CCM wapanga kuhujumu CHADEMA


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 08 June 2011

Printer-friendly version
Viongozi wa CHADEMA wakiwa mahakamani

MKAKATI wa makusudi umesukwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kudhoofisha jitihada za kisiasa za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), MwanaHALISI limeelezwa.

Mkakati unalenga kuzuia viongozi wakuu wa CHADEMA kufanya kazi za kisiasa na hata za kibunge; kwa kuwapotezea muda katika malumbano na polisi, serikali na mahakama.

Taarifa zinasema katika mpango huo, CCM na serikali yake wamepanga kuwakamata na kuwafungulia kesi viongozi wakuu wa chama hicho ili kuzima moto uliowashwa na chama hicho mijini na vijijini.

MwanaHALISI limeelezwa na kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa serikali kuwa hata kuzuiliwa kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwenye Kituo Kikuu cha Polisi (Central) jijini Dar es Salaam kwa maelezo ya kutekeleza amri ya mahakama, ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo.

Mbowe aliwekwa rumande jijini Dar es Salaam kwa siku mbili mfululizo, kati ya Jumamosi na Jumatatu asubuhi, baada ya mwenyewe kujipeleka kituoni.

Ilipofika usiku wa manane Jumapili, Mbowe alipelekwa uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam na kupakiwa kwenye ndege kubwa ya jeshi chini ya ulinzi mkali wa viongozi wa Polisi mkoani kwa safari ya mjini Arusha.

Tayari mpaka sasa, wabunge zaidi 10 wa chama hicho wameshakamatwa na kufunguliwa kesi mahakamani au polisi.

Ukimuondoa Mbowe, viongozi waliokamatwa na kufikishwa mahakamani au polisi, ni Godbless Lema (mbunge wa Arusha Mjini), Philemon Ndesamburo (Moshi Mjini) na Joseph Selasini (Rombo).

Wengine ni Meshack Opurukwa (Meatu), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Esther Matiko (Viti Maalum) na Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini).

Mbali na wabunge, viongozi wengine wa chama hicho wanakabiliwa na lundo la kesi mahakamani.

Hao ni pamoja na Dk. Willibrod Slaa, katibu mkuu wa chama hicho, mwenyekiti wa mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na kiongozi wa ngazi ya juu katika Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA), Dadi Igogo.

“Nakwambia kijana, yote haya yanafanyika kwa madhumuni ya kuidhoofisha CHADEMA. Haiwezekani kwamba mtu amejisalimisha polisi mwenyewe, azuiliwe kwa kisingizio cha kutekeleza amri ya mahakama,” ameeleza mtoa taarifa.

Amesema kukamatwa na kuwekwa rumande kwa Mbowe kumefanyika ili “kumdhalilisha yeye binafsi na kuwatisha wanachama na wafuasi wa chama chake.”

Amesema, “Mkakati huu umelenga kuwajenga wanachama woga na kuwafanya viongozi waliofunguliwa kesi kushindwa kutimiza majukumu yao kwa kuwa hadi uchaguzi mkuu unafika wanakuwa bize na kesi na hivyo wanashindwa kufanya kazi zao za kisiasa.”

Kukamatwa kwa Mbowe kumekuja wiki moja baada ya Jaji Mkuu wa Tanzania Bara, Othman Chande kuhudhuria semina elekezi iliyoitishwa na serikali mjini Dodoma.

Haijafahamika mara moja kama kamatakamata hiyo inatokana na semina hiyo au imekuja kwa “bahati mbaya.”

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Arusha, Charles Magessa ndiye aliyetoa amri ya kutaka Mbowe akamatwe kwa madai kuwa, si yeye wala mdhamini wake, waliofika mahakamani kueleza kilichowasibu siku kesi yake ilipotajwa tena.

Tangu Januari mwaka huu, Mbowe na viongozi wenzake kadhaa walishitakiwa kwa tuhuma za kufanya maandamano bila kibali cha polisi.

Gazeti hili limeelezwa na vyanzo vya uhakika kuwa Hakimu Magesa awali alikubaliana na hoja zilizotolewa mahakamani na mdhamini wa Mbowe ambaye alieleza kuwa alikuwa mgonjwa na si kweli kuwa hajawahi kufika mahakamani kwa muda mrefu.

Baada ya maelezo ya mdhamini wa Mbowe, hakimu Magessa alikubali kufuta hati ya kumkamata Mbowe na aliridhia haja ya Mbowe pamoja na wabunge wengine wanaoshitakiwa pamoja kuruhusiwa kushiriki vikao vya bunge.

Lakini katika hali ya kushangaza, jioni ya siku hiyo, hakimu Magessa alitoa uamuzi wa kukamatwa kwa mwanasiasa huyo mwenye ushawishi mkubwa.

Taarifa zinasema ni baadhi ya maofisa wa mahakama waliopeleka taarifa za amri ya kumkamata Mbowe kwa wakili wake, Method Kimomogoro.

Mara baada ya wakili Method kujulishwa kuwa hakimu Magessa ameendelea na msimamo wake wa kutaka Mbowe akamatwe, haraka alirudi mahakamani ambako inadaiwa alikuta hakimu ameshaondoka kazini.

Taarifa zinasema hakimu alikwenda Babati kwenye harusi.

Wakili Method ameelezwa kukutana na msajili wa mahakama. Naye msajili inaelezwa alipitia jalada la mwenendo wa kesi na kukuta, pamoja na kuwapo maelezo ya kutosha ya mdhamini wa Mbowe, hakimu Magessa bado aliamuru Mbowe akamatwe.

“Baada ya kuona hivyo, msajili wa mahakama aliamua kuwasiliana na hakimu kwa simu yake ya mkononi na kumweleza kuwa alikuwa hajafuta amri inayomtaka Mbowe akamatwe. Akatakiwa kumuagiza hakimu kiongozi aliyepo kufuta amri hiyo ili kuondoa usumbufu kwa mhusika,” anasema mtoa taarifa.

Hata hivyo, mtoa taarifa anamnukuu hakimu akisema, “Nitakuja kushughulikia mwenyewe Jumatatu.”

“Unajua yule hakimu alifuta hati ya kukamatwa Mbowe. Lakini hakutoa uamuzi kimaandishi. Hivyo ikatolewa amri Mbowe akamatwe,” ameeleza ofisa huyo wa mahakama mjini Arusha.

Maelezo ya ofisa huyo wa mahakama yanafanana na yale yaliyotolewa na wakili Method, kwamba hakimu Magessa alijichanganya katika uamuzi wake.

Mbowe alijipeleka mwenyewe polisi Jumamosi jioni na kuwa na mashauriano yaliyodumu kwa saa kadhaa kati yake, viongozi wa jeshi la polisi na wanasheria wa chama hicho, Mabere Marando na Lissu.

Hata hivyo, baada ya makubaliano ya jinsi atakavyokwenda Arusha, imeelezwa kuwa aligeuziwa kibao na kushikiliwa hadi juzi Jumatatu alipofikishwa mahakamani mjini Arusha.

Katika mashauriano hayo, viongozi wa polisi walikuwa wamekubaliana na maombi ya mawakili wa CHADEMA kuwa Mbowe aende mwenyewe mahakamani Jumatatu asubuhi, lakini kwa sharti kwamba aripoti katika kituo hicho cha polisi na kisha ataruhusiwa kuondoka.

Wakili Marando amethibitisha kuwa kabla ya Mbowe kwenda kujisalimisha, kulifanyika majadiliano marefu kati yao na viongozi wa polisi; majadiliano yaliyolenga kutafuta njia mwafaka ya kumfanya kiongozi wao kufika Arusha bila bughudha.

“Ni kweli tulikwenda polisi kufanya majadiliano ya jinsi mwenyekiti wetu atakavyofika Arusha. Tulifanya hivyo kwa nia njema. Hatukutaka mwenyekiti wetu kwenda kienyeji ili asije kukamatwa uwanja wa ndege au njiani wakati anakwenda Arusha na kisha ikatafsiriwa kuwa alikuwa anataka kukimbia,” ameeleza Marando.

Anasema, “Tulipokuwa katika majadiliano hayo, ndipo polisi wakaeleza kuwa makubaliano hayo hayawezi kufanyika bila mheshimiwa Mbowe kufika ili aonekane ameripoti polisi. Na sisi hatukuwa na pingamizi; tukafanya kama tulivyokubaliana.”

Habari zinasema baadaye, polisi wakionekana kama waliopokea amri kutoka juu, waligeuka na kumueleza Mbowe kuwa yuko chini ya ulinzi, jambo ambalo wakili Marando anasema linaonekana lilifanywa kwa shinikizo kutoka nje ya jeshi la polisi.

Akizungumzia kukamatwa kwa Mbowe, Dk. Slaa alituhumu mbele ya waandishi wa habari, Jumapili iliyopita kuwa Rais Kikwete na chama chake wamesimama nyuma ya matukio yote ya kukamatwa kwa viongozi wa CHADEMA.

Alionya kuwa chama chake kimechoka kunyanyaswa na kusema, “Hakuna wa kuzima moto tuliowasha.”

0
Your rating: None Average: 3 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: