CHADEMA yatikisa Ikulu


Fred Okoth's picture

Na Fred Okoth - Imechapwa 30 November 2011

Printer-friendly version

RAIS Jakaya Kikwete hakufahamu kwa undani kilichomo kwenye muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba (Constitutional Review Bill 2011), uliopitishwa na bunge hivi karibuni, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa kutoka serikalini zinasema Rais Kikwete alipata undani wa muswada huo pale alipokutana na ujumbe wa viongozi wa ngazi ya juu kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Rais Kikwete alikutana, Jumapili na juzi Jumatatu, ikulu Dar es Salaam na ujumbe wa CHADEMA, ambao imeelezwa kuwa ndio ulimfafanulia rais undani wa mapungufu makubwa katika muswada huo.

Taarifa zinasema, mara baada ya Rais Kikwete kusikikiliza zaidi ya hoja 15 zilizopangiliwa kwa ustadi mkubwa na CHADEMA, alisikika akisema, “Nimewaelewa. Mnazo hoja, tena za msingi.”

Mtoa taarifa amelieleza gazeti hili kuwa baada ya kikao cha pande zote mbili, Rais Kikwete “ameonyesha kukubali” kufanyia marekebisho makubwa katika muswada uliopitishwa na bunge hivi karibuni.

Imefahamika kuwa hoja ya kuacha kutia saini muswada ilishindikana kupatiwa ufumbuzi baada ya Rais Kikwete kueleza hatari inayomkabili mbele ya chama chake iwapo ataacha kusaini muswada ili uwe sheria.

Rais amenukuliwa akisema, “Hata mimi naona mnazo hoja za msingi, lakini nikigoma kutia saini, wenzangu kwenye chama hawatanielewa.”

Hata hivyo, mtoa taarifa anasema Rais Kikwete amekubali ombi la CHADEMA la kutafuta ushauri mpana zaidi kutoka kwa watu wengine mbalimbali juu ya umuhimu wa yeye kutosaini sheria hiyo kwa sasa.

Taarifa zinasema Kikwete alikuwa makini kusilikiza kila hoja ambayo CHADEMA walikuwa wanaieleza na kuitolea ufafanuzi. Kuna wakati alisema, “Kama hoja ni hii, mbona imeshindikana bungeni?” zimeeleza taarifa.

Ujumbe wa CHADEMA uliokwenda kuonana na Rais Kikwete uliongozwa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, makamu wenyeviti Bara, Saidi Arfi na Zanzibar, Said Issa Mohamed na  mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na mshauri wa siasa wa chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu.

Wengine walikuwa mwanasheria wa chama hicho, Profesa Abdallah Safari, mbunge wa Ubungo, John Mnyika, mkurugenzi wa masuala ya bunge na halmashauri ya chama hicho, John Mrema na mwanasheria mwingine wa chama hicho, Tundu Lissu ambaye ni katibu wa kamati hiyo.

MwanaHALISI limeelezwa na mtoa taarifa kuwa, kauli ya Kikwete ilitokana na uchambuzi wa kina wa hoja uliofanywa na Lissu hasa katika eneo linalohusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, adhabu zilizowekwa kwa watakaokiuka sheria na jinsi ya kupata Bunge Maalum la Katiba.

Akiongea kwa kuelekeza macho kwa baadhi ya wasaidizi waliokuwa kwenye mkutano huo, Rais Kikwete alihoji, “Kitu gani kimetokea kabla ya kwenda bungeni mpaka ikashindikana?”

Rais Kikwete alitaka kufahamu kilichotokea, hadi CHADEMA wakaamua kususia muswaada huo bungeni.

Akijibu swali hilo Lissu alisema mambo mengi yametokea. Alisema kwanza, spika alikuwa anawaburuza na hakutaka kuwasikiliza tangu mwanzo. Alisema siku zote alikuwa anasikiliza serikali, badala ya kufanya kazi za bunge.

Lissu alimweleza rais kuwa walimwambia spika kuwa muswada huo ulipelekwa bungeni kwa hati ya dharula, 9 Aprili 2011 na ukakataliwa; bunge liliagiza serikali itoe muda zaidi na iandae muswada huu kwa lugha ya Kiswahili ili wananchi wengi waweze kuusoma.

Alisema baada ya kazi hiyo kukamilika, muswada ulipaswa kuchapishwa kwenye gazeti la serikali na kutangazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari ili kutoa fursa kwa wananchi wengi kuuelewa.

Lissu amenukuliwa akimwambia rais, “Hata hivyo, hakuna hata moja ya maagizo haya ya bunge ambalo lilitekelezwa. Kamati ya Sheria na Katiba haikukaa kuujadili muswada huu tena kati ya tarehe 15 Aprili na 24 Oktoba 2011 wakati muswada ulipoletwa kwenye Kamati ukiwa umefanyiwa marekebisho makubwa.”

Alisema tafsiri ya kiswahili ya muswada wa Aprili ililetwa bungeni, 5 Novemba 2011, siku tatu kabla ya bunge kuanza mkutano wake wa Tano.

Kwa maana hiyo, Lissu alisema muswada wa sheria uliotolewa maoni na wadau kabla ya 24 Oktoba 2011, ulikuwa ule wa Aprili. Alisema wananchi hawakupatiwa fursa ya kutoa maoni yao juu ya muswada ulioletwa bungeni.

Muswada uliopitishwa ulitolewa kwa kamati, tarehe 24 Oktoba 2011 na kugawiwa kwa wabunge wote tarehe 5 Novemba 2011.

Hoja nyingine ambayo CHADEMA walimueleza Kikwete, ni kuhusu ubatili wa wabunge wa sasa wa Muungano katika Bunge Maalum la Katiba.

Kwa mujibu wa muswada uliopitishwa, wabunge wa sasa wa bunge la Muungano, ni sehemu ya bunge la katiba. Hili si sahihi, alisema Lissu kama alivyonukuliwa na mtoa taarifa.

Amesema, “Wabunge wa Bunge la Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar waliopo sasa, hawana uhalali kikatiba wa kutunga katiba mpya, kwani wote walichaguliwa kwa mujibu wa katiba ya sasa na wamekula kiapo cha kuilinda, kuihifadhi na kuitetea; na siyo kuiua.”

Mambo mengine ambayo yameripotiwa kujadiliwa kati ya rais na ujumbe wa CHADEMA ni Muungano. Katika hili, uongozi wa kamati ulimweleza rais kuwa hawapingi Muungano uliopo.

Kamati ilisema kwa hali ya sasa, Muungano ni kama haupo kutokana na hatua ya serikali ya Zanzibar kubadilisha katiba yake ambayo imefuta mambo karibu yote yaliyokubaliwa kwenye mkataba wa Muungano wa mwaka 1964.

Mtoa taarifa amesema, awali akiwasilisha mapendekezo ya CHADEMA, Lissu alimwomba Rais Kikwete kusaidia taifa lake kupata katiba mpya wakati taifa likiwa moja na wananchi wote wakiwa wameshikamana.

Amenukuliwa akisema, “Mheshimiwa Rais, tusaidie kupata katiba mpya ya nchi tukiwa tumeshikamana. Tusitafute katiba mpya wakati tumefarakana. Wala tusipate katiba wakati wengine wako gerezani, wengine wanasubiri kufungwa na wengine tumeumia,” alisisitiza.

“Muswada uliopitishwa na bunge na ambao wewe unatakiwa kuusaini, umepiga marufuku kufanyika kwa mikutano ya kuhamisisha wananchi kushiriki kwenye mchakato wa katiba na umetoa adhabu ya kifungo cha hadi miaka mitano au faini ya Sh. 15 milioni,” alinukuliwa Lissu akiwasilisha kwa rais.

Hoja nyingine za CHADEMA katika kabrasha walilomkabidhi rais, zinahusu uhalali wa kisiasa wa hoja ya kupatikana Bunge Maalum la Katiba; vigezo muhimu na wingi wa kura za kila chama katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Limo pia suala la mgawanyo wa wajumbe kwenye Bunge Maalum la Katiba ambako CHADEMA, chenye wabunge wengi, kina idadi ndogo ya wajumbe kuliko Chama cha Wananchi (CUF) chenye wabunge wachache, kwa mujibu wa muswada uliopitishwa.

Mengine katika kabrasha la CHADEMA lililoko mikononi mwa Rais Kikwete ni muswada wa sheria uliopitishwa kuwa na masharti yanayokiuka misingi na matakwa ya wananchi walio wengi.

Aidha, CHADEMA wamewasilisha kuwa Bunge Maalum la Katiba linaloundwa na muswada uliopitishwa linaendeleza hodhi ya CCM ya mchakato wa katiba mpya kwa kuipa zaidi ya nusu ya wajumbe wa bunge hilo.

Jingine ni kuhusu Katiba ya Jamhuri kutamka kwamba, “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano,” wakati katiba ya sasa ya Zanzibar inatamka, “Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Maeneo mengine ya makabrasha ya CHADEMA yanahusu migongano kati ya katiba ya Tanzania na ile ya Zanzibar na sehemu kadhaa ambako sheria za kawaida zinaondoa kile ambacho tayari kimewekwa na sheria mama – Katiba.

Unatolewa mfano wa mgongano ambapo katiba ya Muungano inasema, “Rais wa Jamhuri atakuwa mkuu wa nchi, kiongozi wa serikali na Amiri Jeshi Mkuu,” wakati katiba ya Zanzibar ya sasa inasema, “Kutakuwa na rais wa Zanzibar ambaye atakuwa mkuu wa nchi ya Zanzibar... Rais wa Zanzibar atakuwa kamanda mkuu wa idara maalum.”

Katika makabrasha ya CHADEMA kwa rais yamo pia masuala ya ulinzi na usalama; mengine yakigusa migongano, hasa katika kuanzisha majeshi upande wa serikali ya Muungano na ule Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: