CCM na zimwi la Sarwatt

SERIKALI ya Jamhuri inatenda kama vile iko kwenye mashindano na mahakama. Kila mahakama inapotoa tafsiri za katiba au kufanya maamuzi muhimu yanayogusa maslahi ya kisiasa, serikali haitaki kuheshimu maamuzi hayo.
Ni tofauti na nchi nyingine duniani. Huko uamuzi wa mahakama huheshimiwa.
Uamuzi wa mahakama ulitokana na shauri lililofunguliwa mahakamani na Mchungaji Christopher Mtikila aliyepinga uamuzi wa serikali wa kuzuia mgombea binafsi katika uongozi wa kisiasa.
Serikali imekata rufaa kupinga uamuzi huo. Lakini Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustino Ramadhani akiwa mmoja wa wana jopo wa Mahakama ya Rufaa wanaosikiliza rufaa hiyo, amesema uamuzi huo ndio unaotambuliwa kisheria hadi sasa.
Wakati mahakama ikisisitiza kuwa huo ndiyo uamuzi unaotambuliwa kwa sasa, viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameibuka na parapaganda mpya. Wanasema, suala la mgombea binafsi ni tete na halipaswi kufanyiwa parapara. Wanataka wananchi waendelee kuvuta subira.
Hawasemi wasubiri hadi lini. Badala yake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Bunge), Philip Marmo na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John CHiligati wanasisitiza kwamba “CCM haitendi mambo yake kwa papara.” Utadhani nchi hii watu wote ni CCM.
Lakini ukweli ni kwamba serikali inaogopa mgombea binafsi kutokana na yale yaliyotokea huko nyuma ambapo chama cha TANU kilibwagwa na mgombea binafsi.
Ilikuwa ni katika jimbo la Mbulu. TANU ilipambana na Elias Sarwatt (sasa marehemu), ambaye baadaye alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki.
Baada ya Sarwatt kukatwa na chama chake kwa maelezo kuwa hauziki kwa wananchi, aliamua kugombea kama mgombea binafsi. Alishinda kwa kishindo.
Katika mazingira ya sasa ambapo chama kikongwe, kilichochoka na hata kuzeeka, uwezekano wa CCM kukimbiwa na watu makini ni mkubwa kuliko ilivyokuwa wakati wa Sarwatt.
Kinachoogopwa na CCM ni mifano iliyotokea pale ilipoengua wanachama wake walioongoza kura za maoni.
Wananchi wamewapa imani wana CCM waliobadili chama baada ya kuenguliwa na kugombea kupitia vyama vingine.
Bila shaka katika hali hii ambayo wananchi wamepoteza imani na chama hicho, huku wananchi wengi wakiamini zaidi watu badala ya vyama, CCM inaweza kujikuta inatokomea kisiasa.
Ni kuvuna kile ambacho chama hicho kimepanda; dharau kwa wananchi. Ubaya ni kukataa kupokea mavuno hayo.
Maamuzi au amri za mahakama katika nchi nyingi huheshimiwa na kutumika kama sheria kwa jambo husika na wenyewe wanasheria husema “Majaji hutunga sheria” na kuwa nyongeza ya zile zilizotungwa na Bunge.
Dharau inayoonyeshwa na baadhi ya makada wa CCM kwa mihimili mingine ya dola, mahakama na bunge, inazusha mashaka.
Kinachofanywa na CCM ni kuvunja sheria na kudharau dhana ya mgawanyo wa madaraka kwa mihimili ya dola. Umuhimu wa kila mtu kuheshimu misingi ya demokrasia hauhitaji ufafanuzi kwa watu jamii ya Chiligati.
Angalau Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye ameliona hili sasa, miaka mitano baada ya kuondoka madarakani na miaka 10 ya kuwapo kwake madarakani kama waziri mkuu.
Nini hasa kinachosababisha viongozi wa CCM na mawakala wao kukataa wagombea binafsi? Ni kuendekeza siasa za ukiritimba na woga wa kukubali demokrasia.
Baba wa taifa la China, Mao Dze-dung aliwahi kusema “Let the 1,000 flowers bloom” akimaanisha kuwa acheni maua 1,000 yachanue. Alikuwa anaamini mawazo ya wengi ni rutuba.
Utamaduni wa kila kitu kuendeshwa kwa kuzingatia fikra za mtu mmoja, na kwa maana ya mjadala, kuzingatia sera ya chama tawala tu peke yake, hauna nafasi tena zama hizi za uwazi, ukweli na utandawazi.
Kuruhusu wagombea binafsi katika uchaguzi, ni moja ya njia sahihi za kukomaza demokrasia katika taifa. Ni vema CCM ikajifunza kutoka kwa wengine.