Chalenji 2011: Mtihani kwa Mkwasa, Julio


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 16 November 2011

Printer-friendly versionSend to friend

MASHABIKI wa soka wa Tanzania Bara walilazimika kusubiri miaka 16 kufurahia timu yao ya ‘Kilimanjaro Stars’ ikitwaa kombe la michuano ya Chalenji mwaka jana.

Mara nyingine ambazo Tanzania Bara ilitwaa taji hilo ilikuwa mwaka 1994 ikiwa chini ya Syllersaid Mziray na Sunday Kayuni. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1974 chini ya Paul West Gwivaha.

Je, Kilimanjaro Stars itatwaa kombe hilo mwaka huu na kuwapa furaha mashabiki mwaka wa pili mfululizo au itasubiri tena miaka 16 mingine?

Bila shaka huo ni mtihani mgumu kwa makocha Charles Boniface Mkwasa na Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ waliokabidhiwa jukumu la kuinoa timu itakayoshiriki michuano hiyo mwaka huu.

Ni michuano mikubwa yenye historia ndefu na ushindani wa hali ya juu katika nchi za ukanda wa maziwa makuu kwa ngazi ya timu za taifa wanachama wa Baraza la Soka la Afrika Mashariki (CECAFA).

Michuano ya Chalenji ni urithi wa mashindano ya Kombe la Gossage ambayo fainali zake zilianza mwaka 1926. Iliitwa jina hilo kutokana na udhamini wa kiwanda cha sabuni cha Gossage.

Ilikuwa inashirikisha nchi za Afrika Mashariki; Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar kwa wakati huo ambapo fainali za kwanza zilikutanisha Kenya na Uganda Mei, mwaka huo wa 1926.

Kenya ilishinda kwa mabao 2–1 katika mchezo wa marudiano. Tanzania Bara au Tanganyika ilianza kushiriki mwaka 1945 huku Zanzibar wakijiunga mwaka 1949.

Tangu michuano hiyo kuanza kuitwa Chalenji miaka 37 iliyopita, Tanzania imetwaa taji hilo mara tatu. Tena mara mbili ikiwa kwenye ardhi ya Tanzania. Michuano hiyo ilianza mwaka 1993.

Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1974 ikiwa nyumbani baada ya kuwalaza mabingwa watetezi Uganda kwa mikwaju ya penalti 5-3 baada ya kutoka sare ya bao 1-1.

Mwaka 1994 ilitwaa taji hilo katika fainali zilizofanyika Kenya baada ya kuing’oa tena Uganda ambao timu yao ya taifa huiita The Cranes. Ilikuwa ni baada ya sare ya mabao 2-2 na kuingia kwenye mikwaju ya penalti  Kili Stars kushinda kwa 4-3.

Mwaka jana ilifanyika Tanzania Bara ikiwa ni mara ya pili mfululizo kuandaa fainali hizo. Haijawahi kutokea nchi moja ikaandaa fainali hizo mfululizo. Itakuwa ni mara ya saba kwa Tanzania kuandaa fainali hizo kama ilivyo kwa Uganda.

Kicheko cha Tanzania Bara kilikuwa Desemba 12, mwaka jana baada ya timu hiyo kutwaa taji na kujiona wazi ya kuwa imejitoa katika nuksi ya ‘kichwa cha mwendawazimu’.

Wageni waalikwa Ivory Coast, wakiwa na timu yenye nyota wanaokipiga ligi ya kwao, waliingia fainali na Tanzania Bara ambayo kwa mkwaju mmoja wa penalti ulifanya Watanzania kutoa uwanjani vifua mbele na chereko, nderemo na hoi hoi za kutosha.

Kipute kimerudi tena na tayari CECAFA, wametangaza kwamba michuano hiyo itaanza 25 Novemba kabla ya fainali zake kufanyika 10 Desemba, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye alisema mashindano hayo yatadhaminiwa na Kampuni ya bia ya Serengeti kupitia bia yake yaTusker iliyotoa Sh 823 milioni.

Timu 12 zinatarajiwa kushiriki michuano hiyo ikiwemo The Flames ya Malawi ambayo itacheza kwa mwaliko maalumu. Mwaka jana timu zilizoalikwa zilikuwa ni Ivory Coast na Zambia. Ndoto za Musonye kupitia michuano hiyo ni kupaa kwa soka la Afrika Mashariki sambamba na kuweka mazingira mazuri kwa timu za ukanda huu kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 zitakazofanyika Brazil.

Timu zinazotarajiwa kushiriki fainali hizo ni pamoja na Tanzania Bara, Rwanda, Ethiopia na Djibouti zinazounda kundi A wakati kundi B zimo Uganda, Burundi, Somalia na Zanzibar huku kundi C likiwa na timu za Kenya, Sudan, Eritrea na Malawi.

Timu hiyo kwa sasa itaongozwa na Mkwasa anayetoka timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ na Julio, kocha wa Coastal Union ya Tanga.

Mafanikio ya wazalendo hao huenda ikawa ni chachu ya mabadiliko ya benchi la ufundi ambalo limebebwa na wageni ambao wameshindwa kuonyesha cheche.

Mbrazil Marcio Maximo huenda akawa kwenye rekodi nzuri ya kuinoa Taifa Stars kwa kuifanikisha kucheza fainali za Kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaokipiga ligi za ndani (CHAN 2009).

Mwaka jana ilitwaa taji hilo ikiwa chini ya kocha wa Taifa Stars, Mdenishi Jan Borge Poulsen ambaye safari hii huenda akawa mtazamaji tu.

Hii ni kwa sababu kikosi chake Taifa Stars huundwa na wachezaji wanaotoka Zanzibar ambao pia ni washindani katika michuano hiyo.

Je, itarejesha italinda hadhi ya kutwaa taji hilo, tena safari ikiwa na makocha wazalendo wanaopigiwa chapuo kila uchao kuchukua timu? Bila shaka ni jambo la kusibiri na kuona kwani subira yavuta kheri.

Kwa taarifa yako tu, Kilimanjaro Stars imetwa mataji hayo kwa miaka hiyo kwa ushindi wa penalti.

0
No votes yet