CCM usanii mtupu


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 17 February 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Mwenyekit wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) ni "usanii mtupu." Kelele za kupambana na ufisadi zimeishia kwenye ndoa na watuhumiwa wakubwa.

“Wamefunika kombe mwanaharamu apite; badala ya kufunua kombe ili mwanahalali asimame,” ameeleza mjumbe mmoja wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho mjini hapa.

Kilichotarajiwa katika vikao vya chama hicho vilivyoanza Jumamosi iliyopita, ni watuhumiwa ama kuondolewa katika chama au kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Lakini kilichofanyika ni kuweka kando tuhuma za aina zote za ufisadi zinazokabili baadhi ya viongozi ndani ya NEC na wote kuonekana kama kwamba hakukuwepo tuhuma wala msutano.

Hali hii ya “muwafaka” na watuhumiwa wa ufisadi ilianza kuonekana Alhamisi iliyopita pale Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ilipojinyenyekeza kwa serikali.

Kamati, kana kwamba kulikuwa na shinikizo, ilikubali karibu majibu yote ya serikali juu ya utekelezaji wa maazimio 23 ya bunge kuhusu mkataba kati ya serikali na kampuni feki ya Richmond.

Ni kashfa ya Richmond iliyomng’oa aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa na mawaziri wawili wa wizara ya nishati na madini, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi.

Mwingine ambaye amekuwa akihusishwa na kashfa ya Richmond na ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kutumia kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, ni Rostam Aziz, mbunge wa Igunga.

Rostam amekuwa akitajwa mara kadhaa kuwa mmiliki wa Kagoda ambayo ilichota zaidi ya Sh. 40 bilioni; kughushi nyaraka na kumhusisha rais mstaafu, Benjamin Mkapa kuwa ndiye aliyeruhusu ukwapuaji kufanyika.

“Sasa huwezi kuamini kuwa kulikuwa na mvutano kati ya watuhumiwa wa ufisadi na wabunge waliokuwa wamejipambanua kama makamanda dhidi ya ufisadi. Ghafla wote wakawa kama wamepigwa pasi,” ameeleza mjumbe huyo wa NEC.

Habari za ndani ya vikao zimeeleza kuwa aliyepigilia msumari wa mwisho kwenye uhasama uliokuwa umejengeka ni mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.

Imeelezwa kuwa Rais Kikwete, baada ya baadhi ya wajumbe kuonyesha kung’aka, wakitaka watuhumiwa wafukuzwe kwenye chama, alilalia upande wa Kamati ya Mwinyi na kusema ilihitaji muda zaidi kumalizia kazi yake.

CCM iliunda Septemba mwaka jana kamati ya viongozi watatu kuchunguza kiini cha mvutano ndani ya bunge na kati ya bunge na serikali, na ndani ya baraza la wawakilishi. Mwenyekiti wake alikuwa Ali Hassan Mwinyi.

Ilikuwa baada ya taarifa ya Kamati kujadiliwa ndani ya Kamati Kuu na baadaye kuwekwa wazi ndani ya NEC, baadhi ya wajumbe walipendekeza watuhumiwa wa ufisadi wafukuzwe kwenye chama.

Watuhumiwa hao ni pamoja na aliyekuwa waziri wa miundombinu, Andrew Chenge anayehusishwa na mlungula kwenye ununuzi wa rada na ambaye alikuwa na zaidi ya Sh. 1 bilioni katika akaunti ya benki nchini Uingereza.

Aidha, kuna taarifa kwamba mbunge wa Ukonga, Makongoro Mahanga alisimama kikaoni na kutaka NEC imsafishe Lowassa kwa madai kuwa “alituhumiwa bila kusikilizwa.”

Makongoro alinukuliwa akisema kitendo kilichompata Lowassa kinafanana na kile kilichowahi kumkuta rais mstaafu Mwinyi ambaye alijiuzulu kwa makosa ya wengine.

Hata hivyo, hoja ya Makongoro ilijibiwa papo hapo na Mwinyi mwenyewe aliyenukuliwa akisema, “…lakini mimi sikusafishwa,” kauli ambayo ilisababisha baadhi ya wajumbe waangue kicheko na kuzima kabisa mpango wa Lowassa na wapambe wake kutaka asafishwe.

Taarifa zinasema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Bernard Membe na John Chiligati walikuwa miongoni mwa wajumbe wa NEC waliotaka Chenge achukuliwe hatua kwa kilichoitwa “kuaibisha chama chao” kwa kuhusishwa na kashfa ya rada.

NEC iliambiwa na Kamati ya Mwinyi kuwa ilikuwa haijakamilisha kazi yake na hivyo ilihitaji muda zaidi. Taarifa za baadaye juzi zilisema iliongezewa miezi miwili.

Mjumbe wa NEC ambaye hakutaka jina lake litajwe ameiambia MwanaHALISI kuwa alikuwa na maoni tofauti kuhusu kamati hiyo kuongezewa muda.

kwa maoni yake, alisema, kamati ya Mwinyi haina kazi nyingine ya kufanya isipokuwa “hiyo ni njia ya kupoteza muda tu” ili kuonekana kamati inashughulikia mapatano ya makundi.

“Ukiangalia kwa makini utaona kuwa hakuna muda zaidi wa kujadili masuala haya. Kuanzia Aprili chama kitakuwa katika pilikapilika za uchaguzi. Hapa ndipo kinafunga mjadala wa ufisadi. Tutakutana majimboni,” ameeleza.

Wachunguzi wa mambo ya siasa wanasema “muwafaka” na watuhumiwa wa ufisadi umeonyesha sura halisi ya CCM na mwelekeo wake katika siku za usoni.

“Kwa hatua hii, watuhumiwa wamepata mahali pa kupumulia. Watapata nguvu zaidi na kujiimarisha. Hapa ndipo watawashughulikia wale wanaowachukulia kuwa ni maadui zao,” wameeleza.

Kumekuwa na madai kuwa Spika wa Bunge Samwel Sitta amekuwa akitumia “kivuli cha kupambana na ufisadi” ili kumuangamiza Lowassa kisiasa.

Pamoja na spika, walikuwa Dk. Harisson Mwakyembe, Anne Kilango Malecela, Fred Mpendazoe, William Shelukindo, Lucas Selelii, Christopher Sendeka, James Lembeli, Aloyce Kimaro, Injinia Stella Manyanya ambao sasa wamenywea.

Habari zisizorasmi zinasema wabunge hao wanaweza kuwa wameamua kuachana na malumbano ya wazi ili kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Katika hatua nyingine, NEC imekubali maridhiano kati ya Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad lakini kwa masharti magumu yanayoweza kuleta sura mpya ya maridhiano hayo.

“NEC imekubali maridhinao hayo lakini wamesema maazimio ya Butiama ndiyo yazingatiwe na utekelezaji wake utakuwa ni kura za wananchi wa Zanzibar. Kazi ya kutafuta maoni kwa mujibu wa kikao ni baada ya uchaguzi mkuu,” kilieleza chanzo chetu.

“Baada ya uchaguzi serikali itaundwa. Kazi ya kwanza ya serikali hiyo itakuwa ni kuendesha kura ya maoni ya wananchi juu ya serikali hiyo ya kitaifa, baada ya hapo ndio mabadiliko yatafanywa kwenye serikali,” ameeleza.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: