CCM wamepanda farasi kiwete


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 08 September 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi

HOJA za uchaguzi mkuu nchini zimewekwa kando. Mahusiano ya kifamilia ya mpinzani mkuu ndio yamewekwa mbele. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinashangilia kupanda farasi kiwete ambaye hatainuka.

Katika wiki moja hadi jana asilimia 72.3 ya maudhui ya siasa katika matoleo ya magazeti yote yaliyosambazwa, yamelenga Dk. Willibrod Slaa, mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mchumba wake, rafiki yake na makandokando yake.

Kitaaluma, hakuna ubaya wa kutoa taarifa zote na kamili juu ya anayetafuta uongozi kisiasa. Tatizo litaonekana tu pale zana zote zitakapoelekezwa wakati mmoja, kwa mtu mmoja, mgombea mmoja, familia moja, chama kimoja cha Demokrasia na Maendeleo, tena katika ladha ya ukakasi.

Hapo utoaji wa taarifa au habari utakuwa umechukua sura na tabia ya “mashambulizi.” Hautoi taarifa tu au uchambuzi juu ya kilichopo na kinachoendelea, bali unakuza, kushamirisha na kusherehesha mahusiano.

Kama vyombo vyote vya habari vingeingia uwanjani na vingine kuchukua upande wa pili, hata uchaguzi mkuu mwaka huu usingekuwa na maana yoyote.

Kwani waliolishwa taarifa za mahusiano ya kifamilia peke yake au kwa wingi na kwa muda mrefu; au waliomwagiwa upupu wa tuhuma za kufanya ngono, kuoa mapema, kupora wake na kufumaniana; wangekuwa wanakwenda vituoni kuchagua nini siku ya 31 Oktoba mwaka huu?

Fikiria kama upande mwingine ungetoka na picha za wagombea urais, wake zao, wapenzi wao, vimada vyao na hata wale ambao hawakuwa wapenzi lakini walilazimisha kufanya nao ngono za chapuchapu, tena ndani ya ofisi za vyama vya siasa au serikali!

Angalia orodha ndefu ya wanawake wanaobubujikwa machozi yasiyokauka; waathirika wa uchu wa viongozi wanaume, waliowabaka ili waweze kuwaruhusu kugombea “uongozi” ndani ya vyama vyao. Ni vema mashambulizi hayajawa ya pande mbili.

Taarifa au habari za aina hii; zilizoendelezwa kwa kipindi kirefu kwa kurudiwarudiwa, kukuzwa na kupewa upekee wa aina yake, huwa na athari kubwa kwa jamii na hasa kwa shughuli kuu inayoandaliwa, inayotekelezwa au inayotarajiwa.

Hili la kung’ang’ania mahusiano ya kifamilia ya Dk. Slaa; kwa msisitizo, muda mrefu na kwa njia ya kukandia, tena wakati huu kuelekea uchaguzi mkuu, linaweza kuwa limetokana na sababu zifuatazo:

Kwanza, kumdhoofisha kisaikolojia na kumnyong’onyeza mapema. Kumfanya awe na kigugumizi na kupoteza ujasiri wake na kauli pevu juu ya masuala ya kijamii anayosimamia.

Pili, kumpokonya muda. Kwamba achukue muda wake mwingi kufikiria na kupanga jinsi ya kupambana na kile ambacho tayari kimeitwa “kashfa” na akose fursa ya kujiimarisha kwa uchunguzi na uchambuzi ambavyo tayari vimekuwa mwiba mkuu kwa CCM.

Tatu, kumwanika mbele ya umma kama mtu “mbaya” kuliko wengine wote, ambaye wananchi hawastahili kumsikiliza, kumwamini na kumchagua – ingawa kwa hadithi ya Biblia, hakuna “aliye safi” miongoni mwa wagombea wa kuweza kuwa wa kwanza kumtupia jiwe.

Nne, kumnyamazisha, hasa baada ya kutangaza kuwa ana “mabomu 20” anayotaka kuyatumia kulipua CCM, kati ya sasa na Oktoba. Hili limelenga asiaminike.

Tano, kuondosha hoja kuu za uchaguzi mwaka huu na kuziweka pembeni. Hii ni kwa kuwa tayari zimemvuruga mgombea wa CCM na chama chake na kumfanya ageuze kampeni nzima kuwa ya ahadi, badala ya kuonyesha na kujivunia alichofanya, kama kipo.

Sita, kuhamisha mawazo ya wananchi kutoka hoja kuu za wakati huu – ujinga, umasikini, elimu duni, ukosefu wa ajira, ujira kiduchu na njaa ya mwaka hadi mwaka katika nchi iliyojaa mito, maziwa na mvua za kuaminika.

Saba, kupotosha mkondo wa mashambulizi kwa serikali kutokana na viongozi wake kutokuwa makini, kutowajibika, kutotimiza ahadi, kutelekeza wafanyakazi, wastaafu na wakulima.

Nane, kuvunja nguvu za wimbi kuu la kukosoa serikali kutokana na kuzama katika rushwa, wizi na ufisadi na kuwa na matumizi mengi na makubwa yasiyo ya manufaa kwa umma.

Tisa, kuwapa viongozi wa CCM na vyama vingine vichovu, nafasi ya kupumua baada ya kuhenyeshwa mkuku kwa hoja muwafaka za kuleta mabadiliko katika kipindi kifupi tangu kampeni zianze.

Kumi, kuua sauti kuu ya upinzani kwa sasa, ambayo imebadili mkondo wa siasa na kwa mara ya kwanza, kufanya CCM kulialia, kuishi kwa kujihami na kulazimika kujibu hoja.

Kumi na moja, kuziba nafasi ya kujadili tabia na mienendo ya wagombea urais wa vyama vingine, hasa CCM.

Lakini nani angependa, wakati huu, kusikia kwa kina na kwa kipindi kirefu kwa mfano, simulizi juu ya Jakaya Kikwete na mke au wake zake; au malumbano kati ya mke mdogo na mkubwa; nyumba ndogo na ahadi za pembeni, kama zipo?

Katikati ya tuhuma za ukwapuaji mabilioni ya shilingi kutoka Hazina na Benki Kuu kwa kutumia makampuni ya kitapeli kama Kagoda Agriculture Limited, nani anategemea wananchi wawe na hamu kubwa ya kusikia uvumi kuwa rais wao ameishiwa nguvu tena na kudondoka mikutanoni huko Sengerema na Mbeya?

Hii haina maana kuwa hayo hayastahili kufahamika; bali vipaumbele vya wakati uliopo vinalazimu hayo yatajwe na kuachwa ili akili na nguvu za wananchi na vyombo vya habari, vielekezwe katika kupigania uhuru, haki na ustawi wa jamii zao na mustakabali wa taifa.

Lakini mkuki kwa nguruwe, kwa binadamu ni mchungu. Mapema mwaka huu mhariri na mwandishi wa MwanaHALISI waliitwa mara tatu kwa Msajili wa Magazeti (MAELEZO) kuhojiwa kwa nini wanaandika makala “juu ya Salma Kikwete,” mke wa rais.

Haifahamiki iwapo rais anajua malalamiko hayo, kwani makala zenyewe hazikuwa zinachimba usichana, umama au biashara za mke wa rais. Zilikuwa zikijadili nafasi ya mke wa rais (yeyote yule kwa mifano ya Marekani, Zimbabwe, Kenya na Tanzania) katika mustakbali wa taifa.

Bali MAELEZO waliamuru makala zisitishwe kwa madai kuwa “mama amelalamika.” Je, leo Dk. Slaa hajalalamika?

Ukiyavulia sharti uyaoge. Dk. Slaa au mwasiasa mwenye hoja kuu hana sababu, kwa sasa, ya kuzunguka nchi nzima akijibu tuhuma juu yaliyotokea faragha na kwa utashi binafsi wa wawili.

Hasa wapeperushaji wa tuhuma wanapokuwa watuhumiwa wakuu kwa kutopea katika wizi, ufisadi, matumizi mabaya ya kodi za wananchi, kutokuwa makini, kutowajibika na kushindwa kujenga mazingira ya kuleta mabadiliko yaliyotarajiwa.

Uchaguzi huu una ushindani mgumu hasa wapinzani wanaposema na kudhihirisha kuwa hawadanganyiki. Na hiyo ndiyo kauli ya CHADEMA na Dk. Willibrod Slaa.

Na tayari wananchi wameamua wanataka ubongo wa Dk. Slaa na sio sehemu zake za nyeti.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: