CCM wamevua gamba, wameacha sumu


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 20 April 2011

Printer-friendly version

UNAFIKI haujengi. Migogoro mingi serikalini, vyama vya siasa, vya kiraia na mitaani husababishwa na unafiki. Hili ndio moja ya magamba yanayokitesa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mathalani, Samuel Sitta, akiwa Spika wa Bunge alionekana nuksi ndani ya chama, lakini leo kinatekeleza aliyosimamia kupinga ufisadi katika Bunge la Tisa.

  Sitta alinuniwa na baadhi ya wanachama wa CCM akidaiwa kuwa kiini cha mpasuko ndani ya chama. Eti uendeshaji wake wa bunge ulioruhusu mijadala mikali ‘iliyowakaanga’ vipenzi vyao uliigusa serikali na CCM.

Watetezi wa ufisadi walipendekeza Sitta apokonywe kadi ya CCM. Wabunge waliojipambanua na kupinga ufisadi walichukiwa na kusakamwa na waliovaa gamba la ufisadi. Chama kikakosa msimamo; watuhumiwa wakapata pepo.

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akatekwa; akaasisi kupitia serikali ‘funika funika’ ufisadi. Kwanza bungeni ambako walitetea hatua ya Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi kubeba mkataba wa madini kwenda kutia saini hotelini usiku mjini London, Uingereza.

Pia wakatetea hatua ya kampuni ya Richmond kupewa zabuni ya kufua umeme wa dharura licha ya kushika nafasi ya mwisho mara tatu katika ushindani wa zabuni, ili kuwanasua watuhumiwa wakuu – waziri mkuu, Edward Lowassa aliyelazimika kujiuzulu, na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Halafu wakatetea kitendo cha Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge kuweka kwenye benki ya nje, kile alichoita “vijisenti,” vilivyohusishwa na rushwa ya rada iliyonunuliwa kifisadi na serikali. Ni kashfa hiyo iliyomlazimu naye kujiuzulu uwaziri.

Pili, Rais Kikwete akatuma mawaziri na makada wa CCM nchi nzima kutetea ufisadi. Lakini haikusaidia, serikali yake ikavunjika mapema Februari 2008.

Kilichoisibu serikali yake ni ripoti ya uchunguzi wa kina wa kamati teule ya Bunge chini ya Mwenyekiti Dk. Harrison Mwakyembe iliyoonyesha ‘dili’ la Richmond lilipatikana kifisadi na kwa hiyo Lowassa, bila ya shaka baada ya kubanwa sana, akalazimika kung’atuka.

Hadi anajiuzulu, serikali ilikuwa imerithisha mkataba huo wa kufua umeme kwa kampuni nyingine ya Dowans ambayo rais amepigia debe ilipwe mabilioni ya shilingi.

Kikwete akaunda upya serikali na kumteua Mizengo Pinda kumrithi Lowassa. Lakini akajitosa kufunika tukio hilo kwa kudai yaliyompata Lowassa ilikuwa “ajali ya kisiasa.”

Kama ufisadi ni ajali ya kisiasa, basi wote akiwemo Rais Kikwete walikumbwa na ajali hiyo Septemba 15, 2007 pale Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa alipotangaza orodha ya mafisadi 11 kwenye viwanja vya Mwembe-Yanga, Temeke, mkoani Dar es Salaam yakiwemo ‘magamba matatu ya CCM’.

Kisha Kikwete akanaswa ‘laivu’ kwenye ‘rada’ ya ufisadi. Katika kampeni za urais mwaka 2010, alipita majimbo yote kuomba kura na kunadi wagombea wa CCM. Akathubutu kusifu hata ‘magamba’.

Siku ya kufunga kampeni viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, alisema, “…Sasa walitaka nisiwapigie kampeni ili wapinzani washinde?”

Mwanzoni mwa mwaka huu akaingiwa hofu ya chama kumfia. Februari 5, 2011 wakati wa sherehe za miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM, akatangaza azma ya chama kijivua gamba.

Aprili 9, 10 na 11 akaongoza vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) kuvua gamba.  Akavunja sekretarieti iliyokuwa chini ya uongozi wa Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, ili kuwatosa Rostam, Chenge na Lowassa. Unafiki!

Hao si ndio walipewa kinga wakimwona Sitta, ambaye ni Waziri wa Afrika Mashariki kuwa ndio nuksi?

Unafiki.

Desemba 2010, Sitta aliwasilisha jina lake ili lipitishwe na kupata fursa ya kutetea kiti chake cha uspika bungeni, lakini akawekewa vigingi viwili. Kwanza CCM wakapokea jina la Chenge, lakini pili wakaongeza sharti gumu la kuwa safari hii chama kinataka spika mwanamke.

Akateuliwa Anne Makinda, naibu wake kwa miaka yote.

Nini kimetokea hadi watu wenye nguvu ndani ya CC na NEC – Rostam, Chenge na Lowassa – wapoteze kinga? CCM wamegundua lini kuwa makada hao ni gamba? Je, ufisadi wao ni nini? Umeliathiri vipi taifa kiuchumi? Sasa watachukua hatua gani za kisheria dhidi yao?

Katika kipindi hicho chote, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Robert Manumba alifumbia macho tuhuma za ufisadi dhidi ya makada hao.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hoseah alipulizia pafyumu kuhusu tuhuma hizo. Kwanza alidai hakuona harufu ya rushwa wakati wa mchakato wa kampuni ya Richmond kupewa zabuni ya kufua umeme nchini.

Pili alijiumbua aliposoma taarifa eti Chenge alisafishwa tuhuma zilizokuwa zinamkabili na Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO). Ubalozi wa Uingereza nchini ulipinga madai ya Dk. Hoseah ndipo Chenge akatoka mwenyewe.

Kama vyombo vya serikali vilikataa kuwepo kwa ufisadi, Rais Kikwete amepata wapi orodha hii aliyoitangazia vita kwenye vikao vya CC na NEC?

Je, ni utaratibu wake uleule, kama alivyofanya kuhusu uraia wa Hussein Bashe aliyenuia kugombea ubunge jimbo la Nzega, kuacha kupeleka tuhuma nzito kwenye vyombo vya dola badala yake kupeleka CCM na NEC ambako hakuhusiki? Au naye hawaamini Manumba na Dk. Hoseah?

Kwanini Rais aamini ripoti ya siri ya Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St. John Dodoma, Prof. Eginald Mihanjo badala ya vyombo vya dola? Ni profesa Mihanjo au taasisi za dola ndizo zipo kisheria kushughulikia ufisadi?

Kama Rais anaweza kutumia vyombo vingine kupata ukweli, Manumba na Dk. Hoseah ambaye alipaswa awe ameadhibiwa mwaka 2008 kwa tukio la Richmond, wanasubiri nini ofisini?

Katika hili, Rais Kikwete amethibitisha madai ya Dk. Hoseah aliyokaririwa kwenye mtandao wa WikiLeaks kwamba kiongozi huyo mkuu wa nchi ndiye kikwazo cha watuhumiwa wenye majina makubwa kuchunguzwa na kufikishwa kortini.

  Baada ya CCM kubaini mafisadi sasa wakabidhi orodha hiyo kwa vyombo vya dola ili taratibu za kisheria zichukue mkondo wake – uchunguzwe ufisadi wao na hasara waliyosababisha, warejeshe mabilioni ya shilingi waliyofisidi kisha washitakiwe mahakamani.

Pia kama CCM wanakiri Lowassa ni gamba na kwa kiasi kikubwa tuhuma zake zimejikita katika mradi wa Richmond, serikali itakuwa inaendeleza ufisadi kwa kumlipa mshahara mtu ambaye anapaswa kufukuzwa kazi na kushitakiwa.

Kikwete abatilishe barua ya Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu, ampe barua ya kusitishiwa mamilioni ya shilingi anayolipwa kama waziri mkuu mstaafu na arejeshe zile fedha alizolipwa.

  Tatizo la nyoka si gamba ila sumu yake, ndiyo maana vikundi vya sanaa hung’oa meno na siyo kuvua gamba. CCM haijang’oa meno ya sumu ya ufisadi ndiyo maana wanasema wamevua gamba kuukuu na kuvaa gamba jipya. Bado gamba la ufisadi limewaganda. Hawaponi.

0753 626 751
0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: