CCM ni mwendo wa vitisho, mauaji


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 16 May 2012

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

MOJA ya agenda za kudumu katika vikao vyote vya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) huwa hali ya usalama nchini. Taarifa fupi inayotolewa baada kila kikao huwa “hali ni shwari.”

Wanachozingatia wajumbe wa NEC katika kujadili agenda hiyo huwa kutokuwepo nchini kwa mapigano au vita vya wenyewe kwa wenyewe na kutokuwepo vita dhidi ya majirani.

NEC haijawahi kujadili vitisho wanavyopewa baadhi ya wanasiasa mashuhuri nchini kwamba vinaashiria kuwepo usalama mdogo. Wanasiasa wa vyama vyote – CCM, CHADEMA, CUF katika nyakati tofauti wamepata simu za vitisho.

Wabunge waliojipambanua bungeni kupambana dhidi ya ufisadi nchini, akiwemo aliyekuwa Spika wa Bunge ambaye ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta walitishiwa maisha na watu wasiojulikana hadi serikali ikamweka ulinzi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge iliyofuatilia kashfa ya Richmond ambaye sasa ni Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango-Malecela; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe wote walitishiwa maisha.

Sasa wabunge wawili, Deo Filikunjombe, mbunge wa Ludewa na Kangi Lugola wa Mwibara mkoani Mara, ndio wa hivi karibuni kupokea vitisho, siku chache tu baada ya kuunga mkono hoja kupiga kura kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutokana na utendaji mbaya wa mawaziri.

Kwa hiyo, kwa vile mafisadi na mawaziri fisadi wamo ndani ya CCM ni dhahiri, vitisho hivyo vinatolewa na wana CCM hao hao. Na ingawa CCM inadai “usalama upo wa kutosha”, ndani ya CCM yenyewe wanasiasa mashuhuri wanaishi kwa hofu kutokana na vitisho hivyo.

Mfano, katika Bunge la Tisa, mbunge mmoja wa CCM alidaiwa kunyunyiza ‘ndumba’ bungeni. Hata Rais Jakaya Kikwete aliwahi kusema uhasama katika chama umewafanya wana-CCM wasiaminiane tena, kiasi cha kuogopa kuacha wazi glasi ya kinywaji mmoja akitoka kidogo.

Tangu Rais atoe kauli hiyo, ni kama alifungulia vitisho, vipigo na mauaji. Tarehe 17 Mei 2010 Katibu wa Kata ya Isamilo, wilayani Nyamagana, Bahati Stepahano (50), aliuawa saa 6.30 mchana kwa kuchomwa kisu.

Wahusika walikamatwa na kufunguliwa mashitaka akiwemo aliyekuwa Meya wa Jiji la Mwanza, Leonard Bihondo (64). Wengine waliokamatwa wakihusishwa na mauaji hayo ni Jumanne Oscar (30), Baltazar Shushi (47) na Abdul Ausi (45), ambaye ni kada wa CCM kata ya Isamilo.

Kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu mwaka juzi, wafuasi wa CCM walikuwa wanavamia mikutano ya wapinzani na kufanya fujo.

Walivamia Maswa Magharibi kwa lengo la kumfanyia vurugu mgombea ubunge kupitia CHADEMA, John Magale Shibuda. Katika vurugu hizo, kada wa CCM aliuawa. Shibuda alikamatwa na kuwekwa ndani kuhusiana na tukio hilo, lakini baada ya upelelezi wa kina, aliachiwa huru ingawa alizuiwa kufanya kampeni hadi uchaguzi.

Novemba mwaka jana, mgambo, polisi, askari wa Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Wananchi waliacha majukumu yao na kuwapiga kwa risasi za moto wamachinga wa mkoa wa Mbeya kama vile ni waasi. Vurugu zile zilihusishwa na siasa.

Katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Jimbo la Igunga Oktoba mwaka jana, kada wa CHADEMA aliuawa na wana CCM; na polisi hawakujihangaisha kusaka wauaji.

Tarehe 13 Agosti 2011 Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Urambo, Tabora, Juma Dewji alipigwa risasi na watu wasiojulikana. Dewji hakumtaja yeyote isipokuwa alihisi sababu ni msimamo wake wa kutetea haki za wananchi dhidi ya kudhulumiwa fedha na mali na hasa katika kilimo.

Mei mwaka jana mkoani Shinyanga, watu watatu akiwemo mgombea ubunge aliyeangushwa katika kura za maoni Jimbo la Kishapu, Bonda William, walifikishwa mahakama ya mkoa wakikabiliwa na mashitaka ya kutishia, kwa maandishi, kumuua Mbunge wa jimbo hilo, Suleiman Nchambi (CCM).

Walioshtakiwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Shinyanga, John Chaba, ni William, ambaye pia ni Mhasibu, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika; Costantine Deus na Nestory Elias.

Mei mwaka jana aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Mbeya na diwani wa kata ya Kiwira, John Mwankenja (50) aliuawa kwa kupigwa risasi nne kichwani na kufa papo hapo.

Tukio hilo lilizua hisia mbalimbali zikiwemo za kulipiza kisasi katika masuala ya kisiasa. Mwankenja aliuawa majira ya saa mbili usiku nyumbani kwake muda mfupi baada kutoka Mbeya alikokwenda kumuuguza mkewe aliyekuwa amelazwa Hospitali ya Wazazi Meta.

Aprili mwaka jana, watu sita walikamatwa mkoani Mwanza kwa kutishia kumuua aliyekuwa mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni.

Katika tukio hilo, mmoja wa watuhumiwa wakubwa ni mbunge wa sasa Dk. Titus Kamani. Waliokamatwa na kufikishwa mahakamani ni Dismas Zacharia Kamani, Erasto Casmil, Queen Joseph Bogohe na Ellen Bogohe ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa na diwani wa zamani wa Viti Maalum Kata ya Kisesa wilayani Magu.

31 Machi 2012; Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia na Mbunge wa Ukerewe CHADEMA Salvatory Machemli walipigwa mapanga na kuumizwa vibaya na watu wanaosadakiwa kuwa wafuasi wa CCM tena mbele ya polisi baada ya kufunga kampeni za udiwani.

29 Aprili 2012 baada ya CHADEMA kushinda ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki, mwenyekiti wa chama hicho kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo aliuawa kwa kuchinjwa na kitu chenye ncha kali na watu wanaohisiwa kuwa wana CCM. Polisi walikaa kimya hadi CHADEMA walipotoa siku saba.

Mwishoni mwa wiki iliyopita vijana wa CCM mkoani Iringa walimzingira kwa mapanga Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (CHADEMA) wakitaka kumdhuru eti kwa kosa la kushawishi watu kuihama CCM. Lakini wenzake walicharangwa vibaya.

Hali hii inaonyesha wazi CCM wanachukua mkondo usiofaa katika masuala ya siasa na kuhatarisha usalama siyo tu wa wanasiasa mashuhuri bali pia hata yenyewe.

Matukio haya ni mbali na yanayotekelezwa na polisi kuihami CCM. Kwa vigezo vya CCM, Tanzania ina usalama wa kutosha, lakini…..

0789 383 979
0
No votes yet