CHADEMA wametoa somo, lizingatiwe


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 17 August 2011

Printer-friendly version
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Wilibrod Slaa

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewafuta uanachama madiwani wake watano wa mkoa wa Arusha. Wengine wanasema haya ndiyo maamuzi magumu.

CHADEMA, kama vyama vingine vya siasa wana vikao vya chama. Matatizo ya kichama yaliyotokea yametatuliwa ndani ya chama. Uongozi ulio bora hujua nini cha kufanya na kwa wakati gani. Hakuna uswahili. Hakuna unafiki. Hakuna kupindapinda.

Madiwani waliovuliwa uanachama wamedhihirisha kuwa chama cha siasa hakiwezi kuwa chama cha ukombozi. Wananchi lazima wajikomboe wenyewe. Viongozi wa vyama ni wanadamu wenye matumbo na midomo. Waroho wa vyote, mali na madaraka, wapo hata ndani ya CHADEMA.

Walichosahau madiwani ni kwamba watu walipoteza maisha Arusha. Damu njema ya wanawema iliyomwagika haikuwa kwa ajili ya maslahi ya madiwani binafsi. Kuna baadhi ya wanachama na viongozi wa CHADEMA wanaokabiliwa na kesi mahakamani hadi hivi sasa kwa tukio hilo hilo ambalo madiwani hawa walitaka kulimaliza kwa kutanguliza maslahi yao mbele.

Kama ingetokea kwa viongozi wa kitaifa ingekuaje? Wako viongozi wa kitaifa wa CHADEMA waliowahi kutamka hadharani kuwa wanataka serikali ya umoja wa viongozi (wao wanasema serikali ya umoja wa kitaifa).

Maamuzi ya CHADEMA yanatoa fursa kwa vyama vingine vya siasa, hasa CCM na CUF, kujifunza kutokana na somo hilo. Tumeona maamuzi ya CUF kule Zanzibar ambako kama madiwani wa Arusha, viongozi wa CUF walikubaliana na viongozi wa CCM kugawana madaraka katika serikali ya Zanzibar.

Nao walisahau kuwa Pemba, maisha ya watu yalipotea, watu walikufa! Wako waliojeruhiwa na wangali na vilema vya maisha hadi leo! Kwa mara ya kwanza Tanzania ikazalisha kundi la wakimbizi. Hawa walikuwa wanapigania haki sawa kwa wote. Haki iliyohodhiwa na CCM. Zamani hawa wangeitwa wapigania uhuru.

Wana ANC wa Afrika Kusini walipigania uhuru wao kwa damu, kama CUF walivyoupigania Zanzibar na kama CHADEMA inavyoupigania Tanzania. Baada ya maridhiano walikubaliana kuunda serikali moja lakini Nelson Mandela wa ANC akiwa kiongozi mkuu, nchi ikaongozwa kufuata sera na itikadi za ANC.

Zanzibar na CUF haikuwa hivyo. Badala yake viongozi wa CUF waliamua kuachana na sera zao na itikadi ya chama chao na kukubali kutumika na CCM kwa ahadi ya vyeo serikalini. Leo wako ndani ya serikali kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM. Wanachama wa CUF wamebaki solemba.

Kama watu waliopoteza maisha yao Arusha wangejua kuwa walikuwa kwenye harakati zile ili madiwani wale watano wapate vyeo, nani angekubali kuutoa uhai wake?

Vivyo hivyo Pemba, waliokufa na waliojeruhiwa wangejua lengo ni kutaka viongozi wao wa juu kuingizwa katika utawala wa CCM, nani angekubali kuutoa uhai wake?

Maisha ya viongozi wao yameboreka kwa ushirikiano huu. Maisha ya wanachama je? Ugumu wa maisha ya waponda kokoto, wamachinga na wakulima waisho vijijini umeboreshwa?

Tangu waingie katika neema kuu walishawahi kuzuru makaburi ya marehemu waliowafanya leo waingie katika hiyo neema kuu? Walishaongelea fidia? Serikali ya CCM inayotumikiwa na viongozi wa CUF inaweza kuwaenzi mashujaa hawa? Kama hapana, wahenga waliposema wajinga ndio waliwao walikuwa na maana gani?

Kumbe shetani ni mbaya anapokula peke yake. Akiwashirikisha katika ufisadi wake, anageuka na kuwa malaika? Tuliwauliza viongozi CUF, dawa ya shetani ni kushirikiana naye?

CCM inapaswa kusoma somo la CHADEMA ili ijifunze namna bora ya kuwaondoa mafisadi bila kuwapigia kelele wananchi na bila kuisimamisha nchi kufanya maendeleo. Wananchi wameachwa waendelee na shughuli zao. Hawakupanda katika majukwaa na kuwabwatukia wananchi hovyo kama wendawazimu. CHADEMA imeonyesha umakini, ukomavu na busara ya hali ya juu.

Mafisadi ndani ya CCM walipozidiana waligawanyika. Mafisadi wengine wakaanzisha upuuzi waliouita vita dhidi ya ufisadi. Badala ya kutumia vikao na taratibu za chama walizojiwekea wenyewe kuwaondoa mafisadi, wao wakatoka nje ya chama wakawa wanapanda jukwaa moja baada ya jingine hadi wakaizunguka nchi nzima huku wakiipigia dunia baragumu kuwa ndani ya nyumba yao wenza wao, nguo zao za ndani ni chafu, zinanuka.

Kwa kufanya hivyo wakajikuta wamejidhalilisha wenyewe na kuichafua nyumba yao mbele ya wananchi. Wananchi ndipo walipofunguka macho na kutambua kuwa ala, kumbe CCM ni chama cha mafisadi! Wakaipotezea CCM hadhi iliyokuwa nayo machoni mwa wananchi.

Waliposhindwa kwa hilo, wakaja na ujinga mkubwa zaidi. Wakaanza upya kuizunguka nchi huku wakiwaeleza wananchi matakwa yao ya moyoni kuwa wangependa wenza wao wazivue nguo zao chafu wenyewe.

Wendawazimu wote hupitapita huku na huko wakisemasema hovyo yale wanayoyataka, bila kuwaambia wanaowasikiliza wanatakaa wawasaidieje?

Hawa nao wakawa wanawabwatukia wananchi bila kuwaambia wanataka msaada gani kutoka kwao ili matakwa yao ya kutaka mahasimu wao wajivue gamba wenyewe yatimie!

Wakati mwingine mtu unajikuta umesukumwa kukumbuka usiyotaka kukumbuka. Sijui kwanini nimeyakumbuka maneno ya Meya wa Dar es salaam Dk. Didas Masaburi kuhusu watu kufikiri. Ni muhimu sasa somo walilolitoa CHADEMA likazingatiwa.

Hali ya kisiasa nchini mwetu inasikitisha. Uongozi  wa nchi umetuama kama maji katika mtungi. Umefichama hata pale nchi ilipotikiswa na mgomo wa wauza mafuta.

Akiwa bungeni Januari Makamba aliuliza, “Waziri mbona husemi kitu? Waziri mkuu, siku saba sasa, mbona uko kimya? Semeni kitu! Serikali inakuwa kama haipo.”

Sijui kwa  nini Januari aliishia kwa waziri mkuu bila kuuliza mkuu wa nchi alikuwa wapi! Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ugumu wa maisha ya wananchi haumuhusu. Anahangaika na magamba yake. Mwenyezi Mungu atamsaidia!

Hatujui Mwenyezi Mungu ametupangia siku ngapi za kuishi hapa duniani lakini ni jukumu la kizazi chetu kuwatengenezea mazingira bora vijana wanaokuja kurithi uongozi wa taifa hili kutoka kwetu.

Siku za wazee tunaziona zikielekea ukingoni kama jua linavyokwenda kuzama Magharibi. Tunapowasikia vijana mahiri kama John Mnyika, Januari Makamba, Halima Mdee, Freeman Mbowe na wengine hamu ya kurejea kwake Muumba inazidi kuturejelea. Tunajawa imani kuwa nyuma yetu tunaacha viongozi thabiti.

Basi shikamaneni katika umoja na upendo kwa maana wote mmetoka katika udongo wa nchi hii, na humo wote mtarudi!. Ole, wake yule atakayeendelea kuhubiri fitina na chuki kati yenu kwa maana aliyemtuma ana dhambi kubwa zaidi!

0713334239
0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: