CCM, upinzani wana safari ndefu


John Kibaso's picture

Na John Kibaso - Imechapwa 13 October 2010

Printer-friendly version
Gumzo

CHAMA cha upinzani ni chachu katika kufichua maovu yote ndani ya serikali. Kwa mfano kama isingekuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) masuala ya wizi Benki Kuu (BoT), yasingejulikana.

Ni chama hicho ambacho kilikuwa cha kwanza kufichua wizi kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya BoT.

Ufisadi katika mkataba wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond na uidhinishwaji wa malipo kwa makampuni ya Meremeta, Deep Green Finance, vyote visingefichuliwa kama siyo kwa kiongozi wa CHADEMA. 

Katika hili, Dk. Willibrod Slaa, ambaye ni mgombea urais kupitia CHADEMA, anastahili pongezi kwa kazi nzuri aliyoifanya bungeni.

Lakini je, ameandaaje viongozi wake wa kuja kumsaidia? Au watakuwa wasaliti wa kununuliwa kama walivyonunuliwa baadhi ya wagombea wa chama chake na vyama vingine ili wawaachie nafasi wagombea wa CCM?

Hiki ndicho John Tendwa, Msajili wa Vyama vya Siasa amenukuliwa akisuta baadhi ya wapinzani kwa “wagombea wake kukubali kushawishiwa kupanga matokeo na wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliopita bila kupingwa katika baadhi ya majimbo.”

Ni jambo la msingi na muhimu wakati huu, kuchambua sifa za wagombea uongozi katika vyama vya upinzani.

Leo wapinzani wanaona udhaifu wa chama tawala kwa sababu tu wako nje ya mfumo; endapo watabahatika kushika dola, nao watachambuliwa kwa udhaifu kwani watakuwa chama tawala.

Wasomaji na wadau wengine wanaopenda mabadiliko (mimi binafsi ni mwana mageuzi, ningefarijika na kuwaomba), watambue kwamba mabadiliko hayo yatawagusa Watanzania wote bila kubagua aliyepiga kura na ambaye hakupiga kura.

Chama kinachoshinda kinarudi kuwa chama cha Watanzania wote. Inabidi watambue pia kwa kuchambua udhaifu wa vyama vya upinzani haina maana kwamba wakosoaji hawapendi mabadiliko. Kuna siku mabadiliko haya yatatokea, watu wapende wasipende.

Kimsingi, watu wakubali kwamba mfumo wa uchaguzi wa kidemokrasia ni kutofautiana kiitikadi, kifikra na kimtizamo, lakini siku ya mwisho wote watarudi kuungana mkono chini ya chama kilichoshinda kwani kitakuwa kinatekeleza sera zake.

Tatizo hapa ni kwamba baadhi ya wapigakura bado wana ushabiki wa mageuzi na mabadiliko ya kupata chama mbadala ya CCM kwa imani, mabadiliko hayo yatailetea nchi neema kubwa kwa muda mfupi.

Wengi hawana muda wa kuchambua udhaifu wala mapungufu ya vyama vya upinzani; kwao kikubwa ni kupatikana kwa chama mbadala tu. 

Watanzania wote wanasafiri kwenye boti moja ya utaifa. Kama wataguswa na uzalendo na kuweka mbele maslahi ya taifa, hakika watafanikiwa kuchagua chama bora na kiongozi bora. 

Chama tawala CCM nacho kinapaswa kusikia vilio vya wanachama wake. Kudharau maoni ya wanachama ni sawa na kujikaanga kwa mafuta yako mwenyewe.

Wanachama, wapenzi na wakereketwa wamesikika mara kadhaa wakitahadharisha viongozi wa juu wa CCM kumsaidia Rais Jakaya Kikwete ili aondoe kero ndani ya chama, matokeo yake baadhi yao wanampa takwimu zisizofaa.

Je, hawa ni kwa sababu wamelewa madaraka au wanajua wakimpotosha watampata mbadala wake?

Mwenyekiti wa CCM na katibu mkuu Yussuf Makamba (bila kuficha hisia zangu), hakika wamejitahidi kwa dhati kusafisha maovu ndani ya CCM, lakini viongozi au wanachama wanaowazunguka baadhi yao ni mamluki.

Umamluki huu unatokana na utaratibu wa kuwajaza viongozi kutoka upinzani kwenye nafasi nyeti na kuwasulubu wale ambao wamekaukiwa koo wakipigia debe chama kwa muda mrefu.

Haipendezi kuona mtu uliyeshindana naye kwenye jukwaa kutoka chama cha upinzani, huku akitoa matusi na kukashifu sera na ilani ya chama chako, baada ya uchaguzi kwisha anarudi na kukumbatiwa eti “mwana mpotevu amerudi kwa baba yake”.

Mwisho wa siku anakuwa bosi wa yule aliyevumilia mavundo ya maudhi yake, halafu anabaki kubeba mkoba wa mpinzani aliyehamia CCM na kupewa cheo. Hakika hii inauma sana.

Kwa hiyo, wakati vyama vya upinzani vikikosolewa, ni vyema chama tawala nacho kikajiweka katika mizani ya kujiangalia kwa hasi na chanya; la sivyo kuna siku kitakuja kujikuta hapatoshi. Nani atalaumiwa kwa usaliti huu?

Pengine ni vyema mwenyekiti wa CCM akashauriwa kuchukua hatua na kufanya mageuzi makubwa katika mfumo na muundo mzima wa chama endapo atapata ushindi katika kipindi hiki.

John Kibasso ni mbunge wa zamani wa Jimbo la Temeke kupitia CCM. Anapatikana kwa SIMU: 0767/0713 399004
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: