CCM watamani Wangwe awaokoe Tarime


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 30 September 2008

Printer-friendly version
Marehemu Chacha Zakayo Wangwe

VYAMA vya siasa vinavyowania ubunge wa jimbo la Tarime vipo katika kampeni ya kunadi wagombea wake ili wapate ridhaa ya wananchi kuchukua kiti hicho. Jimbo hilo limetokea kuwa moja ya majimbo yenye ushindani mkali wa kisiasa nchini.

Kwa Tanzania Bara, tofauti na visiwani Zanzibar, maeneo yenye ushindani wa kweli wa kisiasa yanajulikana. Na ni kawaida katika maeneo hayo kuona kila aina ya vitimbi.

Kuna vitimbi vya wanasiasa ucharwa kujitokeza kwa ajili ya kuchumia matumbo yao; kuna vitimbi vya wenye nafasi serikalini kutamani sana kutumia jeshi la Polisi kuwasaidia; na kuna hata vitimbi vya kutumia njia za ghilba kwa nia tu ya kusaka kura.

Tarime kwa muda mrefu kambi ya upinzani imejijenga, lakini pengine si Tarime tu labda ni mkoa wa Mara kwa ujumla. Mwaka 1995 mkoa huu kwa mfano ulipata wabunge wanne kutoka kambi ya upinzani.

Kwa  maana hiyo Tarime kuwa ngome ya upinzani si kitu cha kushangaza, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinafahamu.

Zaidi sana Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere anafahamu. Kwani wakati akiwania ubunge kwa kupitia NCCR-Mageuzi Arusha mjini mwaka 1995 na kushinda kiti hicho kabla ya ushindi wake kutenguliwa na Mahakama Kuu, alijua nguvu ya upinzani mkoani Mara.

Wasira ambaye sasa ni Waziri wa Kilimo na Chakula anafahamu vizuri nguvu ya upinzani mkoani Mara.

Anaifahamu vilivyo kwa sababu mwenyewe alichangia kujenga nguvu hiyo kwa sababu yapo mambo ya msingi ambayo anajua wazi kwamba serikali ya CCM tangu mtangulizi wake, TANU 1961-1977; imeshindwa kabisa kutekeleza mkoani humo.

Kwa hali hii Tarime imejingea heshima mbele ya umma wa taifa hili kuwa ni eneo ambalo siasa za kweli za upinzani zinachezwa.

Tatizo linalojitokeza ni moja tu, kwamba CCM ama kwa kujua au kwa makusudi ya kujitia kichwangumu, imekataa kukiri kwamba imeshindwa kufanya lolote la maana kwa mkoa huu tangu uhuru.

CCM inafahamu ni sera zake zisizozingatia maslahi ya taifa zimezidi kujenga makundi makubwa ya vijana wasiokuwa na ajira mkoani Mara.

Ni sera za CCM kwa miaka yote hii zimeruhusu vijana waliokuwa na kazi yao ya kuchimba dhahabu katika ardhi waliopewa na babu zao kama urithi wanaondoshwa kwa kisingizio cha kupisha wawekezaji kwa kulipwa fidia sawa na makombo ambayo hata mbwa hapewi chini ya meza ya bwana wake.

Ni sera za CCM za kushindwa kutambua kwamba wananchi wa Tarime hawana tena imani nao kwa sababu wamegeuzwa kuwa wapakazi ndani ya nchi yao. Ni sera ambazo zimeshindwa kutambua kwamba huwezi kuwaleta wawekezaji katika nchi ili kuwageuza wananchi wako kuwa watu wasiokuwa na ajira kwa kisingizio chochote kile.

Hii ni Tarime ambayo wananchi wake walikwisha kuamua siku nyingi kwamba hawako upande wa serikali.

 Hii ni Tarime ambayo mbunge wao, Marehemu Chacha Zakayo Wangwe, akiwawakilisha bungeni kupitia Chadema, hakwisha kuvutana na serikali juu ya uvunjaji wa haki za wapigakura wake waliokuwa wanapambana na wawekezaji ambao serikali imeamua tu kuwapa ardhi yao na wao wakaambiwa waende kufa njaa.

Ni Tarime ambayo wananchi wamejenga uadui na serikali kwa sababu nyingi za kiuchumi; kuzuia kufanya biashara ya mpakani kiasi cha kuwekewa vizuizi vya barabarani hata kushindwa kusafirisha chakula kutoka wilaya moja hadi nyingine.

Hii ni Tarime ambayo kero na kupuuzwa kwa kilio chao miaka na miaka imezaa watu wasioogopa, watu waliotayari kupambana na polisi kama vile Wapalestina watumiavyo gombeo kupambana na vifaru wa Waisrael.

Hawa ni raia waliochoshwa na unafiki wa siasa za amani za CCM wakati wakiwaswaga kwenye njaa na ufukara utakaochukua roho zao.

Hii ni Tarime iliyomjenga Wangwe akawa diwani wao na baadaye Mbunge kiasi cha kujizolea ufuasi usiokuwa na shaka kwa sababu alikuwa anazungumza lugha ya wenye kiu, wenye njaa, waliokuwa wanabambikiziwa kesi kama yeye mwenyewe alivyobambikiziwa kesi zisizo na idadi.

Sera hizi za ovyo kabisa za CCM ndizo zilimjenga Wangwe kiasi cha kushindikana na watawala wakaanza kumtafutia njia ya kumdhibiti si kwa kupitia sanduku la kura, ila kupitia nguvu za dola.

Wangwe huyu akawa adui namba moja wa CCM akafunguliwa kesi juu ya kesi, wakamweka ndani, bila kujua kwamba wanamjenga. Huyu akawa ni adui kweli kweli. Adui wa sera zao, adui wa umashuhuri wa CCM, adui wa wawekezaji wa CCM wanaochimba dhahabu ya nchi hii pasipokutuachia chochote.

Adui namba moja wa CCM Tarime ghafla akatwaliwa katika ulimwengu huu wa majonzi na mapambano yasiokwisha, CCM wakaamua kuguuza sifa zake.

Wakaanza kumlilia. Wakalia machozi ya mamba; wakavaa hata sare za chama chao, CCM, kwenda kumzika Wangwe, ili tu wapate huruma ya wananchi wa Tarime.

CCM wakashindwa kuteka hata msiba wake baada ya vijana jasiri kuwakemea na kuwaokataa na sare zao msibani, sasa wameamua kutumia jina la Wangwe na msiba wake kutafuta kura.

CCM imesahau kwamba sera zao za ovyo ndizo zilimnjenga Wangwe, wanashindwa kusimama jukwaani sasa wakiri kwamba njaa, dhiki, ukosefu wa kazi, na kila aina ya umasikini unaoendelea mkoani Mara hususan wilayani Tarime, ni matokeo ya sera zake mbovu.

CCM sasa inacheza tambola Tarime, mara inarusha kadi ya kifo cha Wangwe, mara inatumia familia ya marehemu, mara inatuma mamluki wake kununua shahada za wapiga kura na mwishowe inaelekea kutuma hata walinda usalama wavunje sheria ya kutokushabikia chama cha siasa kununua kadi ya chama cha siasa.

Haya yote yanafanyikwa kwa nia moja. Kutaka kuchukua jimbo la Tarime. Lakini CCM inashindwa kujua kwamba mchawi wake ni sera zake yenyewe, ndiyo maana Tarime imejengeka kuwa ngome ya kweli ya vyama vya upinzani.

Ni katika mazingira haya, kifo cha Wangwe hakiwezi kuwa mtaji wa kisiasa wa CCM, sana sana wataingia kaburini Tarime, wajue tu Wangwe ni mfu sasa hataweza kuwaokoa kwa sababu walimtesa na kumsamakama mno akiwa hai, mzimu wake utawachoma.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: