CCM wanahitaji maridhiano, hakuna aliye msafi ndani yao


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 30 November 2011

Printer-friendly version

KUMEKUWA na juhudi za kueleza mparaganyiko ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuibua dhana za kutaka kuvisha nguo udhaifu wa kimfumo na uwajibikaji wa viongozi kwa muda mrefu sasa.

Nitaeleza. Baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangazwa kuwa mgombea urais kupitia CCM mwaka 2005, ndipo alibainisha kuwa alikuwa na kitu kinaitwa MTANDAO.

Akiwa amewabwaga makada wenzake wawili, Dk. Salim Ahmed Salim na Prof Mark Mwandosya, Kikwete aliwashukuru aliowaita wanamtandao.

Mtandao huu ndio ulijipa jukumu la kumbeba Kikwete kwa gharama zozote hadi aingie ikulu iwe kwa njia za haki au hila.

Nilipata fursa ya kukutana na kiongozi mmoja wa mtandao mwishoni mwaka 2004, alinieleza jambo lililonishitua. Alieleza kwa nini Kikwete pekee alistahili kuwa mgombea urais wa CCM na kwa nini ilikuwa muhimu vyombo vya habari, hasa waandishi wa habari wenye heshima nchini wakati huo, kuwa nyuma yake.

Nilipomuuliza pamoja na wao kujiamini sana , walikuwa na fikra gani kama Kikwete asingepitishwa na chama, alijibu: “Hatuwazi kushindwa na hatutaki kuwaza kushindwa.”

Na kweli kama ilivyokuwa imeelezwa, JK ndani ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM siyo tu aliwabwaga wenzake kwa kishindo mwaka 2005, bali kimbunga hicho kilitokea tena kwenye Mkutano Mkuu, ambako kura hazikupigwa mara mbili kama ilivyokuwa mwaka 1995 alipopambanishwa na Benjamin Mkapa na Cleopa Msuya.

Baada ya kuingia madarakani JK na awamu yake ya nne, hakuna ubishi walikuwa wameumiza watu wengi. Hawa ni wale ambao hawakuwa wanamtandao, waliumizwa kwa kuzushiwa, kwa kuhujumiwa na kila mbinu mbaya ili kuwaondoa kwenye mstari wa kisiasa wa kuwa wagombea. Huu ulikuwa  mpambano nilioufananisha na vita.

Waziri Mkuu wa awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, akilalamika hadharani juu ya kuhujumiwa kwake alisema, wale wanaotumia magazeti kuingia madarakani, wakishinda watatumia risasi kusalia madaralani.

Hakufafanua wala kutaja jina la mtu, mbali ya kusema vyombo vya habari vilikuwa vimetumika vibaya kunyanyua baadhi ya watu na kuangamiza wengine kwa nia ya kujijenga au kuangamizana kisiasa.

Kwa  bahati mbaya zaidi, wanamtandao nao kila mmoja alikuwa na matarajio yake. Wapo waliokuwa wameahidiwa nafasi, wapo waliotumia rasilimali zao nyingi wakitarajia kuja kulipwa fadhila. Wengi ahadi kwao hazikutimia, kilichofuata ni kuzaliwa makundi ndani ya mtandao, yanayotafunana kwa mtindo ule ule wa kuingia kwao madarakani.

Makundi haya yalizidi mno kiasi cha kuwa tishio kwa CCM, ndiyo maana miaka miwili hivi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana,  iliundwa kamati ya watu watatu, iliyoongozwa na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwingi na Pius Msekwa pamoja na Abdurahaman Kinana kwa nia ya kusaka suluhu ya makundi ndani ya wana CCM.

Wengi walikuwa wabunge waliokuwa wanahasimiana kwa kiwango cha kuhatarisha uhai wa chama. Hapana shaka, uhasama huo ndio umeifikisha CCM ilipo leo.

Dhana ya makundi yanayohasimiana ilivyochukuliwa na kutafutiwa ufumbuzi, tangu siku ya kwanza ilikosa uhalali kwa sababu haikujielekeza kwenye chanzo cha mgogoro ambao ni makubaliano na ahadi kedekede kwa wanamtandao kwa upande mmoja, lakini kwa upande wa pili majeruhi wa nje ya mtandao.

Kwa mfano, inazungumzwa kwamba ndani ya mtandao wapo watu wawili waliokuwa wameahidiwa uwaziri mkuu; dward Lowassa na Samuel Sitta. Kila mmoja aliaminishwa ndiye waziri mkuu. Yaliyotokea ni  wazi, Lowassa aliteuliwa na Sitta akatulizwa kwa uspika.

Kwa hiyo, kazi ya kwanza ya Sitta na Lowassa ilikuwa kuonyeshana nani zaidi – Sitta kama kiongozi wa Bunge na Lowassa kama mkuu wa shughuli za serikali bungeni. Mpambano huu unajulikana ulivyomalizika, Februari 7, 2008 kwa Lowassa kujiuzulu.

Siku baada ya siku ni siasa za makundi, ni kutuhumiana na kushughulikiana ama kupitia kwenye vyombo vya habari, au hata ndani ya vikao vya chama.

Ugomvi huu ndani ya CCM ambao kwa kiwango kikubwa chimbuko lake ni mbio za urais tangu mwaka 1995 baada ya Rais Mkapa kuingia ikulu, umejithibitisha kuwa wa kijinga, wakati mwingine wenye matinki.

Kibaya zaidi wakati wote uongozi wa juu wa CCM ulikosa njia sahihi ya kushughulikia au hata unaposhughulikiwa unatazamwa kwa macho ya makengeza. Udhaifu huu umekuwa ajenda isiyoisha ndani ya  CCM. Vita ya makundi.

Dhana ya kujivua gamba ni juhudi za kutaka kumaliza ugomvi na vita ya makundi lakini bila kujielekeza kwenye chimbuko la vita hii ambayo kwangu mimi ni mtandao.

Aprili 10-11, mwaka huu NEC ya CCM ilikutana Dodoma na kutoka na maazimio 27 ya kufanya mageuzi, miongoni mwake lipo linalosomeka hivi:

“Kwa kutambua kuwa suala la ufisadi limekuwa mzigo mkubwa sana kwa Chama Cha Mapinduzi licha ya juhudi kubwa ambazo serikakli ya CCM imezifanya katika kupambana na tatizo hilo hapa nchini, Halmashauri Kuu ya Taifa ilielekeza kuwa Chama Cha Mapinduzi lazima kipige vita ufisadi kwa nguvu zaidi, na ionekane kinafanya hivyo ndani ya chama chenyewe, katika jamii na katika serikali inazoziongoza. Kwa ajili hiyo Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua kuwa viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi watafakari, wajipime na kuchukua hatua wenyewe kwa maslahi ya chama. Wasipofanya hivyo chama kitawawajibisha bila kuchelewa.”

Hawa walitajwa na viongozi wa CCM kuwa ni Lowassa, Andrew Chenge na Rostam Aziz ambaye amekwisha kujiuzulu nyadhifa zote ndani ya chama hicho, Julai 13, mwaka huu. Aliachia ubunge na ujumbe wa NEC.

Waliokuwa wanatazamwa wachukue hatua kama hizo ni Lowassa na Chenge ambao wanasema wazi kuwa hawajui mashitaka dhidi yao . Katika mkutano wa NEC uliopita, Kamati Kuu ya CCM imeomba kibali cha NEC kuchukua suala hilo ili kulifanyia maamuzi yaani ngazi ya chini inaomba kibali kutoka ngazi ya juu kufanya kazi ya ngazi ya juu!

Inaaelezwa kwamba suala hilo sasa linapelekwa kwenye kamati ya maadili. Inawezekana huko ufumbuzi ukapatikana. Lakini kama nilivyosema hapo juu, viongozi wa CCM waliopo sasa kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi taifa, viongozi serikalini hususan mawaziri ni zao la mtandao, ambao kwangu mimi ninauona kama ufisadi mwingine wa madaraka.

Kwa bahati mbaya CCM hawataki kuzungumzia chimbuko hili, wanatibu matokeo, kiini kinaachwa kinazalisha virusi mwaka baada ya mwaka. Tangu mwaka 1995 na kwa kasi kubwa zaidi kati ya 2001-2005 uchafu, rafu na kila aina ya hila zilichezwa. Haya hayazungumzwi.

Kwa fikra zangu ndani ya CCM na serikali yake hayupo msafi hata wa dawa, wote wana mawaa yao , la msingi wajifungie watafute maridhiano. Ni vigumu kumaliza tabu iliyoko CCM bila kwenda kwenye mzizi ambao ni mtandao na makandokando yake, wote wanahitaji toba.

0
No votes yet