CHADEMA wamfanyia ushushushu Nchemba


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 27 May 2013

Printer-friendly version
    Yanasa ripoti yake; yeye agwaya 
Mwigulu Nchemba

TAARIFA ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyokuwa iongeze nguvu kwa chama hicho na serikali katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii bungeni, imeangukia mikononi mwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Hii ni taarifa juu ya mkutano wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda na wawakilishi wa wafugaji kutoka Loliondo, ambao wanapinga ardhi yao kumegwa na kuwekwa kwa eneo la mwindaji kutoka Nchi za Falme za Kiarabu.

Wafugaji walikutana na waziri mkuu na “mawaziri wenye dhamana za ardhi na maliasili katika ukumbi wa ofisi ya waziri mkuu, bungeni” mjini Dodoma tarehe 18 Aprili 2013.

Ni baada ya kikao hicho, serikali ilitangaza juzi kuwa wafugaji hawatanyang’anywa ardhi yao; ardhi itaendelea kutumiwa kama ilivyokuwa na kwamba “serikali itaanzisha utaratibu wa Wildlife Management Area – yaani utaratibu utakaoendeleza matumizi ya eneo hilo kwa binadamu, ufugaji na wanyamapori,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa ilikuwa inatoka kwa mtu mmoja aliyetajwa kuwa Kwagilwa Nhamanilo, ambaye gazeti hili limegundua kuwa ni mfanyakazi wa ofisi ya waziri mkuu. Ilikuwa ikipelekwa kwa Mwigulu Nchemba, mbunge wa Iramba Magharibi na naibu katibu mkuu wa CCM bara.

Wabunge watatu walioisoma, mmoja kutoka CCM wamekiri kuwa ililenga kumpa nguvu aliyetumiwa wakati wa mjadala wa wizara inayoongzwa na Balozi Khamis Kagasheki.

Imefahamika kuwa taarifa hiyo alikuwa aitumie Nchemba kukabiliana na waziri kivuli wa maliasili, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA) na hasa kwa kutumia kipengele cha mwisho kinachosema, “…wananchi wa Loliondo, kupitia wawakilishi wao, walikishukuru sana Chama Cha Mapinduzi na ofisi ya waziri mkuu kwa kuwajali.”

Mnadhimu Mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki, amekiri chama chake kuona taarifa hiyo na kwamba imewapa mtazamo wa nyongeza katika kuwasilisha hotuba yao.

Kwenye taarifa kwa Nchemba imeambatanishwa sehemu ya ripoti juu ya “Athari za Mgogoro wa Ngorongoro kwa CCM.”

Ripoti hiyo inatokana na Kamati Maalum iliyoundwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana kuchunguza mgogoro wa wafugaji katika eneo la Ngorongoro.

Pamoja na mambo mengine ripoti hiyo inasema, “Wananchi wengi wa Ngorongoro wanahisi kwamba CCM imeshindwa kuwatetea.  Matokeo yake tumeyaona, kwa mfano; kwenye  mkutano wa tarehe 02/04/13 uliozuiwa kwenye uwanja wa Wasso. Kadi 139 za CCM na Jumuiya zake zilitupwa na kuokotwa na viongozi wa chama.

Ripoti inakiri, “…tuliona pale wananchi walipowashinikiza mbunge na madiwani wote ambao hata hivyo ni wa CCM wajiuzulu. Hii ingepelekea kuingia katika uchaguzi mdogo ambao ungekiingiza chama katika gharama na kukichafulia taswira ya kisiasa.”

Katika mlolongo wa kukiri kuemewa kwa CCM, ripoti inasema, “Hali hii ikiendelea, inaweza kupelekea tukapoteza jimbo, kata na vitongoji vyote vya Ngorongoro katika chaguzi zijazo…”

Wabunge waliosoma ripoti hii wamesema lile eneo la woga wa CCM ndilo lingemwongezea uchungu na hivyo ukali, yule ambaye alikuwa amepangwa kukabiliana waziri kivuli wa maliasili na utalii.

Kwa upande wa CHADEMA, hotuba yao ya Jumanne ilikariri kilekile ambacho CCM inakiri kuwa wananchi wanakiona – ambacho ni “kushindwa kuwatetea” – kwa kugawa ardhi yao kwa wakuja kutoka nchi za nje kwa matumizi ya biashara ya utalii wakati wao hawana makazi na maeneo ya kulima.

Mchungaji Msigwa amesema serikali ya CCM “…imeelekeza nguvu katika kudidimiza na kudhoofisha uhifadhi, ulinzi na uendelezaji wa maliasili za nchi.”

Amesema “…serikali ya CCM sio tu imeelekeza nguvu kubwa katika uvunaji haramu wa maliasili za nchi, bali pia imefanya hivyo kwa manufaa ya wafanyabiashara wa kigeni wakishirikiana na wafanyabiashara wachache wa ndani ya nchi na viongozi waandamizi wa chama hicho na makada wake.”

Hotuba ya upinzani imeorodhesha kampuni za uwindaji na wamiliki wake na kuonyesha historia ya matatizo ya wafugaji – Wamasaai katika Ngorongoro na Loliondo.

Matokeo yake amesema “mgogoro kati ya wananchi wa Loliondo kwa upande mmoja; na Serikali ya CCM na kampuni ya Orthello Business Corporation (OBC) inayomilikiwa na mfanyabiashara wa kutoka Oman kwa upande mwingine, umezidi kuwa mkubwa.”

Anathibitisha mpasuko kati ya wananchi na serikali ya CCM kwa kutaja alichoita “maasi ya wananchi wa Loliondo yalivyoshuhudiwa mwezi uliopita na viongozi na makada wa chama hicho waliopo ndani ya bunge hili.” Wananchi walitupa kadi za CCM.

Kuibuka kwa taarifa za CHADEMA kunasa taarifa kwa  Mwigulu, kumekuja wiki tatu baada ya Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho na wakili wa mahakama kuu, Mabere Marando, kumwaga hadharani mawasiliano “ya mara kwa mara na isivyo kawaida,” kati ya Mwigulu na mmoja wa watuhumiwa wa ugaidi katika kesi iliyoko mahakamani.

Wachunguzi wa mambo wanasema uanikaji taarifa hizo ulilenga kuonyesha kuwa Mwigulu anahusika na kinachoendelea.

Mbali na Mwigulu, waliotumiwa ripoti ni pamoja na Dk. Asha-Rose Migiro, Nape Nnauye na Zakia Meghji, ameeleza ofisa wa CHADEMA.

“Huyu Mwigulu alikuwa anadhani kina Juliana Shonza, wako CHADEMA tu? Hii ripoti tumeipata humohumo ndani mwao kutoka kwa kina Shonza wa CCM. Tunawaambia hii ndiyo CHADEMA,” anaeleza ofisa huyo.

Shonza anayetajwa na ofisa huyo, alikuwa makamu mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA). Alifukuzwa uanachama mwishoni mwa mwaka jana kwa madai ya “utovu wa nidhamu.” Baadaye alijisalimisha CCM ambako amekuwa akizungushwa nchi nzima “kufungulia bomba la matusi kwa viongozi wakuu wa CHADEMA.”

Taarifa kutoka ndani ya CCM na serikali zinasema, “Ripoti ya Ngorongoro” ndiyo iliyopangwa kutumiwa na Nchemba na chama chake kama mtaji wa kisiasa wa kuonyesha wananchi wa Loliondo na maeneo jirani kuwa serikali ya CCM ni sikivu; na imesikia kilio chao, jambo ambalo limetibuliwa na upinzani.

Naye Mchungaji Msigwa aanakebehi CCM na serikali kuwa ni ya “ajabu sana. Umaskini umekithiri Loliondo. Wakuu wa familia wanazikimbia. Vijana wamekimbilia mijini na kuwaacha wazazi wakihangaika.”

Anauliza iwapo watu wa aina hii wanaweza hata kuipongeza CCM kwa lolote. “Hawana ajira yoyote. Hata ulinzi na udereva hawapati. Wanalalamika, lakini serikali imetia pamba masikioni, huku waziri wa maliasili akitamba kuwa ni lazima wapore ardhi yao.”

Akiongea kwa uchungu mbele ya Bunge, Mchungaji Msigwa alisema, “Wananchi wanalalamika. Kwamba watu kutoka maeneo mengine wamekuwa wakiletwa Loliondo na kufanya kazi ambazo hata wenyeji wana uwezo wa kuzifanya. Serikali haisikilizi kilio hiki.”

“Mgogoro wa Ngorongoro uliibuka upya Machi mwaka huu, baada Waziri Kagasheki kufika Ngorongoro na kuwatangazia wakazi wa eneo hilo kuwa ameagizwa na Rais Jakaya Kikwete kugawa eneo la Loliondo Game Control Area ya zamani, katika sehemu kuu mbili.

“Kule kuwaondoa hawa wafugaji katika maeno yao ya asili, ni sawa na kuiuwa mifugo yao. Wale wananchi wamesema hilo hawako tayari kulishuhudia na kwamba ni bora wafe kuliko kushuhudia mifugo yao inakufa,” alieleza Mchungaji Msigwa.

Soma sehemu ya hotuba ya Mchungaji Msigwa.

0
Your rating: None Average: 3 (2 votes)