Cesc Fabregas: Silaha tegemezi ya Arsenal

KWA muda mrefu sasa, Cesc Fabregas ametajwa kuwa ni mmoja wa viungo anayetarajiwa kufanya makubwa zaidi barani Ulaya. Lakini kama wengi wetu tulivyoshuhudia msimu huu, Fabregas sio tu ameonekana kuwa ni mchezaji mwenye kipaji, bali, kijana huyu mwenye umri wa miaka 21 ameonekana kukua katika wajibu wake akiwa uwanjani .
Sasa , bila shaka yeyote,tunaweza kabisa kusema, kuwa Cesc Fabregas, ambaye pia anaichezea timu ya taifa ya nchi yake ya Hispania, amekuwa mmoja wa wachezaji nyota wa dunia.
Kijana huyu ametoa mchango mkubwa kwa klabu yake ya Arsenal katika msimu wa ligi unaoendelea sasa, na hakika ndiye sababu ya mafanikio makubwa ambayo Arsenal imeyapata hadi sasa.
Kupitia makala hii tutachambua,ni kwanini Cesc Fabregas amekua kimchezo na kwanini Arsenal ya sasa ni bora bila Thiery Henry.
Itakumbukwa ilikuwa ni 25 Juni mwaka 2007 pale ilipowekwa hadharani kuwa aliyekuwa nyota na kiongozi mchezaji wa Arsenal, Thiery Henry alitangazwa kuihama Arsenal. Ilikuwa ni kama siku ya kiama kwa uongozi na wapenzi wa Arsenal.
Kuna ambao hawakuamini kilichotokea, kuwa baada ya misimu minane na klabu hiyo, Thiery Henry alifungasha virago kwenda Barcelona. Ni Thiery Henry alipewa mapenzi yote kutoka kwa mashabiki wa Arsenal.
Kwa kuondokewa na Thiery Henry, na kama kocha Arsene Wenger angeshindwa kumsajili mchezaji mwenye uwezo unaofanana na Thierry Henry, basi mashabiki wa Arsenal waliiona misimu yenye mabalaa mbele yao.
Hawakuamini kabisa kama Arsenal ingeweza kufanya vema katika ligi kuu ya England bila Thierry Henry. Kwamba ndoto ya kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya England nayo ikatoweka. Waliona pia ni jinsi gani klabu yao ingefanya vibaya katika michuano ya Kombe la Washindi na hivyo kupoteza matumaini ya ushindi.
Lakini kocha Wenger hakutetereka, alijikita kwenye mikakati yake. Aliwarudisha wachezaji kama Eduardo da Silva na Niclas Bendtner. Wawili hawa walikuwa ni wachezaji wa Arsenal walioazimishwa kwa klabu ya Birmingham msimu uliopita.
Hivyo basi, mashaka ya mashabiki hayakupotea, maana Arsenal waliuanza msimu huu wa ligi bila ya kuwa na jina la mchezaji- kiongozi mfano wa Thierry Henry. Hawakuwa na mchezaji aliyeaminika kuwa ndiye atakuwa mfungaji wa magoli wa kuaminika. Walionekana kuanza ligi na mtaji dhaifu. Mashabiki walikiona kiza kinene mbele yao.
Leo hali haiko hivyo. Hali ya mashaka imegeuka kuwa hali ya msisimko na kujawa na matumaini miongoni mwa mashabiki wa Arsenal. Ndoto zao na matumaini vimezaliwa upya.
Kwa hivi sasa Arsenal imewadhihirishia wale wote waliokuwa wakitilia mashaka uwezo wa timu hiyo kuwa wamekosea. Arsenal ni moja ya timu yenye kikosi kilicho katika hali nzuri kimchezo kwa sasa. Wachezaji wake wako 'fiti' na wanafanya vizuri mechi baada ya mechi.
Kuna sababu kadhaa zinazopelekea mafanikio hayo ya Arsenal mojawapo ni uwezo ulionyeshwa na kocha Wenger wa kuweza kujenga kikosi imara. Kikubwa zaidi ni kwa kocha huyo kuwaamini na kuwapa majukumu wachezaji wake kadhaa chipukizi.
Lakini sababu kubwa kabisa ni kijana yule anayezunguka uwanjani akiwa na jezi yenye nambari 4 mgongoni. Ni Cesc Fabregas.
Ni mchezaji huyu ambaye amechukua majukumu zaidi uwanjani, ameonyesha uwezo mkubwa kiasi cha kuwaridhisha mashabiki na kuwafanya kuwasahau wachezaji kama Patric Vieira na Thierry Henry ambao walikuwa na umuhimu mkubwa katika kikosi cha timu hiyo.
Kwa sasa Fabregas si tu mchezaji mwenye kipaji akiwa na miaka 22, tukisema hivyo hatutakuwa tumemtendea haki kijana huyu. Cesc Fabregas anaweza kabisa kusemwa, kuwa ni kiungo bora duniani hivi sasa.
Fabregas ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kutengeneza uwiano sehemu ya katikati. Ni ndoto ya makocha wengi kuwa na kiungo kama Fabregas mwenye uwezo wa kuusoma mchezo haraka.
Inapotokea Arsenal wanazidiwa, ni Cesc Fabregas anayechukua jukumu la kusawazisha na kuweka uwiano sehemu ya katikati. Maana, timu kushambuliwa na hata kuzidiwa nguvu ina maana ya timu kupoteza udhibiti wa sehemu ya kiungo.
Kocha Wenger ameonyesha kuridhishwa mno na mchango wa Cesc Fabregas msimu huu. Kwa maneno yake mwenye Wenger alilipotiwa kutamka yafuatayo;
"Sidhani kama kuna mwenye kutia shaka kuwa siku zote nilimwamini sana Cesc Fabregas. Lakini ni lazima nikiri, kuwa sikupata kufikiri kuwa angekuwa ni mchezaji aliyekua na kufikia kiwango chake cha sasa. Kwamba anachukua majukumu makubwa uwanjani kama anavyofanya katika msimu huu." Anasema Wenger.
Bila shaka, Fabregas ni silaha kali ya Arsenal kwa sasa. Msimu uliopita alipachika magoli 4 katika msimu mzima. Ona sasa, msimu huu amepachka mabao 11 katika mechi 17 za mwanzo, hapa tunahesabu pia magoli katika mashindano mengine nje ya Ligi Kuu.
Cesc Fabregas mwenyewe hapendi kuzungumzia mafanikio yake. Anadai hilo ni jukumu la wengine kumzungumzia.
Lakini anapobanwa sana huishia kusema, “Kwamba nani ni bora uwanjani hilo si jukumu langu kuzungumza, isipokuwa naweza kusema kuwa nafurahia kuwa ndani ya Arsenal. Najihisi nimekua na naweza kuendelea kuyabeba majukumu ninayoyabeba sasa niwapo uwanjani."
Anasema Cesc Fabregas aliyezaliwa Hispania akiwa na jina kamili la Francesc Fabregas Soler. Alijiunga na Arsenal mwaka 2004 akitokea shule ya soka ya Barcelona FC.