CCM waanza kutoana macho


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 18 March 2009

Printer-friendly versionSend to friend
Uchambuzi
Makala, Murad hapakaliki
Mweka Hazina wa CCM, Amos Makala

MIEZI 18 kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010, tayari Suleiman Saddiq Murad, mbunge wa sasa wa Mvomero mkoani Morogoro, na Mweka Hazina wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Amos Makala, wameanza kutoana macho.

MwanaHALISI limekuwa wilayani Mvomero kwa wiki nzima na limewanukuu baadhi ya viongozi na wananchi walioshuhudia malumbano na madai ya wawili hao ambayo wameita ya “kupakaziana.”

Murad anadaiwa kumtuhumu Makala kupeleka misaada jimboni ili kujinyakulia umaarufu na kujenga ngome kwa ajili ya uchaguzi ujao.

Taarifa zinaeleza kuwa ingawa kuna wadau wengi wanaochangia maendeleo, mbunge huyo ametokea kumlalamikia Makala kwamba “Kasi yake ya utoaji misaada imekuwa kubwa, hali inayomtia shaka pengine anafanya kampeni za kutaka kuwania jimbo hilo.”

Murad na Makala walishindana kwenye kura za maoni za CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa 2005. Murad alimshinda Makala kwa “kura chache.”

Jitihada za kutaka maelezo ya Murad hazikufanikiwa kumpata. Amekuwa akipigiwa simu hazipokelewi. Simu Na. 0784 424270 na nyingine Na. 0773 786100 zikipigwa zinaita na mwishowe kujibu “Simu unayopiga haipokelewi.”

Hata alipotumiwa ujumbe mfupi kupitia namba hizo uliosema, “Mh. Salaam. Tafadhali tunaomba upokee simu. Hapa ni gazeti la MwanaHALISI,” haukujibiwa ingawa ulionyesha umepokewa.

Murad, aliyeanza kuwa mbunge mwaka 1997 kwa uchaguzi mdogo baada ya kifo cha Nicas Mahinda wa Morogoro Vijijini, amenukuliwa akilalamika kuwa Makala anatumia wadhifa wake katika CCM na anachota fedha za chama hicho Makao Makuu kwa madai ya kufanyia “shughuli za maendeleo katika jimbo.”

Hata hivyo, kabla mwangwi wa kauli hiyo kupotea, Katibu Mkuu wa CCM, Yusufu Makamba, alisema wiki iliyopita fedha za chama ziko salama na Makala anazitunza vema.

“Si kweli kwamba Makala anachukua fedha za chama,” alisema Makamba na kung’aka kama Makala angetumia fedha za chama, angefikishwa mahakamani.

“Na kama Saddiq (Murad) haridhiki ni vema akapeleka malalamiko yake Tume ya Maadili ili kuhakiki jalada la Makala,” amesema Makamba.

Katibu wa CCM Wilaya ya Mvomero, Fikirini Masokola, ameiambia MwanaHALISI kuwa hajawahi kulalamikiwa na Murad kuhusu mwenendo wa Makala jimboni Movemero, lakini akashangazwa kuona mambo hayo yamevuka mikapa hadi ngazi ya taifa.

 “Nashangazwa kusikia CCM taifa inatolea ufafanuzi mambo haya. Mimi sijawahi kulalamikiwa na mbunge,” anasema na pia akishtushwa na mambo hayo kujadiliwa kwenye vyombo vya habari.

“Nimekuwa na Murad katika vikao vya Sekretarieti ya Wilaya, Kamati ya Siasa na Halmashauri ya Wilaya. Lakini hajawahi kuniambia au kulalamika. Ninachokiona ni kama uvunjaji wa kanuni,” anasema Masokola.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mtibwa, Paul Kiumbi anasema, “Misaada tunayopata tunaiomba sisi wenyewe.”

Kiumbi anasema nguvu za wananchi ndiyo tegemeo lao la kwanza. Pili, ni serikali na tatu ni wadau ambao waliwaomba kwa barua.

Miongoni mwa wadau ni mfanyabiashara na Mkurugenzi wa Kiwanda cha Miwa cha Mtibwa, Nassoro Seif, Benki ya Micro-finance (NMB), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mbunge na Makala.

“Kwanza tulimtoza kila mtu mzima Sh. 3,000 na Nassoro Seif alikubali kujenga vyumba vinne vya madarasa; NMB walitoa Sh. 2 milioni; Makala, pamoja na misaada mingine, alitoa mifuko 200 ya saruji na mabati 150,” anaeleza Kiumbi.

Anasema TRA na mbunge Murad hawajatoa michango kufuatia ombi la jimbo. Taarifa nyingine zimeeleza kuwa Murad akifuatwa anajibu, “Endeleeni kunikumbusha.”

Kiumbi anasema kama siyo kwa msaada wa saruji aliotoa Makala, kusingekuwa na madarasa, hivyo wanafunzi wote waliochaguliwa Kidato cha Kwanza, wasingekwenda shule, kwani wilaya ilikuwa imechelewa kupata fedha za serikali.

“Ni misaada kama hii ya Makala imetuokoa. Tunatambua kazi hii, tunamshukuru na tunakiri hajawahi kudokeza kwamba anafanya hivyo kwa kuwa anataka ubunge,” anaeleza Kiumbi.

Kiumbi anasema, “Hatukuwahi kuomba mara moja na kusaidiwa papo kwa hapo. Makala hatusaidii mara moja tu, anachosema ni kwamba yeye ana marafiki zake. Akiombwa msaada na kufanikiwa, naye anasaidia wengine kama sisi.”

“Hata siku moja hakusema kwamba anataka kuwa mbunge au kugombea nafasi yoyote hapa. Labda kwa kuwa wakati haujafika, lakini sisi hajatuambia. Jambo kubwa mbele yetu ni maendeleo,” anaeleza Kiumbi kwa tabasamu.

Jumaa Issa Seif, Katibu Kata CCM, Mtibwa anasema, “Tuna matatizo mengi hivyo tunakimbilia huku na kule. Tunalazimika kuomba ili kuwezesha kujiletea maendeleo. Lakini inaonekana Saddiq (Murad) ana woga; hajiamini na anakimbia kivuli chake.”

Seif anasema wakati Makala anakabidhi misaada yake, uongozi wa wilaya na Murad walikuwepo. Naye Murad aliahidi kutoa milango ya nyumba ya mwalimu. Lakini hadi leo hajatoa.

“Ukimuuliza anasema mbona hamnikumbushi. Na kuna wakati anakuwa mkali, hataki kukumbushwa lakini Makala, Benki ya NMB na Nassoro Seif ndio wamejitokeza kusaidia.”

Hata Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mvomero, Alfred Ng’atibwa Kikombe, ambaye pia ni Diwani wa Kikeo, anamshukuru Makala kwa kutoa msaada wa saruji na mabati kwa kata anayoongoza.

“Alitukabidhi mbele ya viongozi. Hakutoa kwa mtu mmoja tu na hata mbunge alikuwepo kwenye makabidhiano hayo,” anaeleza.

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Hawa Ng’humbi amesema kwa kuwa wilaya aliyomo ni mpya na bado haina mapato, amekuwa akikusanya nguvu mbalimbali katika kusaka misaada ya maendeleo.

“Kwenye elimu ninathibitisha kweli tumeomba watu mbalimbali akiwamo Makala. Tunafanya hivyo kwa kila shughuli ya maendeleo. Kwa mfano, katika ujenzi wa kituo cha polisi Dakawa, ambacho ni kikubwa, tunahitaji nguvu ya serikali, wadau na halmashauri.

Ametoa mifano kuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ametoa mifuko 100 ya saruji na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ametoa Sh. 2.1 milioni.

Ng’humbi amekiri Makala kutoa msaada wa saruji na mabati na kwamba umesaidia katika ujenzi wa madarasa yanayohitajika kwa ajili ya wanafunzi waliofuzu kuingia Kidato cha Kwanza.

Anauliza: “Sasa ikitokea ukamwomba mtu na kwa hiari yake akakusaidia, kuna haja tena ya kuhoji anakotoa fedha?”

Alisema ushirikiano mzuri wa viongozi wa ngazi mbalimbali wilayani umeanza kuzaa matunda kwani Mvomero imeibukia kwenye nafasi ya tatu kwa mkoa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba.

Sheikh wa Wilaya ya Mvomero, Hassan Mamboleo, anakiri kupewa msaada na Makala, akisema ni baada ya kuhaha kutafuta kwingineko bila mafanikio. Anathibitisha kuwa misaada hiyo ilitumika kukarabati misikiti.

“Sasa sisi tunasema kwamba, anayepinga Waislamu kusaidiwa bila shaka anajenga dhana ya udini na anapinga moja kwa moja uislamu. Huyo sisi tunamhesabu kama mtu wa fitina,” anasema Sheikh Mamboleo.

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Jimbo la Mtibwa, Boniface Mgalula, anasema hatasahau kitendo cha Makala cha kuhudhuria harambee ya ujenzi wa ofisi ya jimbo na kuchangia kama walivyochangia waumini wengine.

“Makala asiogope, aendelee na moyo wake wa kusaidia jamii; watu wana mahitaji mengi na makubwa; akiitwa aitike maana watu ndio wanaohitaji kusaidiwa na si kwa malengo ambayo wengine wanahisi na kuandika magazetini,” ameeleza Mchungaji Mgalula.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: