CHADEMA yamweka pabaya JK


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 16 November 2011

Printer-friendly version

BUNGE kama limepasuliwa mapande; serikali imekaidi maoni ya wananchi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikimkasirikia Rais Jakaya Kikwete kutii “kupita kiasi” matakwa ya Zanzibar kuhusu mapendekezo ya muswada wa sheria ya marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Hayo ni matukio muhimu yaliyojiri ndani ya bunge juzi Jumatatu mkutano wa bunge la kumi ulipoanza wiki yake ya pili na mambo hayo yakajenga taswira mahsusi kuwa bunge la kumi siyo tu litakuwa kali zaidi kimivutano, mijadala na maamuzi, bali pia CHADEMA inayoongoza kambi rasmi ya upinzani, itasumbua serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Siku ilianza vizuri huku kiu kubwa ya wabunge wa kila chama, wakiwemo washika dola CCM, ikiwa ni kutaka kujua hasa serikali imejipanga vipi katika kuhakikisha muswada wa katiba unapita hata ikiwa kwa nguvu.

Kweli, baada ya bunge kukamilisha upitishaji wa muswada wa sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2004 ambayo sasa inaruhusu waziwazi serikali kufanya manunuzi ya mashine, mitambo, zana na vifaa vikiwemo vya shughuli za ulinzi vilivyotumika kabla, Spika Anne Makinda alichukua nafasi.

Alisoma kile kilichoonesha aliandaa mapema taarifa yake ya kuandaa wabunge kuisikiliza serikali kupitia mapendekezo yake katika muswada wa marekebisho ya katiba ya nchi. Akahimiza kanuni na utaratibu na kutamka hasa kuwa ni halali na ndani ya sheria na kanuni za bunge kuusoma muswada kwa mara ya pili na siyo ya kwanza kama yalivyo maoni ya wabunge wengi wa upinzani, hasa CHADEMA, pamoja na wanasheria magwiji na wanagenzi na watetezi wa haki za binadamu wanaosimamia haki za raia katika masuala ya wanawake, watoto, walemavu na demokrasia.

Hapo ikiwa tayari jamvi lilishakaa vizuri kwa ajili ya Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, mbunge wa Ulanga Mashariki, mkoani Morogoro, kutumia kuwasilisha muswada, wala hakuchelewa. Kwa kasi huku akitabasamu alifika kilipo kizimba na kusoma mapendekezo ya serikali.

Naye alisema kwamba ni halali kuusoma muswada kwa mara ya pili, siyo ya kwanza, kwa sababu kila hatua iliyotakiwa kufuatwa wakati muswada ulipoondolewa na kurudishwa kwa kamati ya katiba, sheria na utawala, kwa ajilia ya kufanyiwa marekebisho kama bunge lilivyoelekeza.

Lakini, katika kuonyesha umadhubuti wa hoja na uhalisia wa dhamira ya kutoa sauti ya mabadiliko, kila kile kilichoonekana chema alichokifanya waziri Kombani, kilichafuliwa vilivyo na msemaji wa kambi rasmi ya upinzani kuhusu masuala ya katiba na sheria, Tundu Lissu.

Katika hotuba yake iliyochukua chini ya nusu saa (dakika 30), Lissu, mbunge wa Singida Mashariki, aliupinga muswada akianzia na hatua yake ya kusomwa kwa mara pili na kurudia yale maagizo matatu makuu yaliyotolewa na Spika wakati muswada ulipoondolewa hati ya dharura ili urekebishwe upya.

Lissu akatunisha misuli na kumshutumu Spika Makinda kwa kile alichosema, “aliingilia utendaji wa kamati ya bunge” kwa kukataa kuiruhusu kamati kwenda kupata maoni zaidi ya wananchi kuhusu mapendekezo ya muswada.

Alisema kwa hakika muswada umebadilika mno hata kuliko yale mapendekezo yaliyotolewa uliposomwa kwa mara ya kwanza na maoni ya wananchi katika mikutano mitatu ya mjadala wa umma, iliyofanyika Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar ikiratibiwa na Kamati ya Bunge na kukabiliwa na mitafaruku mingi.

“Mabadiliko makubwa na ya kimsingi yaliyofanywa kwenye Muswada wa zamani yalihitaji na bado yanahitaji mjadala wa kitaifa wa wananchi kama ambavyo wengi wamedai katika mijadala inayoendelea nchi nzima.

“Bunge hili tukufu lilihitaji, na bado linahitaji, muda zaidi wa kuyatafakari mabadiliko haya makubwa na ya kimsingi katika muswada wa zamani. Katika mazingira haya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini ni busara na ni sound policy kwa muswada huu mpya kusomwa mara ya kwanza ili kuruhusu mjadala unaohitajika kufanyika,” alisema.

Jambo jingine kubwa ambalo Lissu alilihoji ni namna serikali kupitia muswada huo, ilivyotii matakwa makubwa ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na kusema “ni kama vile Rais Jakaya Kikwete amekubali matakwa yaliyotakiwa na yasiyotakiwa na Zanzibar katika mapendekezo ya muswada.”

Alisema Zanzibar imepewa uwakilishi “mkubwa mno” wakati mshirika mwenzake, Tanganyika, hayupo na hivyo Zanzibar kushiriki hata kwa masuala yasiyohusu muungano.

“Kwa mujibu wa ibara ya 5, Tume (ya Mabadiliko ya Katiba) hii itaundwa na Rais kwa kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar, na kwa ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar… kwa mujibu wa ibara ya 6(1), Rais atateua wajumbe wa Tume “... kwa kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar.

“Ibara ya 6(2) inapendekeza “... muundo wa Tume utazingatia msingi wa kuwepo kwa uwakilishi ulio sawa kwa kila upande wa Jamhuri ya Muungano.” Pendekezo hili linarudia, kwa njia iliyojificha zaidi, msimamo wa ibara ya 6(2) ya Muswada wa Zamani iliyokuwa imeweka wazi kwamba idadi ya wajumbe wa Tume itakuwa sawa kwa sawa kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano!

“Kama ilivyokuwa kwa muswada wa zamani, ibara ya 7(2) ya muswada inapendekeza uteuzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti (wa Tume) utafanyika kwa msingi kwamba iwapo Mwenyekiti atatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, basi Makamu Mwenyekiti atakuwa mtu anayetoka upande mwingine wa Jamhuri ya Muungano.

“Muundo wa Tume unakamilishwa na Sekretarieti ya Tume itakayoongozwa na Katibu. (ibara ya 13(1) Kwa mujibu wa ibara ya 13(2), Katibu huyo atateuliwa na Rais ‘baada ya kukubaliana na Rais wa Zanzibar.’ Watendaji wengine wa Sekretarieti watateuliwa na Waziri ‘kwa makubaliano na Waziri mwenye dhamana ya mambo ya Katiba wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.”

Lissu alisema kinyume na ilivyolalamikiwa katika muswada wa kwanza, katika muswada mpya, Rais Kikwete analazimika kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa kila hatua itakayotekelezwa katika mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya.

Hatua hizo ni pamoja na kuunda tume ya katiba, kuteua makamishna wa tume, sekretarieti ya tume, kupokea ripoti ya tume, kuikabidhi tena tume kuandaa muswada wa katiba utakaopigiwa kura ya maoni.

Lissu ‘alichafua’ hali ya hewa alipotamka kuwa katika muda wote wa uhai wa taifa, Tanzania imekuwa na rais mwenye madaraka ya kifalme na hiyo kutosha kuwa chanzo kikuu cha kukosekana tunu ya uwajibikaji katika ngazi zote za serikali na mwisho kuwa ndio kichocheo kikubwa cha rushwa na ufisadi wa kutisha kiasi cha sasa kuwa ni sehemu ya kawaida ya maamuzi ya kiserikali.

Kwa kunukuu kinachotamkwa katika Ibara ya 37(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaposema, Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote,” Lissu akasema muswada mpya unaendeleza kivuli kirefu hicho cha urais wa kifalme katika mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya.

“Mtu mwenye mamlaka ya kidikteta, kama Rais alivyo kwa mujibu wa Katiba ya sasa, hawezi kusimamia upatikanaji wa katiba ya kidemokrasia. Kwa kutumia mamlaka makubwa ya uteuzi wa Tume yanayopendekezwa na muswada huu, ni wazi Rais Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama tawala cha CCM, atateua wajumbe anaowataka yeye na Rais (Dk.) Ali Mohamed Shein, Makamu wake na pia Rais wa Zanzibar! Ni wazi vilevile watu watakaoteuliwa watakuwa ni watu wasiokuwa tishio kwa status quo kwa maana ya kupendekeza mabadiliko makubwa katika mfumo wa kikatiba na kiutawala na hivyo kuhatarisha maslahi ya CCM,” alisema.

Msimamo wa Lissu na CHADEMA una maana sasa chama hicho kitatekeleza ahadi waliyoweka tangu awali kwamba wataishitaki seriokali kwa umma iwapo itaburuza na kukataa maoni ya kutoa fursa kwa wananchi kuamua namna ya kutunga katiba wanayoitaka ikiwa ni hatua ya mara ya kwanza kabisa tangu wapate uhuru mwaka 1961.

0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)