CCM si tishio tena, wamepuuzwa


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 04 April 2012

Printer-friendly version

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kiliwahi kuwa tishio kwa wananchi. Kwamba ukitaja chama hicho basi watu wanatetemeka.

Arumeru Mashariki na kata kadha wa kadha nchini zimeonesha mara moja na daima kuwa CCM siyo tisho tena. Hawatishi na hata wakijaribu kutisha wanageuka vichekesho kwani watu wamekataa kuogopa.

Kuna msemo kwamba mbwa humfukuza anayeonesha woga. Ni kweli, kwa kadiri unavyomwogopa mbwa ndivyo anavyozidi kukubwekea na unavyokimbia ndivyo anavyozidi kukukimbiza na akikukamata utakiona cha moto.

Kwa muda mrefu, watu wamekuwa wakiogopa sana wakisikia “CCM” au “serikali” kiasi kwamba hata CCM haikutahiji kutisha tena. Yaani, ukiweka bendera tu ya kijani basi watu wanatakiwa kuogopa! Lakini Arumeru na kata kadha wa kadha nchini zimeonesha kuwa CCM si tishio tena.

Walikwenda na rais mstaafu na mwenyekiti mstaafu wa CCM, Benjamin Mkapa wakitarajia watu wa Arumeru Mashariki wangetishika. Hawakutishika. Ving’ora na vimulimuli na umati wa maafisa wa usalama waliomzunguka pamoja na askari lukuki waliokwenda kwa ajili yake havikuwatisha wananchi.

Alizungumza kwa kejeli na dharau kwa wananchi. Aliamini kuwa ana ujiko wa kupendwa, hakujua kwamba wananchi wameshaanza kumkataa moyoni.

Nina uhakika huko aliko haamini kama Watanzania wanaweza kumkataa. Anaweza kuwashangaa kwa “mambo yote mazuri” ambayo anaamini aliwafanyia. Hawakutishwa na wala hawakutishika.

Walikwenda na waziri mkuu wa zamani na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa. Alikuwa kama jinamizi kwenye fikra za watu kwamba kusimama kwake kungesababisha upepo ubadilike, badala ya kupunga kwenda Kusi basi uende Kaskazi. Akasimama na hoja zake za kile alichokiita “kufunga ajenda.” Hakujua wananchi walishafunga “Ajenda ya Lowassa.”

Alijaribu kwa kweli na mtu hawezi kulaumiwa kwa kujaribu. Alijaribu kuwaambia wananchi wa Arumeru Mashariki kuwa tatizo la ardhi lingeshughulikiwa na yeye mwenyewe akiwaongoza wabunge wa mkoa wa Arusha kwenda kwa Waziri wa Ardhi Prof. Anna Tibaijuka. Alitoa na muda kabisa!

Lakini alisahau kuwa yeye mwenyewe aliwahi kuwa waziri wa ardhi kwa muda mrefu!  Alijaribu kuwaambia kuwa tatizo la maji angeweza kulishughulikia lakini alisahau kuwa aliwahi kuwa waziri wa maji kwa muda mrefu tu!

Wananchi wa Arumeru wakapima ukweli wa maneno yake hasa kama kweli alikuwa anataka kusaidia matatizo ya watu wa Arumeru Mashariki. Kama alichosema ni kweli na kama kweli anaamini ana uwezo wa kuwasaidia basi “tarehe 10 saa saba na nusu mchana” atamtafuta mbunge mteule Joshua Nassari wa CHADEMA pamoja na wabunge wengine wa mkoa wa Arusha ambao yeye ni mwenyekiti wao kwenda kwa Tibaijuka.

Kama hatafanya hivyo ina maana alichokuwa anataka ni kumsaidia Sioi Sumari achaguliwe kuwa mbunge, si kwa sababu alikuwa kweli ameguswa na matatizo ya Arumeru Mashariki.

Walikwenda na Waziri Stephen Wassira mmoja wa watu wachache ambao wamewahi kutumikia serikali zote nne katika nyadhifa tofauti tofauti.

Pia ni mmoja wa watu waliowahi kuwa upinzani na kurudi ndani ya CCM. Lakini vile vile  ni mmoja wa watu ambao waliwahi kukutwa na makosa ya rushwa kwenye uchaguzi na bado akapewa nafasi ya kusimamia uchaguzi! Walifikiri watu wangetishika, hawakutishika. CCM haitishi tena.

Wassira alijaribu kurusha vijembe vya kila namna na kujenga hoja zisizo na mashiko kiasi kwamba akajiingiza kwenye matatizo. Badala ya kujijengea heshima kama mmoja wa wazee wa taifa hili akabakia kujishushia heshima yake kwani alipogusa nyumba za watu na yeye nyumba yake ikaguswa! CCM hawakuogopwa!

Walikwenda na mmoja wa wanasiasa vijana Livingstone Lusinde. Lakini kwa uhakika mkubwa, huyo ndiye anguko kubwa la CCM lilipoanzia. Kijana huyu alisimama kwa jina la chama chake na kuanza kuwashambulia CHADEMA na kwa kweli kushambulia aliwashambulia.

Ingekuwa nafuu kama angewashambulia kwa kuonesha udhaifu wa sera zao au ubaya wa hoja zao; angewashambulia kwa kuonesha jinsi gani CDM wameshindwa kuongoza majimbo yao ingekuwa nafuu; yeye aliamua kuporomosha matusi.

Kwa jina la chama chake alianza kutukana; alitukana matusi yanayoandikika na yale yasiyoandikika wala kutamkika. Aliitukana CHADEMA kama chama, lakini kama mtu mmoja mmoja; alimtukana Godbless Lema (mbunge mwenzie) na alimtukana Dk. Willbord Slaa (mtu ambaye nusura angekuwa rais!).

Alitukana mbele ya watoto huku akishangiliwa; alitukana mbele ya kina mama na wasichana. Cha kushangaza chama chake hakikuona makosa; chama chake kiliona ni sehemu ya kampeni tu.

CCM ingeweza kujiokoa vizuri kabisa tena kwa haraka kama ingeamua kumwondoa Lusinde kwenye kampeni na kuonesha kusikitishwa na kitendo hicho. Hawakufanya hivyo, walibariki matamshi yale ya aibu. Walidhani wananchi wangetishika!

Waliongeza polisi, wakapeleka usalama wa taifa, wakabebwa na televisheni ya taifa hadi siku ya mwisho mtangazaji wa watu alitaka kuibeba CCM, kwa bahati mbaya wakampeleka Sioi maskini kijana wa watu akaangusha macho chini asijue la kufanya. Walibebwa hawakubebeka, mwisho wa siku ilibidi wakubali.

Walifanya makosa. Walimteua mtu ambaye asingeweza kushinda, na waliendesha kampeni kana kwamba ndio ulikuwa uchaguzi wao wa kwanza kushiriki. Lakini pia walimpa Lowassa kamba ya kujimalizia na amejimaliza mwenyewe.

Wananchi hawakutishika. Tume dhaifu ya uchaguzi imeshindwa kusimamia uchaguvi vizuri na kwa mara nyingine watu wamemwaga damu! Mabomu ya machozi yamerindima kuanzia Kiwira hadi Usa River kuwatisha wananchi. Hawakuogopa.

Ni kwa kuwa CCM haiogopwi tena, serikali haihofiwi tena. Wanaweza kutisha, wanaweza kujaribu kuogopesha lakini wanaweza kuwaogopesha wale tu wenye kuogopa aliyevuka mstari wa woga haogopwi. Watu pekee ambao bado wanaoogopa kuikataa CCM katika Tanzania hii siyo wa vijijini bali wa sehemu moja tu – Dar-es-Salaam.

Pole pole watapata ujasiri na kufunguka. Wakitambua kuwa kinachotisha ni rangi tu siyo kitu kingine. Nani anaogopa rangi ya kijani?

0
No votes yet