CCM wapata funzo kura ya maoni


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 04 August 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi

HATA wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hawana hamu na chama chao. Wamerudisha kadi zao kwa viongozi wao.

Wanapinga ufedhuli, ubabe na utovu wa uadilifu ulioonyeshwa na viongozi wao wakati wa mchakato wa kura ya maoni Jumapili iliyopita.

Wanachama halali wa matawi ya Mtambani A na B katika Kata ya Jangwani, jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa wanachama wa CCM nchi nzima waliosimama imara kupinga kunyang’anywa haki yao ya kupiga kura ya maoni.

Ni hivi: Majina ya wanachama halali wapatao 760 (vyombo vingine vya habari vimerekodi 490) katika Kata ya Jangwani, hayakuonekana kwenye orodha ya wapigakura.

Wanachama walipouliza maofisa wao na maofisa wakakosa majibu, wakaamua kurejesha kadi zao kwa njia ya kukana chama au kutishia kufanya hivyo.

Hayo yemetendeka ndani ya chama kilichopanga ikulu kwa karibu miaka 50 sasa; kinachojidai kuwa na “demokrasia pana;” kinachojigamba kwa kusimamia “amani, umoja na mshikamano.”

Hayo yametendeka kilomita mbili kutoka ikulu – Ofisi Kuu ya utawala nchini na makao ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hayo yametendekea kilomita mbili kutoka Makao Makuu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ambayo inadai kuwa imejipenyeza “kila mahali” kukabiliana na wala rushwa.

Hayo yametendekea – kata ya Jangwani – kwenye mdomo wa ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba.

Kwingine jijini Dar es Salaam – mbele ya utawala wa nchi – baadhi ya wananchi wamepewa kadi feki; kadi nyingine hazina picha za wahusika na baadhi ya zenye picha hazina namba zilizo katika mtiririko wa kiofisi katika eneo hilo.

Mmoja wa wagombea, Shy-Rose Bhanji, alikiambia kituo cha televisheni – ITV kuwa udanganyifu ulikuwa mwingi – mawakala wake walikataliwa na katika maeneo mengine waliambiwa waende vituoni saa 10.

Baadhi ya wapigakura watarajiwa jijiji Dar es Salaam, wameeleza kuwa wamekuta majina yao yamewekewa alama ya “ndiyo” kuonyesha kuwa tayari wamepiga kura, wakati hawajapiga.

Kilichotendeka Dar es Salaam ndicho kimetendeka Kata ya Kisabuka, Tarime ambako zaidi ya majina 1,000 ya wanachama hayakuonekana katika daftari la chama la wapigakura.

Katika wilaya ya Musoma Vijijini usambazaji wa vifaa vya kupigia kura ulicheleweshwa kwa baadhi ya vituo.

Kwenye kituo cha Nyamatale, wanachama walioonekana kuwa na hasira walinyakua masanduku na kukimbia nayo kwenda kusikojulikana.

Katika kata za Lamadi na Kalemela wilayani Magu, Mwanza, taarifa zinasema katibu wa wilaya wa CCM alibeba karatasi za kupigia kura lakini “akasahau” masanduku.

Ukifanya majumuisho ya yaliyotokea katika mchakato wa kura za maoni, hutashindwa kuhitimisha kuwa kuna udanganyifu, ukora na ubabaishaji.

Hutashindwa kuona kuwa kulikuwa na maamuzi ya awali, miongoni mwa wasimamizi, juu ya nani awe mshindi na hivyo kuandaa mazingira yanayoelekeza huko.

Ukiona au hata kusimuliwa juu ya kilichotendeka katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM, utapata sura inayofanana na ile ambayo imekuwa ikilalamikiwa, mwaka hadi mwaka tangu 1995 katika uchaguzi mkuu.

Hii ni sura ya uvurugaji – alimradi kila kitu kiende ovyoovyo na wenye nia yao wanufaike na hali hiyo.

Sura ya wizi – ili kura zipigwe bila masanduku au masanduku yakicheleweshwa, basi hakutakuwa na muda wa kuyakagua, wakati tayari yamesheheni kura kwa yule ambaye waandaaji wanapenda.

Sura ya utawala mbaya – uvunjaji haki kwa kunyang’anya wanachama haki yao ya kupiga kura. Hii inafanywa kwa kuweka alama inayoonyesha mtu kapiga kura wakati hajawahi kufika hata kwenye kituo.

Sura ya ufisadi – kwamba baadhi ya wagombea wanaandaliwa na “kuchaguliwa” hata kabla hawajaingia kwenye uchaguzi. Kinachofanyika siku ya uchaguzi ni kuhalalisha uteuzi wa awali.

Kinachosikitisha ni kwamba yote haya yametendeka ndani ya chama chenye serikali; kile ambacho kimekuwa ikulu tangu kupatikana kwa uhuru wa kisiasa wa Tanganyika na baadaye Tanzania.

Kinacholeta uchungu ni kwamba hayo yanatendeka katika chama ambacho serikali yake, pamoja na kutuhumiwa kusaidia au kufumbia macho wizi wakati wa kupiga kura, ndiyo itasimamia uchaguzi mkuu mwaka huu.

Kinachotetemesha wengi ni kwamba, kama chembechembe za nia mbaya, uchafuzi, wizi wa kura na ufisadi vimejitokeza ndani ya CCM wakati wa mchakato wa kura za maoni, basi kuna uwezekano wa serikali ama kuiga au kuendeleza mkondo huohuo.

Wakati naandika makala hii, rafiki yangu alinisimulia njia nyingine iliyotumiwa na mmoja wa wanaotafuta kuwa wagombea ubunge mkoani Dar es Salaam.

Mgombea mtarajiwa alimweleza rafiki yangu kuwa alishona mashati mengi ya kijani kwa ajili ya wajumbe. Ndani ya kila shati akashonea Sh. 20,000. Aliacha mashati kwa fundi kwa kila mmoja kujichukulia. Mashati yote yamechukuliwa na hakuna aliyelalamika.

Huu unaonekana mfano mmoja “mdogo” na labda wenye sura ya kuchekesha. Lakini ndivyo rushwa zinavyotolewa katika mazingira ambamo CCM inapeperusha mdomo kulaani rushwa na TAKUKURU inajigamba kutoepukika.

Kinachoweza kuleta matumaini kwa wananchi ni kwamba hata ndani ya CCM kuna wanaochukia rushwa; tena wengi – kuanzia Dar es Salaam hadi kila kona ya nchi hii.

Kinachochochea matumaini ni kwamba viongozi ndani ya CCM wanaendelea kuwadhihirishia, tena kwa vitendo, wanachama wao kuwa rushwa itaendelea na kuendelea.

Kinachowapa mwanga wanachama wa CCM, juu ya wanavyoendelea kutelekezwa, ni matukio ya mwishoni mwa wiki iliyopita; pale waliposhuhudia wao au wenzao wakinyang’anywa haki yao ya kupiga kura ya maoni.

Matukio haya yamekuwa mwalimu mkuu kwa wanachama wa CCM. Yamekuwa changamoto kwao – waamue kubaki katika fumanizi ya kisiasa au waseme hapana kwa vitendo vya unyimaji haki.

Ni mazingira haya ya msongo ndani ya chama kikongwe, yanayounganisha wanachama wake na umma nje ya CCM, katika kutafuta uongozi mbadala.

Kuanzia sasa, wananchi watakuwa katika nafasi nzuri ya kuona, kusikia, kuzingatia na kupima hoja za wanaotafuta uongozi wa kitaifa kabla ya uchaguzi mkuu Oktoba 31 mwaka huu.

Kwa msisimko wa wagombea, na hasa kujitokeza kwa Dk. Willibrod Slaa wa CHADEMA kugombea urais mwaka huu, hakuna kisingizio cha wananchi kusema hawana wa kuchagua.

Hata wanachama wa CCM hawana sababu ya kuogopa au hata kuhama chama chao, hata kama kinawanyanyasa kwa sasa. Wanaweza kuchagua rais au mbunge wa chama kingine huku wakiendelea kuwa wanachama wazuri wa chama chao.

Kule kuchagua mtu makini wa viwango vya Dk. Slaa, kutalazimisha kuwepo mabadiliko katika CCM na katika vyama vingine. Kutachochea kuwepo viongozi makini na kuongeza ushindani wa kisiasa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: