Chenge ataka kuunajisi uspika


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 10 November 2010

Printer-friendly version
Tafakuri
Samwel Sitta na Andrew Chenge

TANZANIA ingekuwa ni nchi inayojali japo kwa chembe tu uadilifu, mtu kama Andrew Chenge hasingethubutu kuwania nafasi yoyote ya kuchaguliwa na wananchi. Kikubwa ambacho angelikifanya ni kuendesha biashara zake.

Lakini ni bahati mbaya kwamba chini ya mwavuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kila kitu kinawezekana. Kupitia chama hiki, unaweza kutuhumiwa kwa mambo makubwa kabisa na ushahidi wa dhahiri upo, lakini kesho unasimama jukwaani na kujinadi kwamba wewe ni mtu safi na muadilifu.

Ni ndani ya CCM tu kiongozi hapimwi kwa uadilifu wake na kujitoa kwake kuwatumikia wananchi, ila kwa nguvu za fedha zake hata kama ni chafu.

Ni ndani ya chama hicho tu umashuhuri wa mtu unanunuliwa kwa ama uwezo wake wa kukichangia fedha au mbinu zake za kufanikisha kupatikana kwa fedha kutoka kwa marafiki wake wa karibu au wa mbali. Hii ndiyo CCM ambayo Chenge pamoja na mlolongo mrefu wa tuhuma anaonekana lulu.

Chenge ni miongoni mwa wanachama wa CCM waliojitokeza hadharani kuchukuwa fomu kuwania uspika. Kisheria ana sifa ya kuwa spika. Kwa kuwa ni mwanachama wa chama cha siasa, kwa maana hiyo sifa za kisheria anazo.

Ambacho Chenge hana ni sifa mbele ya jamii. Jamii huwa haidai tu sifa za kisheria, kuna mambo mengine yanashikamanishwa na sifa za kisheria, uadilifu ni mmojawapo.

Chenge si mgeni kwa Watanzania. Huyu alikuwa mwanasheria mkuu wa serikali kwa miaka 10, mwaka 1995-2005. Chini ya Chenge ndipo taifa hili lilishuhudia uporaji mkubwa wa rasilimali za taifa chini ya sera ya kubinafsisha mashirika ya umma.

Alianza kidogo wakati awamu ya pili inafikia ukingoni, lakini alikuwa ni kiungo wa kila kilichofanywa na serikali ya awamu ya tatu. Ukizungumza mikataba ya uchimbaji madini ambayo serikali ya awamu ya tatu iliingia na makampuni makubwa ya uchimbaji huwezi kukosa jina la Chenge.

Ukitazama habari ya kutolewa bure kwa makaburu Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), huwezi kumkosa Chenge. Ukizungumza dhuluma iliyofanyiwa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ya kuporwa mchana kweupe kwa mkataba mbaya wa kuuza hisa zake kwa kampuni ya MSI/ Detecon Chenge huwezi kukosa jina lake.

Ukizungumza habari ya kununuliwa kwa rada ya bei mbaya ambayo hata hao waliotuuzia na baadaye wakubwa wao wakatuonea huruma na kufanya uchunguzi na kukuta kiasi kikubwa cha fedha kikiwa kimelipwa kama kamishieni (rushwa), mchakato wa uununuzi ulifanywa na Chenge.

Vijisenti vyake dola za Marekani 1.2 milioni ambazo zilikutwa benki katika kisiwa cha Jersey, ingawa Chenge amekuwa akikanusha mara nyingi kuwa na uhusiano na mgawo wa fedha za rada, bado hisia za wengi zimekataa kumuamini.

Chenge anadaiwa kutumbukiza kitita hicho kwenye kisiwa hicho tangu mwaka 2002, lakini hakuweza kutaja fedha hizo katika fomu za kutangaza mali ambazo kila kiongozi mkubwa wa ngazi ya Chenge hujaza na kuwasilisha kwa sekretariati ya maadili ya viongozi, hakufanya hivyo, lakini anadai yu msafi. Msafi!

Lakini hata baada ya kumaliza muda wake kama mwanasheria mkuu wa serikali na mwaka 2005 akajitosa kwenye ubunge akafanikiwa na kuwa waziri, kwanza wa ushirikiano wa Afrika Mashariki na kisha wa Miundombinu, aliwajibika vilivyo katika kufikiwa kwa mkataba baina serikali na kampuni ya RITES ya India wa kuendesha shirika la reli, TRL.

Chenge alinukuliwa na vyombo vya habari akisema “serikali ilikuwa makini kumpata RITES na kusingekuwa na matatizo yoyote katika mkataba wake” miaka miwili baadaye RITES si tu kwamba walishindwa kuendesha TRL, ila waliifikisha chumba cha wagonjwa mahututi.

Chenge hawezi kukwepa kuwa chanzo cha matatizo ya TRL. Mkataba wa TRL umefungwa Chenge akiwa waziri wa miundombinu kabla ya kujiuzulu kwa sakata la rada.

Ni vigumu kuchambua madudu ya Chenge na kuyamaliza kwa kuwa ni mengi mno, si ndani ya ofisi ya umma wala kwenye maisha yake binafsi mtaani. Itoshe tu kusema, Chenge ana mambo mengi yenye ukakasi.

Lakini pamoja na yote haya nani amguse Chenge? CCM wanamuona mali, ni mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ndani ya chama chake, ni mjumbe katika Kamati ya Maadili; ni mshauri wa mambo ya kisheria na mbunge wa chama hicho katika jimbo la Bariadi Magharibi. Ni Chenge ni Chenge ni Chenge tu.

Pamoja na historia hiyo, Chenge amejitokeza kuutaka uspika wa Bunge. Spika si mtu mdogo, huyu ni kiongozi wa moja ya mihimili mitatu ya dola. Anatazamwa kwa darubini sawa na ile ya Jaji Mkuu ambaye ni kiongozi wa muhimili wa Mahakama na Rais ambaye kiongozi wa utawala (serikali).

Chenye hasumbuliwi na historia yake na wala haoni kama anawakwaza wananchi ndiyo maana anatafuta uspika.

Kwamba anawaambia wananchi mtake msitake mimi nitakuwa kiongozi wenu, kwa kuwa naamini CCM watanipitisha kutokana na fedha zangu. Hakuna wa kunizuia.

Anatafuta uspika kwa sababu hataki Samwel Sitta, spika anayemaliza muda wake kuendelea kushikilia nafasi hiyo. Ameamua kumwandama kwa kila neno baya na ovu. Anamtuhumu kuwa chanzo cha mifarakano na migongano ndani na nje ya Bunge. Anataka kumkomesha.

Mwalimu Julius Nyerere alipata kufananisha CCM na dodoki au kokoro. Alifikia hatua hiyo baada ya kuona aina ya viongozi waliokuwa wamejichimbia madarakani ndani ya chama hicho. Mwalimu ilimuiya vigumu kuelewa inakuwaje waadilifu, wachafu na watu laghai wanakuwa pamoja katika chama kimoja na wanaelewana.

Ndiyo msingi wa kuita CCM kokoro lilolokokota kila kitu kutoka ziwani au baharini.

Sifa ya ukokoro kwa CCM ndio inatoa jeuri kwa viongozi aina ya Chenge kuthubutu kuuwaza uspika licha ya kujua kwa hakika kabisa kwamba amechafuka, amechafuliwa na hakuna mwenye ubavu wa kumsafisha.

Hata Taasisi Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) ya Uingereza, zingesimama hadharani na kusema Chenge hakuhusika katika wizi wa rada, bado wananchi watataka maelezo kwamba Chenge akiwa mtumishi wa umma amepata wapi uwezo wa kumiliki Sh. 1.5 bilioni na kuziweka bila kuzifanyia kazi?

Chenge ni lazima akumbuke kwamba mtu hatazamwi kusheria tu, bali jamii pia uangalia uadilifu wake vitu ambavyo hujumuisha mwenendo wa muda mrefu wa mtu na jamii inavyomuona.

Mtu anaweza kumpora yatima mali yake na kushinda kesi mahakamani, kisheria yu safi , likini jamii haiwezi kumkumbatia kwa sababu amekengeuka kiasi cha kukosa moyo wa huruma kutambua kwamba yatima ni wa kuonewa huruma, ni mtu dhaifu mwenye kustahili msaada.

Kiongozi katika ofisi ya umma anapimwa kisheria lakini zaidi uadilifu wake; mtu mwenye historia ya kudhulumu; kutumbukiza nchi katika matatizo; kuhusishwa na mambo machafu, inakuwa ni vigumu kuaminiwa.

Chenge ni mwanasheria, anajua jinsi ya kujiwekea kinga ili kusheria asikamatwe kwenye lolote chafu; lakini jamii inamuona kuwa mchafu, hana mamlaka ya kiuadifu kustahili ofisi kama ya spika.

Hili ndilo wabunge wanastahili kuelezwa na kutambua kwamba ni hatari kulitumbukiza Bunge kwenye mikono ya Chenge, kwa kuwa kote alikopita amecha maumivu. Ubunge aliopewa ni zaidi ya alichostahili kwa hadhi ya uadilifu wake, itoshe na aishie hapo hapo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: