CCM yatamani utawala wa kijeshi

SERIKALI imekiri udhaifu. Hapana. Imekiri kushindwa kutawala. Sasa inasema itapeleka jeshi wilayani Tarime litawale badala yake.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema iwapo halmashauri za wilaya za Tarime na Rorya hazitamaliza "mapigano ya wananchi" yanayoendelea, basi serikali itazivunja na kupeleka jeshi kutawala.
Kinachotendeka Tarime na Rorya ni wizi wa mifugo miongoni mwa jamii. Walioibiwa wakifuata nyayo na kukumbana na watuhumiwa wa wizi, mapigano yanaanza.
Ni bahati mbaya kwamba viongozi wa serikali ngazi ya taifa, mikoani na wilayani wamekuwa wakidai kuwa haya ni "mapigano ya kikabila." Lakini ni bahati mbaya zaidi kwamba serikali imeshindwa kuyasitisha. Serikali kuu inayakimbia. Inatamani matumizi ya jeshi.
Pinda amefika mbali kwa kusema kuwa mapigano yasipositishwa au kumalizwa, viongozi wa halmashauri wajiuzulu. Bila shaka akitumia siasa kutishia halmashauri ya Tarime ambayo inaongozwa na upinzani chini ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Waziri Mkuu alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Mkendo mjini Musoma kuadhimisha Siku ya Serikali za Mitaa, wiki mbili zilizopita.
Ametoa miezi sita kwa halmashauri za wilaya hizo mbili kuweka mkakati wa kumaliza mapigano vinginevyo zitafutwa na "litapelekwa jeshi kutawala…"
Nina mashaka kama Pinda amekubaliana kwanza na Rais Jakaya Kikwete kwamba jeshi linaweza kutangazwa hadharani kuwa linamegewa sehemu moja ya nchi hii, ili litawale badala ya siasa na utawala wa hiari.
Nina mashaka ya kutolewa kauli hii hadharani lakini sina mashaka juu ya matumizi ya jeshi kimyakimya kukidhi mahitahi ya wanasiasa kama ambavyo Pinda anadhihirishwa.
Imetokea katika nchi kadhaa; kukawa na vurugu kubwa ambazo polisi wameshindwa kutuliza, hivyo kusababisha serikali kupeleka askari wa jeshi la ulinzi kurejesha utulivu kabla hatua za kuleta amani hazijaanza.
Lakini limekuwa suala la kurejesha utulivu tu, siyo "kupeleka jeshi kutawala." Limekuwa suala la kukiri polisi kuelemewa, siyo tuhuma kwamba serikali za mitaa zimeshindwa kazi. Limekuwa suala la kuangalia haraka uhai wa raia na mali zao, siyo vijembe kwa halmashauri za wilaya kuwa zimeshindwa kazi.
Bali kauli ya waziri mkuu inalenga kuonyesha kuwa kila patakapokuwa na mapigano na mauaji ya wananchi, serikali itapeleka wakuu wa mikoa na wilaya ambao ni askari wastaafu wa jeshi la ulinzi au itamwaga askari moja kwa moja kutoka kambini.
Aidha, kauli ya waziri mkuu imetolewa wakati mbaya. Ni wakati wa maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa, Oktoba mwaka huu na uchaguzi Oktoba mwaka kesho.
Katika kipindi cha uchaguzi tunashuhudia serikali ikitangaza matumizi ya jeshi la nchi, tena kwa majigambo, katika moja ya wilaya zake ambako waajiriwa wake wameshindwa kufanya kazi.
Tamko la waziri mkuu limefuatiwa na tangazo jingine la serikali, kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani, la kuajiri askari polisi 7,000 mwaka huu wa fedha kwa maelezo kuwa "watasaidia" kulinda amani na utulivu wakati wa chaguzi zinazokuja.
Na uchaguzi mkuu wa mwakani unatarajiwa kuwa mgumu kwa chama kilichoko ikulu. Hii ni kutokana na migongano ndani ya chama hicho na mwamko na uelewa wa wananchi juu ya kinachoendelea ndani ya utawala.
Kwa hiyo, kauli ya waziri mkuu ya kutumia jeshi Tarime na Rorya, yenye shabaha ya kuua sisimizi kwa kutumia bunduki, inaonekana kuwa pendekezo, leo au kwa siku zijazo, la kuchukua njia ya mkato ya kupunguza "adha za uchaguzi na matokeo yake."
Bali ili kupunguza makali ya serikali kuonekana imeshindwa kazi, Pinda anasema mapigano yakitokea, mwenyekiti wa halmashauri anamlilia, "…mzee huku hali mbaya; nifanye nini mimi wakati ninyi ndio wenye watu," anauliza.
Hapa ndipo kuna undumila kuwili. Kwanza, waziri mkuu anataka kuitua serikali kuu jukumu la ulinzi na usalama, na badala yake kulitwisha halmashauri za wilaya ambazo, kwa maana yoyote ile, ni asasi za kijamii.
Pili, waziri mkuu anajichanganya. Wakati anatamani matumizi ya jeshi, anajigamba kuwa mkoa wa Mara, ambako mapigano yanaendelea kuua watu wengi, ndiko kuna watawala waliowahi kuwa askari wa jeshi.
Ni Pinda aliyekaririwa na vyombo vya habari na hajakanusha, kuwa mkuu wa mkoa wa Mara ni "mwanajeshi." Mkuu wa wilaya ya Rorya ni "kanali" wa jeshi. Mkuu wa wilaya ya Tarime ni "kada" wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuongeza, "…tukiona anashindwa tutamtoa…tuweke mwanajeshi."
Kauli hizi za Pinda zina maana nyingi na pana. Kwanza, kwamba si siri tena kuwa uteuzi wa askari wastaafu wa jeshi kuwa wakuu wa wilaya na mikoa, siyo wa bahati mbaya. Ni makusudi.
Pili, kwamba sehemu za mkoa wa Mara, bila tangazo maalum la serikali, zinatawaliwa na jeshi na kwamba ana mpango wa kujaza wilaya zote na "watawala wa kijeshi." Ni makusudi. Si bahati mbaya.
Tatu, kwamba siyo bahati mbaya kuwa wilaya nyingi nchini zina wakuu wa wilaya na mikoa ambao ni askari. Hii ni kwa kuwa askari hawa wanakuwa kimbilio la wanasiasa walioshindwa kutumia siasa kuleta mabadiliko; kulinda wananchi na mali zao.
Bali kwamba mkoani Mara kuna mkuu wa mkoa ambaye ni askari mstaafu; katika wilaya moja kuna askari mstaafu pia, lakini bado kuna mapigano mkoani humo – Tarime na Rorya – hili nalo laweza kuwa na maana ya nyongeza.
Askari ni wapiganaji na siyo watawala katika nafasi za kisiasa. Mkoani Mara ambako walipewa nafasi za kutawala wameshindwa kutumia siasa na wameshindwa kutumia mabavu kukomesha mapigano na mauaji. Waziri mkuu anaona kigugumizi kuwalaumu hadharani.
Utawala ni menejimenti. Maana ya menejimenti ni matumizi ya akili, stadi maalum na werevu katika eneo la kazi. Ni matumizi ya yote hayo katika kuandaa mipango na kuweka mikakati ya utekelezaji na kuitekeleza. Haya ni mambo ya kusomea shuleni au kazini kwa kupanda ngazi.
Menejimenti haihusiani na uwezo wa kutoa amri, ukubwa wa sauti, urefu au ufupi wa muhusika; ni stadi zinazokua na kukuzwa katika medani maalum ya utendaji. Bali menejimenti zinatofautiana; ndiyo maana hazihitaji kupandikizwa – menejimenti ya jeshi juu ya menejimenti ya siasa.
Ama wewe ni askari, unabaki jeshini; ukiacha au ukistaafu kazi unatafuta kazi inayolingana na ulichosomea, ulichofanya miaka yote au kile kinachoshabihiana. Hupandikizwi katika menejimenti inayohitaji stadi na werevu tofauti.
Mahali pengine ambako askari wamebebeshwa nyadhifa za menejimenti katika siasa, wamejikuta wakipwaya; bila nyenzo za kitaaluma kuwawezesha kujua kinachohitajika; kushiriki kuandaa mipango na kuisimamia na hatimaye kushindwa kuleta mabadiliko au maendeleo yaliyotarajiwa.
Hapa ndipo panazaa obunula bubili – "huku tamu na huku tamu." Serikali inakuwa na hamu ya kutumia askari wastaafu katika nafasi za siasa kwa shabaha ya kupandikiza woga, kama Pinda anavyoeleza kwa makini.
Serikali inatazama bila kuona na inaogopa kusema kuwa iliowatarajia kutumia mitulinga kuisaidia, sasa wameshindwa. Hili ndilo linavunja usiri na kuonyesha mapungufu katika kuchaganya utawala wa kiraia na ule wa kijeshi.
Ni hili linaloibua hisia kwamba nia ya baadaye ya baadhi ya wanasiasa walio kwenye utawala sasa ni kutelekeza utawala wa kiraia mikononi mwa jeshi, pale watakaposhindwa menejimenti ya kisiasa au watakapokwanguliwa, kwa njia ya kura, kutoka kileleni. Hii ni hatari.
Hatari hii inajitokeza kwa uwazi zaidi kutokana na waziri mkuu kuogopa kulaumu utawala mkoani Mara na badala yake kulaumu asasi za kijamii. Kwani mambo ya ulizi na usalama yako chini ya serikali kuu.
Wawakilishi wa serikali kuu na wenye mamlaka ni mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya, siyo halmashauri za wilaya. Vitisho ambavyo Pinda anavurumishia halmashauri vilistahili kuelekezwa kwa serikali kuu na wawakilishi wake kwa ngazi za chini.
Badala ya kujiangalia, kujitafiti na kugundua udhaifu wake na kuuondoa, hapa serikali inalaumu viongozi wa halmashauri za wilaya na kutafuta upenyo wa kutimizia nia yake ya kutawala kwa ubia na jeshi.
Nani atatuhumu bundi wa kisiasa kwa kilio chake kuwa watawala wanataka kutumia jeshi ili wabaki madarakani au katika mazingira magumu zaidi, basi jeshi lichukue madaraka, lakini asichukue mwingine katika mpangilio wa kisiasa?
Nani anataka utawala wa kijeshi Tarime, Rorya na nchini? Nani anatamani mabavu ya jeshi badala ya utawala unaotokana na utashi wa wananchi; hata kama ni kwa watawala kutumia kile walichowahi kuita "teknolojia" kuiba kura za wapinzani wao?
Vitisho na wizi wa kura ni mambo ya muda tu pale umma unapokuwa haujaelewa vya kutosha. Kadri kunapokucha, ujinga ukatokomea kama jua la Magharibi, ujasiri ukaibuka mapema kama alfajiri ya nyakati za kiangazi – mitaji hii miwili – woga na ujinga, huyeyuka mara moja.
Siyo tu wananchi huweza kupinga ghiliba; huweza pia kukataa na kupinga utawala wowote uliowekwa au ulioendelezwa kwa hila na mabavu.
Kuna hatari. Kama serikali inataka kusambaza mabavu katikati ya menejimenti ya siasa huko Tarime, Rorya na sehemu nyingine nchini, bora itambue mapema kwamba wanajeshi ndio wamesomea mabavu.
Watakapoona wanaotaka mabavu hawana mabavu, watajiuliza kwa nini wao, waliosomea mabavu, wasiingie serikalini na kutumia mabavu? Kiama!