhidi ya kundi lililokuwa moja, kisa baada ya wengi kukosa kile walichotarajia, au na wengine kutaka kuwanyamazisha daima wapinzani wao.

Hii ni vita iliyoanzishwa na kikundi kidogo, imekua, imeumuka na sasa imekuwa utamaduni, kuchinjana kwa gharama yoyote.

Baada ya akina Millya na Gambo, watachinjwa wengine wengi, kadri kiti cha urais mwaka 2015 kitakavyokuwa kinahitaji mtu wa kukikalia. Sumu ya kuchinjana kisiasa ni kali ndani ya CCM na hakika haitawaacha hadi watakapomalizana. Ole wao!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: