CCM watamtosa Kikwete


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 30 November 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

KABLA ya kufikia uamuzi wa jambo fulani la kitaalam, wasomi hubungua bongo taaluma iwaongoze. Hakuna kupiga kura.

Kura hutumika katika masuala ya kisiasa. Mtindo huu wa kura huwa hauzingatii uzito wa hoja ila wingi wa kura kurahisisha mambo.

Upande unaopata kura chache huhesabika umeshindwa hata kama una hoja zenye maslahi. Wajumbe hutumia msemo wa wengi wape.

Bungeni utasikia, “Nadhani waliosema ‘ndiyooooo’ wameshinda” na mara utasikia wabunge wengi wa CCM  wakishangilia kupitishwa jambo hata kama halina faida.

Maamuzi yenye madhara yaliyotokana na dhana hiyo ni mengi. Nitadondoa machache.

Fikra za mwelekeo wa michezo nchini chini ya Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa zilijionesha kupitia kwa Waziri wa Elimu na Utamaduni, Joseph Mungai.

Akawasilisha bungeni hoja ya kufuta michezo. Upinzani haukusikilizwa. CCM wakaridhia, wakapiga makofi na meza kuunga mkono.

Mwaka mmoja baadaye, wabunge walewale walianza kupita kwenye vyombo vya habari kulaani michezo kufutwa shuleni. Tayari katika baadhi ya shule, maeneo ya viwanja yalijengwa madarasa na majengo mengine na shule zilizoanzishwa hazikulazimika kutenga maeneo ya viwanja.

Kana kwamba wabunge wa CCM wamerogwa, Mungai aliungwa mkono alipowasilisha bomu jingine – akafuta baadhi ya masomo na mengine akayaunganisha.

Uamuzi huo ulipitishwa mwaka 2004, mitaala mipya ikaandaliwa kwa dharura ili itumike kuanzia mwaka 2005. Mwaka huo mmoja wa utekelezaji wa mitaala ya Mungai, ikawa vurugu kubwa.

Baada ya kuingia Jakaya Kikwete, fikra zake zilijionesha kupitia kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Margaret Sitta, aliyewasilisha hoja ya kurejesha mitaala ya zamani.

Katika kipindi cha Mkapa, mwaka 2004 wabunge wa CCM walipitisha sheria ya manunuzi ya umma kwa nia ya kudhibiti vitu kuukuu, lakini mwaka huu, wabunge wale wale wa CCM wamepitisha sheria kuiruhusu serikali kununua ‘mitumba’.

Mwenendo huu ni vigumu kujua lini wabunge wa CCM wanakuwa na busara na lini hawana au lini wana uwezo wa kupinga uozo na lini hawana.

Kati ya 1995 – 2000 CCM walishupalia kupitisha sheria ya mgombea urais awe na shahada lengo lilikuwa kumbana Augutine Mrema wa TLP. Loo, kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 CCM wakagundua ‘wangejiua’ upande wa Zanzibar, wakaacha.

Tume ya Jaji Nyalali iliyokusanya maoni kuhusu haja ya kuanzishwa vyama vingi nchini au la, ilisema asilimia 20 tu ndio waliunga mkono mfumo wa vyama vingi huku asilimia 80 wakitaka chama kimoja.

Mwalimu Nyerere alishauri serikali izingatie uzito wa hoja za wachache na mabadiliko ya kidunia. Serikali ya CCM ‘ikapata’ busara ikaanzisha mfumo wa vyama vingi lakini inakosa busara katika utekelezaji kwani ndiyo inaeneza uvumi kuwa vyama vingi vinasababisha vita.

Mtazamo wa Rais wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi kuhusu Katiba unajionesha alivyochuja maoni ya Tume ya Jaji Nyalali, na mtazamo wa Mkapa kuhusu katiba ni alivyomfokea na kuchuja ripoti ya Tume ya Jaji Robert Kisanga.

Mtazamo wa Nyerere kwamba asilimia 20 wasikilizwe na pia kuzuia mgombea binafsi ni kuzima demokrasia, ndiyo ‘boti’ anayopaswa kusafiria Rais Kikwete badala ya mvumo wa wanafiki eti wengi wape.

Kikwete anajua. Aprili aliungwa mkono na wana CCM alipoibua falsafa ya kujivua gamba, lakini wamemwacha anasutwa kila upande huku wakitaka kumvua uenyekiti. Hata suala la katiba, CCM watamtosa aanguke.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: