Chenge kufuru tupu, amiliki bilioni 25


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 15 April 2008

Printer-friendly version
Amchotea kigogo bilioni moja
Amwashia indiketa Ben Mkapa
Andrew Chenge

WAZIRI wa Miundombinu, Andrew Chenge anaogelea katika utajiri wa zaidi ya Sh. 25 bilioni zenye utata huku Rais Jakaya Kikwete akiendelea kumkumbatia, MwanaHALISI limegundua.

Chenge amekuwa mfanyakazi serikalini kwa karibu miaka 30 na hafahamiki kuwa mfanyabiashara.

Kiwango kinachotajwa ni pamoja na fedha zilizogunduliwa na makachero wa Uingereza katika akaunti zake za nchi za nje.

Fedha zilizoko kwenye akaunti yake ya nchini, Na. 011101006950 katika benki ya NBC Limited, ni Sh. 25,794,805.89 za Tanzania hadi Ijumaa iliyopita, tarehe 11 Aprili 2008.

Katika akaunti yake ya Uswisi, ambako ana akaunti ya fedha za kigeni, Chenge amehamishia dola za Marekani 467,000, sawa na zaidi ya nusu bilioni kwa fedha za Tanzania.

Fedha za Uswisi zimelimbikizwa katika akaunti Na. 030105000364. Zilihamishwa kutoka akaunti Na. 011105011782 ya kampuni ya TANGOLD Limited, tangu 22 Februari 2006 kupitia NBC Limited.

Taarifa za kuaminika ambazo MwanaHALISI imezipata zinasema Chenge ni Mkurugenzi wa kampuni ya TANGOLD Limited ambayo ina dola 12,997,950.84 sawa na Sh. 15 bilioni za Tanzania katika NBC Limited tawi la Makao Makuu.

Aidha, kampuni hiyo inahifadhi Sh. 1,379, 359,367.39 katika akaunti Na. 011103024852 tawi hilohilo la NBC Limited.

Habari tulizopata wakati tukienda mitamboni, zinasema kwamba makachero wa Uingereza wanafuatilia uhalali wa Euro 3 milioni (sawa na zaidi ya Sh. 8 bilioni za Tanzania) zinazodaiwa kuwa Chenge alizipeleka kwenye akaunti zake nje ya nchi.

Taarifa nyingine ambazo hatukuweza kuzithibitisha haraka, zinasema Chenge alihamisha kwa mkupuo dola 600,000 za Marekani kwenda kwenye akaunti ya ofisa mwandamizi mmoja aliyekuwa Benki Kuu miaka kadhaa iliyopita, na ambaye kwa sasa anaongoza shirika la umma nchini.

TANGOLD ni kampuni ambayo inadaiwa kumilikiwa na serikali kwa asilimia 100 na ambayo inadaiwa pia kuwa ndiyo imerithi mali na madeni ya kampuni ya Meremeta Limited iliyokuwa ikijihusisha na uchimbaji madini, Buhemba, mkoani Mara.

Hata hivyo, kuna utata juu ya lini kampuni hiyo ilianzishwa nchini. Wakati aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Nazir Karamagi aliuambia Mkutano wa Tisa wa Bunge kuwa TANGOLD iliundwa mwaka 2006 kupitia Task Force maalum ya serikali, kumbukumbu zinaonyesha kuwa kampuni ilianzishwa mapema 2000 au kabla.

Hiyo inathibitishwa na ukweli kwamba tarehe 1 Januari 2000 walikuwa na akaunti ambayo haikuwa hata na senti moja katika akaunti zake mbili hadi 29 Desemba 2005 zilipoingizwa dola 13,340,168.37.

Fedha hizo zilikuwa zinatoka Hazina kupitia Benki Kuu (BoT).

Kwa akaunti ya fedha za Tanzania, tarehe 1 Agosti 2005, TANGOLD Limited ilichota kutoka Hazina kupitia BoT, Sh. 4,703,221,229.08 kwa hundi Na. 241741 na kufanyiwa uhamisho wa haraka (special clearance).

Chenge, akiwa mkurugenzi, anahusika na uhamishaji, ulimbikizaji na ulipaji wa fedha kutoka akaunti za TANGOLD.

Wakurugenzi na waidhinishaji malipo wengine wa kampuni hiyo ni, Daudi Ballali, Gray Mgonja, Vincent Mrisho na Patrick Rutabanzibwa.

Ballali alikuwa gavana wa BoT, Mgonja akiwa Katibu Mkuu Hazina, Mrisho akiwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Rutabanzibwa akiwa Katibu Mkuu Maji na Umwagiliaji.

Matumizi ya fedha kutoka akaunti hizi ambako kuna mkono wa Chenge ndiyo yanaongeza utata.

Kutoka kwenye akaunti ya binafsi ya Chenge, mamilioni ya shilingi yamelipwa kwa watu mbalimbali wakiwa ni pamoja na Janet Mashale, Mary Nchimbi, Mary Chitanda na Livingstone Ruhere.

Wengine ni Getrude Mtiga, Hawa Kiama, Leocardia Kalumuna, Athumani Sheha na David Sanga.

Miongoni mwa waliolipwa ni viongozi wa CCM, waandishi wa habari na wengine ambao hawakuweza kutambulika. Muhimu ni kwamba karibu fedha hizo zote zililipwa wakati uchaguzi wa CCM mwaka jana ambapo Chenge aliwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC). Alishinda kwa kura nyingi.

Akaunti ya TANGOLD inaonyesha kutoingiza kiasi chochote cha fedha kwa miaka mitano, kati ya Januari 2000 na Desemba 2005.

Kampuni hiyo, ilichota kutoka Hazina kupitia BoT, tarehe 29 Desemba 2005 dola 13,340,168.37 na 30 Desemba 2005 ilichota kiasi kama hicho.

Siku hiyohiyo, 30 Desemba, kampuni ilihamisha dola 13,340,168.37 na kuzipeleka mahali ambapo hapajafahamika.

Hii ni siku ambayo Rais Kikwete alizindua Bunge jipya mjini Dodoma baada ya kumalizika uchaguzi mkuu na kabla ya kuunda baraza lake la kwanza la mawaziri.

Katika uteuzi wake wa mawaziri, Chenge alipewa uwaziri wa Afrika Mashariki kabla ya mabadiliko yaliyompeleka kuwa Waziri wa Miundombinu na kurejea kwenye nafasi hiyo rais alipounda baraza jipya baada ya kulivunja kufuatia kashfa ya Richmond.

Kwa mujibu wa taarifa ilizonazo MwanaHALISI, TANGOLD ilipokea kutoka kampuni tata ya Deep Green Finance Limited Sh. 39,761,397.98 hapo 8 Oktoba 2005 wakati tarehe 10 Desemba 2005 TANGOLD ililipa Deep Green Sh. 100,940,489.71.

Wakati wa kuchezesha malipo hayo, kulikuwa na uchaguzi mkuu ambapo inadaiwa kuwa fedha hizo huenda ziliingizwa kwenye uchaguzi huo.

Kampuni ya Deep Green ndiyo ilisajiliwa na kampuni ya uwakili ya IMMA ya Dar es Salaam, ambako mtoto wa rais, Ridhiwani Kikwete na mtoto wa Rais Amani Karume, Fatma wanafanya kazi.

Ni kampuni hii mashuhuri ambayo mmoja wa waanzilishi wake ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha na mmoja wa mawakili waanzilishi, Protas Mujulizi aliteuliwa kuwa jaji wa mahakama kuu.

Kampuni ya Deep Green ndiyo imetia fora kwa viroja kwa kuonyesha kuwa ilifungua akaunti yake benki siku ya Mei Mosi wakati siyo siku ya kazi.

Tarehe 23 Novemba 2005 TANGOLD iliichotea Meremeta Sh. 555,300,040 ambazo haijulikani ni kwa kazi ipi.

Siku mbili kabla ya uchaguzi mkuu wa 2005, hapo 12 Desemba, TANGOLD iliichotea tena Meremeta Sh. 551,060,000 ambazo haijafahamika zilikuwa kwa shughuli ipi.

Kinachozidisha utata ni kwamba tangu Februari 2006 baada ya kuundwa baraza la mawaziri, akaunti ya TANGOLD ya fedha za kigeni haijalipa wala kupokea fedha yoyote hadi tarehe 31 Machi 2008 huku ikiwa na akiba ya dola 12,997,950.84 (sawa na zaidi ya bilioni 15 za Tanzania).

Wakati hali ikiwa hivyo kwenye akaunti ya nje, akaunti ya ndani ya TANGOLD imefanya malipo yamwisho 6 Juni 2006 ya Sh. 220,980,370. Hadi 31 Machi mwaka huu ilikuwa na akiba ya Sh. 1, 379,359,367.39.

Kiasi cha fedha kilicholimbikizwa kwenye akaunti za TANGOLD ambako wakurugenzi ni pamoja na Chenge na watumishi wengine wa serikali, zinalingana na kiasi ambacho serikali inapigia magoti kutoka kwa wafadhili.

Hivi sasa Chenge anachunguzwa na makachero wa Uingereza na Tanzania kuhusiana na uwezekano kuwa alipokea hongo katika biashara ya kununua rada ya kijeshi kutoka kampuni ya BAE Systems ya Uingereza.

Alipoulizwa kuhusu hali hii ya uchotaji fedha na ulimbikizaji nje, Dk. Willibrod Slaa, mbunge wa Karatu amesema, "kama hizi fedha ni za serikali kwa nini serikali igeuke ombaomba wakati zimelala benki?"

Kwa nini umma usiamini kuwa fedha hizo zimo mikononi mwa mtandao wa kifisadi, anahoji Dk. Slaa na kuongeza, "Kigugumizi cha serikali kinatoka wapi hapa wakati fedha hizi zinatosha kujenga madarasa 400 ya sekondari au wastani wa shule moja kwa kila mkoa."

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: