CCM yafyata kwa mafisadi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 May 2011

Printer-friendly versionSend to friend
Andrew Chenge

VIONGOZI wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameshindwa kuwaondoa katika chama hicho wale wanaowaita watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini, imefahamika.

Viongozi ambao waliotajwa kuwa wanatakiwa kujiondoa kwenye uongozi au chama ndani ya siku 90 kwa kuwa ni “mafisadi wanaochafua sura ya chama mbele ya jamii,” ni Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge.

Kinyume na majigambo ya viongozi wa juu wa chama hicho, kuwa sharti watuhumiwa hao waondolewe kwenye vikao vya maamuzi, hadi sasa chama kimeshindwa kuwapa barua za kuwajulisha juu ya suala hilo.

Katibu Mkuu Wilson Mukama, katibu wa itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, John Chiligati wamekuwa wakishindilia kuwa “mafisadi lazima waondoke.”
 
Hata hivyo, Mukama aliwaambia waandishi wa habari juzi Jumatatu, jijini Dar es Salaam, “…hakuna mahali popote katika maazimio ya NEC panapotaja siku 90.”

Alisema, “Kama ni muda basi ni pale mwenyekiti wetu aliposema NEC ijayo. NEC hukutana kila baada ya miezi minne na kwa hiyo kama ni siku, basi ni 120 na siyo 90,” alieleza Mukama akijibu swali la mmoja wa waandishi waliotaka kufahamu ni lini chama hicho kitaandika barua na kukabidhi watuhumiwa.

Kauli ya Mukama kwamba hakuna mahali ambapo NEC imeagiza Lowassa, Rostam na Chenge waondoke ndani ya chama katika muda wa siku 90 zijazo, imekuja wiki moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kukutana kwa faragha na Lowassa.

Taarifa za ndani ya chama na kutoka baadhi ya viongozi wa CCM, zinasema mazungumzo ya viongozi hao wawili yalijikita katika kile kilichoitwa “kujivua gamba” na kwamba Lowassa anamtuhumu Nape kusambaratisha chama chao kwa kuendeleza tuhuma katika mikutano ya hadhara.

Lowassa na Kikwete walikutana ikulu jijini Dar es Salaam, 25 Aprili 2011 baada ya kushindwa kukutana mjini Dodoma, 3 Aprili 2011 kama ambavyo Kikwete alikuwa ameahidi.

Katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari, Mukama alisema, “NEC ilitoka na maazimio 26. Azimio mojawapo linasema chama kiendelee na mapambano yake dhidi ya ufisadi na kwamba watuhumiwa wakitafakari, wajipime na kuchukua hatua.”

Alisema, “Sehemu ya hotuba ya mwenyekiti wakati akifunga mkutano ilisema tunatambua athari ya kukosekana maadili katika chama na tuendelee kupambana; na katika hili hakuna ajizi. Viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi wajitafakari, wajipime na wachukue hatua,” alisema Mukama akinukuu kauli ya mweneykiti wa CCM, Rais Kikwete.

Alipoulizwa ni watuhumiwa gani wa ufisadi kwa kuwa chama hicho hakijawahi kuwa na orodha yake, badala yake orodha inayofahamika kwa wengi ni ile iliyotolewa na kiongozi mkuu wa upinzani nchini, Dk. Willibrod Slaa, Mukama alisema, “…CCM ni taasisi kubwa yenye mfumo wake na miongozo yake; hivyo haitegemei orodha ya CHADEMA.”

Mukama alikuwa akijibu swali la Manyerere Jackton wa New Habari House. Alitaka kufahamu vigezo vinavyotumika kutambua mafisadi; na iwapo wataweza kumwondoa Kikwete ndani ya chama hicho kwa vile naye ametajwa katika orodha ya Dk. Slaa ya tarehe 15 Septemba 2007.

Hata hivyo Mukama aliendelea kushikilia kuwa chama chake hakiwezi kufuata orodha za vyama vingine, hasa CHADEMA.

Kwa upande mwingine Lowassa amenukuliwa akimtaka Kikwete kumdhibiti Nape kwa kuwa “anakivuruga chama” kwa hatua yake ya kusisitiza kuwa NEC ilipitisha maamuzi ya kuwataka wajiuzulu, wakati akijua fika kwamba hilo si kweli.

“Mkutano kati ya Lowassa na rais ulikuwa mfupi sana. Lowassa alimueleza Bwana Mkubwa (rais Kikwete), jinsi asivyofurahishwa na mwenendo wa Nape hasa jinsi anavyowatuhumu ufisadi. Alimsihi Rais Kikwete kumweleza hilo katibu wake mwenezi, Nape…,” ameeleza mtoa taarifa.

Kikwete, taarifa zinasema, alimhakikishia Lowassa kuwa “…hakuna lolote litakalotokea,” kauli ambayo imethibitishwa na Mukama katika mazungumzo yake na wahariri.

“Yule bwana (Lowassa) alimuuliza Kikwete, mnataka kunipa barua kwa kosa lipi? Nimefanya nini? Nini ambacho wewe hukifahamu,” anasema mtoa taarifa wa MwanaHALISI.

Gazeti hili limejulishwa na vyanzo vyake vya ndani ya serikali kuwa uamuzi wowote utakaochukuliwa na Lowassa, unaweza kuzidisha mgawanyiko ndani ya CCM.

Mara baada ya Lowassa kukutana na Kikwete, taarifa zinasema mbunge huyo wa Monduli alikutana na kufanya mazungumzo marefu na Peter Kisumo, mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya chama hicho.

Katika mazungumzo yao, Lowassa alionya kuwa CCM kiko hatarini kupasuka kutokana na kauli za Nape na mwenzake John Chiligati juu ya ufisadi na watuhumiwa wake.

“Huyu bwana anaua chama. Nakuhakikishia mzee Kisumo, hawa watu wakiendelea kunishutumu bila sababu, nitatoka hadharani na kujibu mapigo,” anaeleza mtoa taarifa akimnukuu Lowassa katika mazungumzo yake na Kisumo.

Naye Kisumo anaripotiwa kumhoji Lowassa, “Mbona ninyi marafiki wawili mnataka kusambaratisha chama?” Naye Lowassa alijibu, “Kheri iwe hivyo…”

Mwandishi wa gazeti hili alimtafuta Lowassa ili kuthibitisha walichojadili na Kikwete, lakini simu yake iliita bila kupokelewa.

0
Your rating: None Average: 2 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu:
Barua ya Wazi kwa Mh Rais JK juu ya Vikwazo vya Elimu Tanzania Mimi ni mwalimu mzoefu wa miaka takribani 25,nimekuwa nikikerwa na vikwazo vinavyorudisha maendeleo ya elimu nyuma hapa nchini. Kwa kawaida wananchi wengi baadhi ya vikwazo wanavyovijua ni pamoja na upungufu wa walimu,uhaba wa majengo na vifaa vingine vya kufundishia na kujifunzia, uwajibikaji mdogo wa baadhi ya walimu na wadau wengine muhimu,nk. Pamoja na vikwazo hivyo nakupongeza wewe na serikali yako kwa jitihada zilizokwisha fanyika ikiwa ni pamoja na kupeleka uendeshaji wa shule za sekondari TAMISEMI suala lililoondoa ukiritimba na urasimu uliokuwepo kabla. Mh JK, pamoja na hayo ziko sababu zingine zinazokwamisha elimu ambazo maafisa walioko wizara ya elimu hawakwambii ama kwa maksudi au malengo binafsi. Naomba nikuume sikio, nitataja sababu mbili tu. Ya kwanza ni mfumo mbovu wa uteuzi wa maafisaelimu ngazi mbalimbali ambao ndio wasimamizi wa elimu huko. Katika hili mazingira ya rushwa,udugu na urafiki ndiyo hutawala. Wafuatao ni maafisa wachache walioteuliwa kwa mfumo huo.1. H.Batinoluho ambaye ni afisa elimu Karagwe- aliwekwa na Bw Kagolo wa wizarani kwa lengo la kusimamia mashamba yake huko kijijini Karagwe,huyu tayari ana kesi mahakamani ya wizi wa fedha ya serikali, 2. G.Fabian aliwekwa katika nafasi na Bw Kagolo kuwa afisaelimu Bukoba- wilaya ambayo ni ya mwisho kitaaluma katika mkoa licha ya kuwepo mazingira mazuri 2. O.Rujuba ambaye ni afisa taaluma Ngara aliwekwa na Bw.Ndabise wa wizarani kwa lengo la kusimamia mashamba yake kijijini, licha ya kwamba alifeli mtihani wa dipoloma ya ualimu. 3. Elian Yowel- licha ya kwamba ana vyeti vya kughushi lakini aliwekwa katika nafasi ya uafisa sayansi kimu na kaka yake wa wizarani aitwaye Elia Kibga, 4. Afisa Elimu Rombo alihamishwa kinyemera ili kukimbia kesi ya wizi wa fedha ya serikali, sasa amerudishwa kujibu kesi. Mh JK hawa ni mfano tu lakini wako wengi nchi nzima. Je, tutafika? Ningependekeza uteuzi wa maafisa elimu pia upelekwe TAMISEMI na Maafisaelimu Mikoa wahusike katika mchakato kwani wao ndio wanajua utendajikazi wa maafisa walioko chini yao. Mh JK tatizo la pili ni mfumo wa baraza la mitihani unaoruhusu uvujaji wa mithani.Nampongeza Dkt Ndalichako na vijana wake, kwa jumla wanajitahidi lakini mfumo huo ni wa zamani sana , unahitaji marekebisho uli uweze kuhimili mzigo mkubwa wa watahiniwa waliopo sasa tofauti na zamani. Ningependekeza uanzishwaji wa kanda maalum za mitihani katika mikoa mbalimbali ili kuimarisha uratibu wa mitihani. Mh JK, nakusudia kuendelea kutoa maoni moja kwa moja kwako ili kuepuka upuuziaji wa taarifa na maoni ya wananchi unaofanywa na baadhi ya watendaji wako wakuu katika wizara ya elimu na mafunzoa ya ufundi. Mwl Mhoro Joseph, Morogoro
Lowasa unasubiri nini? Hivi unafikiri mzee wa kaya anampango na wewe au anavuta muda tu huku akikupa matumaini, ukweli ni kwamba wewe umeshika mpini kwa uhai wa chama mimi nakushauri toka hadharani maliza kazi ili tujue moja